Jeshi
la Polisi jijini Dar es Salaam jana lilifanya upekuzi mkubwa katika
nyumba ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) baada ya kumtilia shaka
kuwa na nyaraka muhimu za vikao vya uchaguzi wa Meya wa Jiji hilo.
Kikosi
cha jeshi hilo kilifika katika nyumba ya mbunge huyo majira ya saa tisa
alasiri na kufanya mazungumzo na Mwanasheria wake, John Mallya ambapo
baada ya kukamilisha taratibu za kisheria walianza zoezi la upekuzi
uliochukua zaidi ya saa moja.
Kiongozi
wa kikosi hicho cha Polisi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa
walilazimika kufanya upekuzi katika nyumba hiyo baada ya kusadikika kuwa
wakati wa vurugu zilizotokea katika ukumbi wa Karimjee jijini humo
wikendi iliyopita kufuatia kuahirishwa kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji,
Mdee aliondoka na faili muhimu lenye madokezo yanayohusu uchaguzi huo.
Hata
hivyo, baada ya kukamilisha upekuzi huo, Polisi walijiridhisha kuwa
hakukuwa na nyaraka hizo ndani ya nyumba hiyo wala kitu chochote ambacho
wangekitilia shaka licha ya kukuta nyaraka nyingi za mbunge huyo.
Hivyo, walitoa cheti maalum cha kuthibitisha kuwa hakuwa na nyaraka
zozote kinyume cha sheria.
“Wamekagua
nyaraka zote. Madai yao ni kuwa Halima alimpora au alichukua nyaraka za
kiongozi wa Jiji, lakini wamekuta hakuna jambo lolote ambalo linatiliwa
shaka. Na wametoa Certificate inayoonesha kwamba hakuna chochote
ambacho kimechukuliwa,” alisema Mwanasheria wa Mbunge huyo, John Mallya.
Mdee
alishikiliwa na Polisi na kulala rumande juzi kutokana na tuhuma za
kushiriki katika vurugu zilizotokea katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar
es Salaam, Jumamosi, Februari 27.
Wengine wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.
0 comments:
Post a Comment