Ripoti ya Shirika la Amnesty International imebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokiuka haki za binadamu kwa kiasi kikubwa kutokana na dosari za kiutawala, ikiwamo kuzuia uhuru wa kujieleza, mikutano ya kisiasa na ukandamizwaji wa vyombo vya habari.
Ripoti hiyo ya mwaka 2016/17, imetoa tathmini juu ya hali ya haki za
binadamu duniani ikihusisha mataifa yote makubwa na madogo na kueleza
mambo kadhaa yaliyojitokeza kinyume cha misingi ya demokrasia na utawala
bora.
“2016 ulikuwa ni mwaka uliotawaliwa na tabu na hofu miongoni mwa watu
baada ya Serikali na makundi yaliyojihami kwa silaha (armed groups)
kukiuka haki za binadamu kwa namna nyingi,” inaeleza ripoti hiyo
iliyotolewa na katibu mkuu wa Amnesty International, Salil Shetty.
Dosari hizo zimeonekana katika nchi mbalimbali duniani ikiwamo Afrika
Kusini, Kenya, Rwanda, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja
na mataifa makubwa ikiwamo Marekani iliyoshutumiwa kwa ubaguzi.
Kwa upande wa Tanzania, ripoti hiyo ilizungumzia juu ya machafuko
yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Zanzibar ambapo vurugu zilisababisha
majeraha kwa watu 200, huku 12 wakinyanyaswa kijinsia na mmoja kubakwa.
Kasoro nyingine zilizotajwa katika ripoti hiyo ni vyombo vya usalama
ikiwamo polisi kutumia nguvu dhidi ya vyama vya upinzani katika kuzuia
maandamano na mikutano.
Shirika hilo limeripoti juu ya kile kilichotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu
wa Zanzibar 2015 na kuelezwa kuwa CUF ilipinga uhalali wa matokeo baada
ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein kushinda na wanachama
zaidi ya 100 walikamatwa na vyombo vya dola.
Hata hivyo, baada ya uchaguzi huo malalamiko hayo yalipingwa kwa madai
kuwa hakukuwa na kasoro na hakuna mashtaka yaliyofikishwa juu ya Jeshi
la Polisi.
Kuzuiwa kwa mikutano.
Pia, ripoti hiyo imeeleza kuwa Rais John Magufuli alipiga marufuku
mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020 na upinzani ulianzisha kampeni ya
kupinga agizo hilo, suala lililosababisha polisi kuongeza nguvu zaidi
hadi kuzuia mikutano ya ndani iliyofanywa na vyama vya siasa.
“Viongozi wawili wa upinzani pamoja na wafuasi 35 kutoka Bara na
Visiwani walikamatwa na kuhojiwa kwa makosa mbalimbali ikiwamo kupinga
uchaguzi huo,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Uhuru wa habari
Kuhusu uhuru wa habari, ripoti hiyo imeelezea juu ya kufungiwa kwa
baadhi ya vyombo vya habari, huku baadhi ya waandishi wakituhumiwa kwa
madai ya uchochezi kwa mujibu wa Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015 na
Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Ripoti hiyo imevitaja vyombo hivyo kuwa ni gazeti la Mawio ambalo
lilifungiwa pamoja na waandishi wake kushtakiwa kwa madai ya uchochezi
baada ya kuripoti juu ya uchaguzi wa Zanzibar.
Pia, gazeti la Mseto lilifungiwa kwa miaka mitatu kwa kuchapisha makala
juu ya rushwa huku Redio Magic na Radio Five zikifungiwa kwa muda.
Ripoti hiyo imesema wanawake wawili na wanaume sita walishtakiwa chini
ya Sheria ya Mtandao kwa kutuma taarifa mitandaoni zilizohusu uchaguzi
na zingine kumhusu Rais kupitia mtandao wa Facebook.
Haki za wanawake.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa Tanzania imeshindwa kutekeleza mapendekezo ya
Kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) kumaliza ubaguzi dhidi ya wanawake
ikiwamo haki ya kurithi mali.
Imegusia Sheria ya Ndoa katika kifungu namba 13 na 17 vinavyoruhusu
mwanamke chini ya miaka 18 kuolewa kinyume na haki za binadamu na
kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kiwango kikubwa cha ndoa
za utotoni.
Wadau wanasemaje?
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen
Kijo-Bisimba alisema kuwa taarifa hiyo ni sahihi kufuatia hali
iliyokuwapo mwaka uliopita, hususan kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa na
kupingwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.
Alisema kuwa kinachotakiwa ni wananchi wenyewe kutambua mamlaka
waliyonayo dhidi ya watawala wao na kupaza sauti pale kunapokuwa na
ukiukwaji wa haki au sheria.
Pia, aliwataka washauri mbalimbali wa viongozi wa juu serikalini akiwamo
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutumia nafasi zao kuwasihi kufuata
misingi ya sheria katika kuongoza Taifa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema
ripoti hiyo inapaswa kutumika kusahihisha mahali ambapo pameleta dosari
na kuzingatia misingi ya demokrasia katika utawala.
“Rais aangalie upya uamuzi wake, pengine alitaka kunyoosha pale ambapo
hapakuwa sawa, lakini ameshakaa zaidi ya mwaka mmoja na sasa tunaweza
kurudi katika demokrasia, “ alisema.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment