Thursday, 13 April 2017

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Yasema Nafasi ya Sophia Simba Iko Wazi na Itajazwa Hivi Karibuni.Fahamu zaidi hapa.

Tume  ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza nafasi ya ubunge wa Viti Maalumu iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba, ambaye alifukuzwa uanachama hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Semistocles Kaijage, ilieleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343,  Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa baada ya Sophia kufukuzwa uanachama wa CCM Machi 11, mwaka huu, nafasi hiyo  yake bungeni iko wazi.

Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 67 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili mtu ateuliwe au achaguliwe katika nafasi ya ubunge, ni lazima awe mwanachama aliyependekezwa na chama chake husika cha siasa.

“Kwa kuwa Sophia Simba amefukuzwa uanachama wa chama kilichomdhamini, Ibara ya 67 (2) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaelekeza kuwa amepoteza sifa za kuteuliwa au kugombea ubunge.

“Kutokana na kuwepo kwa nafasi wazi ya ubunge wa Viti Maalumu, taratibu za kujaza nafasi hiyo zinaendelea kwa kuzingatia kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343,” alisema Kaijage.

Sophia na wenzake saba walifukuzwa uanachama baada ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa CCM Machi 11, mwaka huu mjini Dodoma huku wengine wakipewa onyo kali.

Waliopewa adhabu sambamba na Sophia ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, Jesca Msambatavangu (Iringa), huku Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Emmanuel Nchimbi akipewa onyo kali kwa kosa la kukisaliti chama wakati wa mchakato wa uteuzi wa mgombea urais mwaka juzi.



Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment