WAKATI bei ya unga wa sembe ikipanda mpaka kufikia kuuzwa kati ya
Sh. 2,200 na Sh. 2,500 kwa kilo, ile ya mfuko wa saruji wenye uzito wa
kilo 50 imeshuka hadi sh. 9,000, sawa na Sh. 180 kwa kilo.
Katika masoko na maduka mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ambayo
Nipashe ilitembelea jana, bei ya sembe ilikuwa ikiuzwa kwa kiasi hicho
kwa rejareja huku wauzaji wa jumla wakiuza kiroba cha kilo 50 kwa kati
ya sh.100,000 na sh.98,000.
Ibrahim Omary, mfanyabiashara wa Kariakoo alisema anauza unga wa
sembe kwa Sh. 2,400 kwa kuwa hununua kwa bei kubwa kutoka kwa
wazalishaji.
Alisema kampuni inayojulikana kwa jina la Mkulima huwauzia unga huo
kwa Sh. 98,000 na Mama Neema huwauzia kwa sh. 100,000 kwa kiroba cha
kilo 50.
Kwenye baadhi ya maduka ya kula ya Kinondoni, unga umekuwa ukiuzwa
kati ya Sh. 2,200 na Sh. 2,500. Tandika bei ya wastani ni Sh. 2,200,
Mwenge Sh. 2,400, Kimara sh. 2,500 na Yombo Vituka sh. 2,200.
Nipashe ilitembelea mashine zinazozalisha sembe katika eneo la
Tandale ambako bei ya jumla kwa mfuko wa kilo 50 ni kati ya Sh. 92,000
na Sh. 94,000 huku kilo ya mahindi ikiuzwa kati ya sh. 1,300 na 1,500.
Baadhi ya wateja walikuwa wakilalamika gharama hizo za unga huku
wakieleza kuwa kwa sasa wamepunguza matumizi ya unga wa sembe na kuamua
kutumia mchele.
Janeth Masawe, mkazi wa Mwenge alisema kwa sasa wamekuwa hawanunui
unga wa sembe mara kwa mara kama ilivyokuwa zamani kwa kuwa sembe
inazidi gharama ya mchele.
“Bora ninunue mchele… maana naweza kupata mchele kwa sh. 1,800 kwa
kilo lakini unga wa sembe ni mpaka niwe na sh. 2,400,” alisema.
Kupanda kwa bei ya unga kumetokana na kupanda kwa bei ya mahindi
kulikosababishwa na uhaba wa chakula hicho kutokana na ukame ambao
ulikumba maeneo mengi ya nchi kabla ya mvua za masika zilizoanza mwezi
uliopita.
Gunia moja la mahindi linauzwa kwa bei ya wastani wa Sh. 112,000
kwa sasa katika maeneo ambayo ni chanzo kikuu cha zao hilo, uchunguzi wa
Nipashe umeonyesha.
TWIGA JENGA
Tangazo kwa wafanyakazi wote lililotolewa na kiwanda cha saruji cha
Twiga Jumatano wiki hii, lilibainisha kuwa mauzo ya mfuko mmoja wa
Twiga Jenga kuwa sh. 9,000, Twiga Extra sh. 9,500 na sh. 10,000 kwa
Twiga Plus.
Tagazo hilo lililoandikwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Jesse
Shuma, lilitaka kuwaarifu wafanyakazi hao kuwa saruji “inauzwa kiurahisi
na kwa bei nafuu katika eneo letu la maegesho ya magari lililoko
Kizuga, nje ya kiwanda.”
“Tafadhali mjulishe mfanyakazi mwenzako, rafiki, ndugu na jamaa.
“Wote mnakaribishwa.”
Kuporomoka kwa bei ya saruji ambayo miaka miwili iliyopita ilikuwa
ikiuzwa sh. 15,000 kwa mfuko wa kilo 50, kwa kiasi kikubwa kumetokana na
ufunguzi wa Kiwanda cha Dangote mkoani Mtwara.
Kwa mujibu wa tovuti ya serikali ya mkoa wa Mtwara, “kiwanda hiki
ni kikubwa kuliko vyote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati” na
kina uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu za saruji kwa mwaka.
Kilianza uzalishaji rasmi Septemba, mwaka jana, baada ya uwekezaji wa dola za Marekani milioni 500 (sawa na Sh. trilioni 1.1).
Credit – Nipashe
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment