Monday 30 November 2015

#YALIYOJIRI>>>Profesa Lipumba Akutana na Rais John Magufuli Ikulu Dar es Salaam.Fahamu zaidi hapa.

  Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Prof Ibrahim Lipumba amemtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli na kumpongeza kwa hotuba nzuri iliyoweka mwelekeo mpya wa Serikali ya Awamu ya Tano. Pia Prof Lipumba amesifu na kuunga mkono Juhudi za Mhe Rais katika kupambana na wakwepa kodi na wahujumu uchumi.
Hii hapa pia taarifa kutoka Ikulu kuhusu mwaliko wa Prof. Lipumba ndani ya Ikulu.

#YALIYOJIRI>>>Chama cha Mapinduzi CCM yakanusha Zilizosambaa Kwamba Imekubali Kumkabidhi Maalim Seif Ikulu.Fahamu zaidi hapa.

Chama cha Mapinduzi CCM kimekanusha Taarifa iliyozagaa katika Mitandao ya Kijamii kwamba Chama hicho kimeridhia aliyekuwa Mgombea wa Urais wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akabidhie nchi kuiongoza kwa miaka mitano. 

Akikanusha Taarifa hiyo mbele ya Waandishi wa Habari Afisini kwake Kisiwandui Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai amesema taarifa hiyo ni uzushi uliotungwa ili kuwatia taharuki WanaCCM na Wananchi kwa Ujumla. 

Amesema toka kusambaa kwa Taarifa hiyo Jana amekuwa akipigiwa simu na Watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kujua ukweli wa Taarifa hiyo hasa ikizingatiwa kuwa ilidaiwa kusainiwa na Naibu huyo. “Huu ni Uzushi Mkubwa na kwamba unafaa kupuuzwa maana hauna lengo jingine zaidi ya kuwagawa WanaCCM” Alismema Vuai. 

Amesema kilichopo nikwamba CCM inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa Marejeo kama ambavyo Tume ya Uchaguzi ilitangaza kuufuta Uchaguzi na hivyo kurudiwa upya. Aidha Vuai amesema kuwa tayari wamewasiliana na Wanasheria wao pamoja na wataalamu mbalimbali ili kuwabaini waliohusika kusambaza Taarifa hizo na kuwapeleka katika Vyombo vya Sheria. 

“Tumeshafanya mawasiliano na Wataalam wetu na tukiwabaini Sheria ya Makosa ya mtandao itachukua nafasi yake” Alisema Vuai. 

Katika taarifa hiyo iliyosambaa na kudai kusainiwa na Vuai Ali Vuai ilisema kuwa Chama cha mapinduzi kimeridhia na kukubali kumpa nchi Maalim Seif Sharif kupitia chama chake cha Cuf kuwa ndio rais wa uchaguzi ulopita,na yeye ndio atakayeongoza serikali ya umoja wa kitaifa. 

Taarifa hiyo ilieleza kuwa CCM imekubali kushirikiana na maalim Seif katika kuongoza nchi chini ya serikali ya umoja wa kitaifa na kukubali kutoa makamo wa kwanza wa rais na nusu ya mawaziri.
 
Vuai amerejea kauli yake kuwa mazungumzo yanayofanywa na Viongozi wa Kitaifa kwa kushirikiana na Viongozi Rais Wastaafu wa Zanzibar hayawezi kubatilisha maamuzi ya Tume ya kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita. 

#YALIYOJIRI>>>Upotevu wa Makontena 349 Bandarini: Watu 12 Watiwa Mbaroni na Jeshi la Polisi.Fahamu zaidi hapa.

Kufuatia agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa la kuwataka watuhumiwa wa wizi wa makontena 329 katika bandari ya Dar es salaam kuchukuliwa hatua na Jeshi la Polisi, tayari Jeshi hilo limewashikilia watuhumiwa kumi na mbili wanaohusika na wizi huo.

Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam,  Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CP) Diwani Athumani amesema kuwa, uchunguzi unaofanywa na wataalamu waliobobea katika makosa ya uhalifu wa kifedha umeweza kuwabaini watu kumi na mbili  ambao wamehusika na wizi huo.

“Kati ya watuhumiwa hao kumi na mbili, watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na saba bado wapo katika upepelezi na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Athumani.

Wanaoshikiliwa kutokana na tuhuma mbalimbali ni Kamishna wa Idara ya Forodha na Ushuru TRA Bw. Tiagi Masamaki, Meneja Kitengo cha Huduma za Ushuru  na Bi.  Habib Mponezia, Msimamizi Mkuu wa Kitengo cha Ushuru wa Forodha.

Watuhumiwa wengine ni pamoja na Bi. Eliaichi Mrema, Msimamizi Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta  Bw. Haroun  Mpande na Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara Bw. Hamis Omary.

Aidha Kamanda Athumani amewaomba wananchi wenye taarifa za ubadhilifu wa mali za Umma kuendelea kulisaidia Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yake.

#YALIYOJIRI>>Rais John Magufuli Akutana na Mabolozi Wa China na Korea Kusini,Ahakikishiwa Ujenzi wa Daraja la Salender Dar-es-salaam.Fahamu zaidi hapa.

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing, Ikulu jijini Dar es salaam leo Novemba 30, 2015.
 Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing, Ikulu jijini Dar es salaam leo Novemba 30, 2015.
Vichwa vya habari za siasa Tanzania bado vinaendelea kubeba stori kila mara kuhusu Rais John Maguful. inawezekana ni kawaida kabisa kila siku kukutana na habari zaidi ya tatu au nne kuhusu Rais John Maguful tangu siku ya kwanza alipoapishwa na kuanza kazi ya Urais wa Tanzania.
 
Ninayo nyingine kutoka Ikulu sasahivi, hii inahusu Rais John Maguful kumuaga Balozi wa Korea Kusini, Chung IL ambapo Balozi huyo amemhakikishia Rais Magufuli kwamba daraja hilo litajengwa kwa ufadhili wa Serikali yake.
 

#YALIYOJIRI>>>Serikali ya Tanzania Yazungumzia Tishio la Marekani Kusitisha Misaada Tanzania.Fahamu zaidi hapa.

Serikali imezungumzia tishio la Serikali ya Marekani la kusitisha misaada kwa Serikali ya Tanzania kutokana na mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kukamatwa kwa maofisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

Ofisi ya Ikulu jana ilisema masharti yaliyotolewa na Serikali ya Marekani yanatekelezeka na yatamalizwa kabla ya kikao cha Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) kukaa Desemba, mwaka huu.

Wiki iliyopita, Serikali ya Marekani iliitaka Serikali ya Tanzania kumaliza haraka mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, vinginevyo upo uwezekano wa kusitishwa msaada wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 472 (Sh. bilioni 999.4), za awamu ya pili ya fedha za MCC la nchi hiyo.

Fedha hizo za MCC awamu ya pili ni kwa ajili ya kuiwezesha Tanzania kusambaza umeme na kuwaunganisha wananchi wengi katika Gridi ya Taifa na uimarishaji wa taasisi zinazohusika na na sekta ya nishati.

Mambo ambayo Serikali ya Marekani iliitaka Tanzania kumaliza haraka ni suala mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar pamoja na kupata ufafanuzi wa watuhumiwa waliokamatwa kwa makosa ya mtandaoni, wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana alisema suala hilo haliisumbui serikali na ni tatizo dogo  ambalo linatatuliwa.

Alisema serikali ina uhakika wa kumaliza masuala hayo kabla ya kikao hicho cha Bodi ya MCC kukaa ambao masuala hayo yatakuwa yameshatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Alisema Bodi ya MCC ilikaa kikao chake cha kwanza Septemba, mwaka huu na inatarajia kukaa tena kikao chake Desemba, mwaka huu.

Alisema serikali ina uhakika Bodi ya MCC ikikaa kikao cha  Desemba, mwaka huu itapitisha pasipo na shaka yoyote.

Aliongeza kuwa suala la sheria ya makosa mtandaoni, kuna watu walikamatwa na watafikishwa mahakamani ambapo mahakama yenyewe ndiyo itakayotoa hukumu na kama wana makosa watahukumiwa na kama hawatakutwa na makosa basi wataachiwa huru.

Balozi Sefue alisema suala hilo ni la kisheria, watu wametuhumiwa na wamepelekwa mahakamani ambako itaamua.

Kuhusu mgogoro wa Zanzibar, Balozi Sefue alisema kuna vikao vinavyoendelea vya kupata muafaka na mgogoro huo nao utamalizwa kwa haraka zaidi.

Marekeni ilieleza kuwa mambo hayo iliyotaka ipatiwe ufumbuzi, yataiwezesha MCC kuipima Tanzania katika sifa za kupata fedha hizo.

#Breaking News>>Sheikh Ponda Aachiwa Huru.Fahamu zaidi hapa.

Mahakama ya hakimu mkazi Morogoro imemuachia huru Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda aliyekuwa akituhumiwa kwa makosa ya uchochezi baada ya mahakama kutoridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka na hivyo kuonekana hana hatia
 Historia ya kesi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda.

Hati ya Mashitaka ya Kesi hiyo ilikuwa na jumla ya Mashitaka matatu  lakini Julai 22 mwaka 2015, Hakimu Mkazi Mary Moyo  alitoa  uamuzi wa kumfutia shitaka la kwanza kwasababu lilishatolewa uamuzi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, na hivyo mahakama hiyo ya Morogoro siku hiyo ilitoa uamuzi wa kumuona ana kesi ya kujibu  katika mashitaka mawili yaliyosalia ambalo ni kosa la pili na la tatu .

Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro  ilimfungia dhamana Sheikh Ponda baada ya kukubaliana na hati ya aliyekuwa  Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), wakati huo Dk.Eliezer Feleshi ambaye kwasasa ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam liloomba Mahakama hiyo imfungie dhamana mshitakiwa huyo chini ya Kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai ya Mwaka 2002.

Hatua hiyo ya kufunguliwa kesi katika Mkoa wa Morogoro ilikuja ikiwa ni muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Agosti 19 Mwaka 2013 saa Tatu asubuhi,  kumfutia kesi ya jinai  Na.144/2013 katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano baada ya DPP kudai kuwa hana nia ya kuendelea kumshitaki katika kesi hiyo No.144/2013  kwa mujibu wa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Hata hivyo baada ya hakimu Liwa kumwachilia huru,Ponda ambaye aliletwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi na wanausalama wa polisi na magereza chini ya ulinzi mkali, alikamatwa tena na kupakizwa kwenye magari ya wanausalama hao ambapo baadhi ya wanausalama hao walisema kuwa wanampeleka Ponda mkoani Morogoro kwaajili ya kumfunguliwa makosa matatu ya uchochezi, kufanya mkusanyiko haramu na kisha akarejeshwa gereza la Segerea Dar es Salaam , lakini baadae Uongozi wa Jeshi la Magereza uliamua kumuamisha Ponda kutoka Gereza la Segerea na kumuamishia Katika Gereza Moja Mkoani Morogoro.

Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, baada ya kuwasili kwa helikopta ya Jeshi la Polisi katika uwanja wa gofu mjini Morogoro.

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate, Mwanasheria Kiongozi  wa Serikali, Bernard Kongola, alidai  kuwa Agosti 10, mwaka 2013, katika eneo la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Morogoro, Ponda aliwaambia Waislamu wasikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwa madai kuwa zimeundwa na BAKWATA, ambao ni vibaraka wa CCM na serikali.

Alidai kuwa Sheikh Ponda ambaye anatetewa  na wakili wa kujitegemea Juma Nassor aliwaagiza waumini hao kuwa endapo watu hao watajitokeza kwao na kujitabulisha kwamba ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha wawapige.

Ilielezwa kuwa kauli hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, mwaka 2010, ambayo ilimtaka Ponda ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani na Kuwa Raia Mwema.

Katika shitaka la pili, Kongola alidai kuwa Agosti 10, mwaka huu, katika eneo la Uwanja wa Ndege, Morogoro, Ponda aliwaambia Waislamu kuwa serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi ili kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi hao ni Waislamu.

Kwamba, Ponda aliwaambia wafuasi wake kuwa serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wa huko ni Wakristu.

Shitaka la tatu ambalo linafafana na lile la pili, ambalo nalo linadaiwa kutendwa Agosti 10, mwaka huu, ambapo kauli ya Ponda inadaiwa kuumiza imani za watu wengine kinyume cha kifungu cha sheria namba 390 na kanuni ya adhabu namba 35 cha mwaka 2002.

Oktoba 18 mwaka 2012, Ponda na wenzie 49 walifikishwa Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa Mara ya kwanza   wakikabiliwa na makosa matano, kosa la kwanza ni la kula njama, kujimilikisha mali, kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang'ombe  Markas,wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh. Milioni 59 na kosa la uchochezi ambapo katika kesi hiyo Jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa na wakili Mwandamizi wa Serikali , Tumaini Kweka .
 
Mahakama pia iliwafunga dhamana ya Ponda na mshitakiwa wa pili tangu 0ktoba 18 Mwaka 2012 hadi siku Kesi hiyo iliyotolewa hukumu Mei 9 Mwaka 2013.

Mei 9 mwaka 2013 Hakimu Mkazi Victoria  Nongwa akitoa hukumu yake katika kesi hiyo ya Ponda na wenzake alisema anawaachiria huru washitakiwa 49  kwasababu upande wa jamhuri  umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi yao na kwamba anamtia hatiani Ponda kwa kosa moja tu  la kuingia kwa jinai na kwamba na anamuachiria huru katika makosa manne yaliyosalia kwasababu pia jamhuri ilishindwa kuthibitisha mashitaka hayo dhidi ya Ponda.

Sheikh Ponda alikata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mei 9 mwaka 2013 ambapo alishinda rufaa yake.

Hata hivyo siku Chache baada ya Kufungwa Kifungo hicho cha nje Mei 9 mwaka 2013, Ponda alikwenda Mkoani Morogoro na kufanya mkutano ambao alidai wa Kutenda makosa ya jinai ambao alikamtwa  Agosti Mwaka 2013 na kuwekwa chini ya ulinzi na kufunguliwa Kesi Mahakama ya Kisutu Na.144/2013 ikafutwa na DPP na ndipo akafunguliwa kesi hiyo Mkoani Morogoro ambayo imetolewa hukumu Leo na kuachiwa huru.

Saturday 28 November 2015

#YALIYOJIRI>>>Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kufungua duka lake kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jumatatu wiki ijayo.Fahamu zaidi hapa.

Medical Store Department of Tanzania (MSD) imeanza kutekeleza kilichosemwa na Rais John Magufuli utaratibu wa kufungua maduka matibabu katika hospitali za serikali, kwa kuanzia na Hospitali ya Taifa Muhimbili Jumatatu ijayo.

MSD Mkurugenzi Mkuu, Laurean Bwanakunu walisema kuwa mikakati tayari kuweka kwa ajili ya kufungua maduka na kwamba wao kwa sasa ni kutafuta kibali cha hospitali, maeneo ya kujenga maduka na kanuni nyingine ya kuweka kwa ajili ya kuanza duka matibabu.

Muhimbili usimamizi alitupa kibali na sasa sisi ni kukamilisha hatua ya mwisho ya kufungua duka juu ya Jumatatu, alisema.

Alisema kuhifadhi itakuwa na dawa zote ambazo ziko na bima ya afya na kutoa huduma kwa wateja wote walihudhuria katika hospitali na wale wa kutoka hospitali za nje.

Bwanakunu pia alisema kuwa baada ya Muhimbili, duka la pili yatafunguliwa Mbeya.

Mapema mwezi huu, baada ya ziara ya kushitukiza Rais  Magufuli katika MNH, aliamuru MSD kwa maduka katika hospitali kufungua akisema maduka binafsi ambayo ni kazi kuzunguka hospitali ni kuuza madawa katika bei ya juu.


#YALIYOJIRI>>>"Dili Limebumbulika"Magogo ya Milioni 300 Yakamatwa Bandarini Yakipelekwa Nchini China Kinyemela.Fahamu zaidi hapo.

Kontena 37 zenye shehena ya magogo aina ya mninga yenye thamani zaidi ya Sh. milioni 300 zimekamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea nchini China bila kibali.
Katika shehena hiyo, kontena 31 zimekamatiwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kati ya hizo mbili zimekamatwa mkoani Mbeya,  na mikoa ya Rukwa na Pwani katika maeneo ya Kibaha na Kongowe, kontena moja kila sehemu na Mbezi ya jijini Dar es Salaam, pia imekamatwa kontena moja na kufanya idadi ya kontena zilizokamatwa kufikia idadi 37.

Kontena hizo zinazodaiwa kutoka nchini Zambia, zimekutwa hazina kibali cha usafirishwaji na kusababisha serikali kupoteza mamilioni ya fedha. 
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam jana,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru, alisema kontena hizo zimeonyesha kupitishwa mpaka wa Tunduma ili zionekane zimetokea nchini Zambia.

Alisema kuna uhalifu wa ukataji wa magogo ambao unafanywa na baadhi ya watu kwa ajili kuharibu maliasili ya nchini.
 
Dk. Meru alisema vyombo vya upelelezi vya wizara hiyo,  vilipata taarifa ya kuwepo na magogo bandarini ambayo yalitakiwa kusafirishwa nje ya nchi.

Alisema mara baada ya kupata taarifa hizo, walizifanyia kazi na kufanikiwa kuzikamata kontena 31 ambazo hazikuwa na kibali cha usafirishaji.

"Baada ya kuzikamata tulichokifanya tulienda kuonana na balozi wa Zambia tukawaeleza na wenyewe wanasema hawawezi kutoa kibali kwa kuwa wanakataza ukataji wa magogo nchini kwao, " alisema.

Aliongezea kuwa ; "Inawezekana magogo hayo wameyakata nchini na kufanya udanganyifu wa kwenda kuzunguka katika mpaka wa Tunduma kuonyesha kuwa yametokea Zambia, lakini balozi ameahidi kushirikiana na sisi."
  
Dk. Meru alionya yoyote atakaye bainika kuhusika katika suala hilo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria ili na wengine wajifunze kupitia tukio hilo.

Alisema Serikali ya Zambia na Tanzania zimeingia makubaliano ya kudhibiti biashara haramu ya ukataji wa magogo.

Naibu Balozi wa Zambia, Elizabeth Phiri, alisema sheria inazuia usafirishaji wa magogo, hivyo hana uhakika kama ni kweli vibali vimetolewa nchini kwake. Tunasubiria tupatiwe document (nyaraka) zinazoonyesha tumeruhusu usafirishaji wa magogo hayo ndipo tutalitolea taarifa, alisema Phiri
 
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala za Huduma za Misitu, Zawadi Mbwambo, alisema jumla ya kontena 37 zilizokamatwa zikiwa na magogo hayo na nyingine zipo kwenye vituo vyao vya ukaguzi.

Alisema hakuna uhakika kama kontena hizo zimesafirishwa kihalali kwa kuwa walipewa taarifa kuwa  yalikuwa yanapelekwa China kwa ajili ya kutengeneza samani na dawa.

Aidha, alisema kampuni tatu zimeonekana kuagiza mzigo huo ambazo ni Pan Atlantic, Best Ocean Air na Dar Global.

#YALIYOJIRI>>>Papa Francis Kumfufua Nyerere,Mama Maria Nyerere Atangulia Uganda.Fahamu zaidi hapa.

ZIARA ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis nchini Uganda imetajwa kuwa itafufua mchakato wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa mtakatifu.

Kwa mujibu wa mtandao wa ETN wa nchini Uganda, ziara hiyo ya kitume ya Papa Francis itamfikisha katika eneo la Namugongo ambalo mashahidi wa imani ya dini ya Kikristu walichomwa moto.

Ni katika eneo hilo la Namugongo ambako Hayati Nyerere alitangazwa kuwa Mwenyeheri huku mchakato wa kumtangaza mtakatifu ukiwa ulianza miaka tisa iliyopita.

Namugongo ndiko ambako pia waumini wa dini ya Kikristu wa Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani hufika kuhiji.

Taarifa ya ETN imeeleza kuwa ziara ya Papa Francis Namugongo itasaidia kufufua mchakato uliodumu kwa miaka tisa sasa wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa kuwa mtakatifu.

Tayari mjane wa Hayati Mwalimu Nyerere, Mama Maria Nyerere yuko nchini Uganda ambako amekwenda kujumuika na waumini wengine wa dini ya Kikristu kumpokea na kushiriki ibada itakayoongozwa na Papa Francis.

ETN imemkariri Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, akisema kuwa mchakato wa kumtangaza Hayati Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu umetokana na mchango wake wa kuhimiza heshima na usawa kwa binadamu ambao aliutoa wakati akiwa kiongozi.

Kwa mujibu wa ETN, Rais Museveni amesifu mchango wa Hayati Mwalimu Nyerere ambao haukuwa tu wa kuunganisha Watanzania bali alifanya kazi kwa kujali utu wa Waafrika.

“Hayati Julius Nyerere alikuwa mwanaharakati wa Afrika ambaye alimpenda Mungu na alijali utu, aliwaunganisha Watanzania wa dini zote na alisaidia ukombozi wa mataifa mengine ya Afrika kama vile Zimbabwe, Namibia, Angola, Afrika Kusini na Uganda,” alisema Museveni.

Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, jana  alisema mchakato wa kumtangaza Hayati Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu unaendelea vizuri.

Alisema suala la kuendesha mchakato huo ni jukumu la Tanzania na si Uganda hivyo jina la Hayati Mwalimu Nyerere linaweza kuibuka katika ziara ya Papa nchini Uganda kwa kutajwa tu, kwa sababu Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, amekuwa na mazingira ya karibu na familia ya Hayati Mwalimu Nyerere.

“Jukumu la kuendesha mchakato wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa kuwa Mtakatifu ni letu na linaendelea vizuri. Kuna mambo mengi ya kuchunguzwa mpaka mtu kutangazwa kuwa mtakatifu, inawezekana Papa akamzungumzia Mwalimu kwa sababu ya Rais Museveni mara kwa mara ameonyesha kuguswa na mwenendo wa mchakato huo,” alisema Askofu Kilaini.

Papa Francis aliwasili nchini Uganda jana jioni saa 4:50 na kulakiwa na Rais Museveni na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo.

Kwa mujibu wa ziara yake nchini humo iliyotolewa na Kanisa Katoliki la Uganda leo anatarajiwa kufanya ziara ya kitume katika miji ya Munyonyo, Nikiyanja, Nalukolongo, Namugongo, Kalolo na Rubaga na kesho atamaliza ziara yake nchini humo na kusafiri kwenda nchini Afrika ya Kati (CAR).

Taarifa kutoka nchini Uganda zinaeleza kuwa ulinzi umeimarishwa na Serikali imeandaa wahudumu wa afya 400 na magari 38 ya kubebea wagonjwa ambayo yamepelekwa maeneo yote ambayo Papa atayatembelea.

Papa Francis atakuwa Papa wa tatu kutembelea taifa hilo ambapo mwaka 1969, Papa Paul VI alitembelea nchi hiyo akifuatiwa na Papa Paul II mwaka 1993.

Kampeni za urais zasimama
Katika hatua nyingine wagombea urais wa vyama vyote wamelazimika kuahirisha mikutano yao ya kampeni kwa ajili ya kupisha ziara ya Papa Francis nchini humo.

Rais Museveni ambaye anawania urais kwa muhula mwingine, aliwaambia wafuasi wa chama chake kuwa atamuomba Papa asaidie kutangaza utalii wa taifa hilo.

Akemea ukabila na rushwa nchini Kenya
Awali kabla hajaondoka nchini Kenya, Papa Francis alihutubia maelfu ya vijana katika Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi ambapo aliwahimiza vijana wa taifa hilo wasijihusishe na ukabila.

Alisema vijana wanaweza kuchangia katika kukabiliana na changamoto za ukabila ambazo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya mataifa ya Afrika.

Aliwashauri viongozi wa Serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu na ajira kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuwazuia kujiingiza katika makundi yenye itikadi kali za kigaidi.

Kabla ya kuhutubia vijana katika Uwanja wa Kasarani, Papa Francis, alitembelea Mtaa wa Kangemi ambako wanaishi watu masikini na kukemea dhuluma ya huduma bora ambazo wanatakiwa wapatiwe masikini.

“Ninafahamu kuhusu tatizo kubwa linalosababishwa na wawekezaji wasio na sura ambao hujitwalia ardhi na hata kujaribu kunyakua viwanja vya kuchezea watoto wenu shuleni. Hili ndilo hufanyika tunaposahau kwamba Mungu aliwapa watu wote ardhi waitumie kwa maisha yao bila kutenga au kupendelea yeyote,” alisema Papa Francis.