Tuesday 23 February 2016

#YALIYOJIRI>>>Wizara Ya Fedha Yasema Makusanyo Ya Fedha Kwa Mwezi Yamefika Trilioni 1.79,Mchanguo Wote Wa Matumizi wa Pesa Uko Hapa.Fahamu zaidi hapa.

SERIKALI imeendelea kupaa katika ukusanyaji wa mapato baada ya kukusanya hadi Sh trilioni 1.79, ambazo imezipeleka katika huduma za jamii, ikiwamo elimu, maji, miundombinu na miradi ya maendeleo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya hali ya mapato kwa kipindi cha Februari mwaka huu. 

Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata alisema makusanyo yameongeza kutoka Sh trilioni 1.2 Desemba hadi Sh trilioni 1.79 Januari.

Kabla ya Oktoba mwaka jana, makusanyo hayo hayakuzidi Sh bilioni 900 kwa mwezi.

Dk Likwelile alitaja maeneo ambayo fedha hizo zimeelekezwa ni kwa Mamlaka ya Elimu (TEA) iliyopewa Sh bilioni 23.078; Sh bilioni 18.7 zinatekeleza utoaji wa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za awali, msingi hadi kidato cha nne kwa ajili ya ada, chakula na ruzuku.

Aidha, Sh bilioni 13 zimeelekezwa kwenye mikopo ya elimu ya juu na Sh bilioni moja zitatumika kujengea uwezo walimu walio masomoni na wakufunzi wao. 

Pia Sh bilioni mbili zimeelekezwa kupanua udahili katika mkoa wa Dar es Salaam kama Rais John Magufuli alivyoahidi katika mkutano wake na wazee wa mkoa huo.

Dk Likwelile alitaja maeneo mengine yaliyonufaika na fedha hizo na shilingi kwenye mabano ni Mpango wa Maji Vijijini (bilioni 17.1), maendeleo ya ujenzi wa barabara (bilioni 58.8), miradi ya umeme vijijini (bilioni 20.2), reli (bilioni 2.034) Serikali za Mitaa (bilioni 4.5), na Mahakama zimepatiwa Sh bilioni 12.3.

Aidha, Dk Likwelile alisema ili kuwajengea uwezo walimu walio masomoni na wakufunzi wao, Wizara imetoa Sh bilioni 1.65 kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Kati ya fedha hizo, wakufunzi wamepatiwa Sh milioni 431.6, walimu walio masomoni wametengewa Sh milioni 249.2 kwa ajili ya vifaa vya kufundishia, posho na nauli.

Alisema kuwa fedha nyingine kati ya hizo, kiasi cha Sh bilioni 573.7 zimetolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma na ulipaji wa deni la taifa kwa mwezi huu zimetolewa Sh bilioni 842.1 na mifuko ya hifadhi za jamii Sh bilioni 81.13.

Aidha kiasi kilichotolewa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ni Sh bilioni 166.2 huku Chuo kipya cha Sayansi ya Tiba kilicho katika hatua ya ujenzi cha Mloganzila huko Kibamba, nje ya Jiji la Dar es Salaam, kimepatiwa Sh bilioni 18 .
 Kaimu kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Alfayo Kidata akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Tarishi Kibenga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata akifafanua kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam jinsi Mamlaka hiyo ilivyofanikiwa kukusanya mapato kutoka trilioni 1.2 kwa mwezi Disemba mpaka trilioni 1 na bilioni 79 kwa mwezi Januari

0 comments:

Post a Comment