BALOZI wa China, Lu Youqing, amesema mpaka kufikia mwaka jana nchi yake
ilikuwa imetoa ajira 150,000 kwa Watanzania baada ya kufanya uwekezaji
wa dola za kimarekani bilioni 6.62 (sawa nash. trilioni 14.6).
Balozi Youqing aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa halfa
ya utoaji wa zawadi kwa wafanyakazi wa kampuni za kichina na wanafunzi
bora waliohudhuria programu ya mafunzo ya Tarajali kwenye kampuni za
Kichina.
Alisema nchi yake imefanya uwekezaji huo kwamba zaidi ya Watanzania
350,000 pia wanafanya biashara kati ya China na Tanzania ikiwa ni sehemu
ya kukuza uchumi na kuongeza maendeleo ya nchi.
“Kampuni nyingi za Kichina zimewekeza nchini Tanzania na zimeleta fedha,
teknolojia na uzoefu wa utawala ambao unahitajika sana hapa Tanzania na
pia zimefanikiwa kuzidisha maendeleo ya kiuchumi na uboreshaji wa
kijamii nchini Tanzania,” alisema balozi huyo.
Balozi Youqing alisema Tanzania imeweka uzito katika suala la uboreshaji
wa miundombinu na ujenzi wa viwanda kama mkazo wa kutimiza lengo la
kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Alisema kuwa jambo hilo linahitaji kuongezeka kwa kasi ya kufundisha
wafanyakazi wenye ujuzi bora ili kufikia malengo ya uchumi wa kati.
“(Hivyo) tulizitaka kampuni za kichina nchini Tanzania kuandaa shindano
la ujuzi wa wafanyakazi Watanzania na programu ya mafunzo ya Tarajali
kwa wanafunzi Watanzania,” alisema.
Aidha alisema nchi yake ina mkakati wa kuisaidia Tanzania kujenga kituo
cha mafunzo ya kiufundi ili kutoa programu za mafunzo ya kina kwa
wafanyakazi Watanzania na kufundisha wanafunzi wengi wenye ujuzi bora
kwa maendeleo ya viwanda vya Tanzania.
Alisema wanafunzi waliopatiwa zawadi pamoja na wafanyakazi wamekuwa ni
mfano bora kwa wachina na Watanzania kwenye kusaidiana na kubadilishana
uzoefu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi Tanzania
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. John Jingu alishukuru
kuanzishwa kwa shindano hilo kwani limesaidia kuwajenga wanafunzi hao
kiuwezo na kiuchumi.
“Mafunzo waliyoyapata yataongeza ufanisi kwani vijana wetu wamejifunza
umuhimu wa kufanyakazi kwa bidii kama inavyosisitizwa na Rais John
Magufuli,” alisema Dk. Jingu.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment