Marekani na Korea Kaskazini zimeendelea kujibizana vikali, ambapo safari
ya meli za kivita za Marekani ikiwemo meli yenye uwezo wa kubeba ndege
za kivita ya Carl Vinson imeibua hisia kubwa na uwezekano wa Marekani
kufanya shambulio la mapema kujaribu kulemaza mfumo wa kijeshi wa Korea
Kaskazini.
Wakati taarifa hizo zikienea, imebainika kwamba meli hizo za kivita za
Marekani hazikuwa zinaelekea upande wa Korea Kaskazini kama
ilivyoripotiwa awali, bali zilikuwa zinaelekea eneo tofauti.
Awali iliripotiwa kuwa, Jeshi la wanamaji la Marekani lilikuwa
likielekea Korea kama hatua ya kuionya Korea Kaskazini, ambapo Rais
Trump pia alitangaza kwamba kundi kubwa la meli za kivita lilikuwa
likitumwa eneo hilo, hivyo imebainika kuwa si kweli.
Hadi kufikia mwishoni mwa wiki, meli hizo zilikuwa zimesafiri mbali sana
na rasi ya Korea na zilikuwa zinapitia mlango wa bahari wa Sunda
kuingia katika Bahari ya Hindi.
Wakuu wa jeshi la wanamaji la Marekani katika Bahari ya Pasifiki
walisema Jumanne kwamba walikuwa wamefutilia mbali safari ya meli hizo
katika bandari ya Perth.
Kundi hilo la meli sasa "linaelekea Magharibi mwa Pasiki kama lilivyoamrishwa".
Bado haijabainika iwapo kulitokea sintofahamu katika mawasiliano au
labla Marekani ilipotosha watu makusudi kujaribu kumtia wasiwasi
kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.
Aidha, Marekani imesema Korea Kaskazini ilipotekeleza jaribio la kombora
ambalo lilifeli mwishoni mwa wiki ilikuwa na nia fulani ya kiuchokozi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis amesema Marekani inafanya
kazi kwa karibu na China kukabiliana na Korea Kaskazini. Amesema kuwa
jaribio hilo lililofanywa na Korea Kaskazini lilikuwa la kutojali na
ilifanya hivyo kwa kuichokoza Marekani.
Aidha, Korea Kaskazini wamesema kuwa itafanya majaribio ya makombora
kila wiki na pia ikaonya kwamba kutatokea vita kamili iwapo Marekani
itaichukulia hatua za kijeshi.
“Iwapo Marekani wanapanga kutushambulia, tutajibu kwa shambulio la
nyuklia kwa mtindo na njia yetu wenyewe,” amesema Naibu waziri wa mambo
ya nje wa Korea Kaskazini, Han Song-ryol
Pande zote mbili zimekuwa zikijibizana vikali baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio hilo la makombora.
Bw Mattis alisema kwamba jaribio hilo la Jumapili halikuhusisha kombora
linaloweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine lakini bado lilikuwa
ishara ya kutojali.
“Inadhihirisha ni kwa nini tunafanya kazi kwa karibu kwa sasa na
Wachina…tunajaribu kudhibiti hali hii na lengo letu ni kumaliza silaha
za nyuklia katika rasi ya Korea,” alisema.
Credit:BBC
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment