Tuesday, 19 July 2016

#YALIYOJIRI>>>>Rais Magufuli Akataa Kuwapandisha vyeo Maofisa 17 wa Polisi.Fahamu zaidi hapa.

Rais John Magufuli, amekataa kuwapandisha vyeo maofisa 17 wa polisi waolipendekezwa na amewapa nafasi ya kujipanga zaidi. 

Rais Magufuli aliwapandisha vyeo maofisa 60 kuanzia Jumamosi iliyopita, kati yao 25 kutoka cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP). 

Wengine 35 aliwapandisha kutoa cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi. 

Akizungumza jana muda mfupi baada ya maofisa hao kuapa kiapo cha maadili ya umma, Rais Magufuli alisema waliokuwa makamishna wasaidizi waandamizi waliopelekwa kwake katika mapendekezo walikuwa 31, lakini wamerudi 25. 
Pia, alisema waliokuwa makamishna wasaidizi wa polisi waliopendekezwa kuwa makamishna wasaidizi waandamizi wa polisi walikuwa 46, “ wamerudi 35.” 

“Wale ambao hawakurudi tuwape nafasi ya kujipanga tena zaidi. Nataka niwaeleze ukweli kwa sababu inawezekana wako wengine walisikia kwamba majina yao yalipelekwa…Sasa mkawaambie hayakurudi kwa sababu yangu. Wala wasihangaike kutafuta mchawi,” alisema Rais Magufuli. 

Alisema baada ya kupata taarifa na data zote walizonazo, “Nikaona tuwape muda wa kujirekebisha. Kwa hiyo nyinyi mliofanikiwa mpaka mmefikia hapa nawapongeza sana. “Mchakato ulikuwa mrefu na mzito,” alisema Rais Magufuli. 

Aliongeza, “Nyinyi sasa ni makamanda tunaowategemea katika nchi hii. Mmechaguliwa siyo kwa makosa. Mnastahili. Katekelezeni wajibu wenu bila woga kwa kuzingatia sheria.” 

Kuhusu mchakato huo, Rais Magufuli alisema alimwagiza, IGP Ernest Mangu karibu miezi mitano iliyopita kuanza mchakato huo.
Alisema mchakato ulianzia na ukapita kwa wakuu wao (wa polisi) kwa kuangalia historia za wale ambayo majina yao yalikuwa pamoja na kazi zao. 

“Wakapita (majina ya wapendekezwa) mahali pengine mpaka yamefikia kwangu…Ninajua hamtaki kusema lakini mimi nimeumbwa kusema ukweli.” 

Watumishi ‘raia’ kuondolewa  Katika hotuba yake ya takriban dakika 30 aliyotoa bila kusoma popote, Rais Magufuli alisema inawezekana wapo watendaji wachache ndani ya Jeshi la Polisi ambao aidha kwa makusudi au kwa nia yao mbaya wanalichafua jeshi hilo. 

“Ninawaomba mkawashauri na kuwaelekeza, ikishindikana mkawaondoe katika Jeshi la Polisi. Mfano mzuri ni mhasibu ambaye aliorodhesha watumishi ambao si maaskari kulipwa pensheni wanayolipwa maaskari. 
“Mtu mwenyewe siyo askari, la kujiuliza nyinyi lakini mmeshindwa kumshika,” alihoji. 

Mhasibu huyo, Frank Msaki (ambaye si polisi) alisimamishwa kazi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, kwa makosa ya kufanya malipo hewa ya posho ya chakula kwa watu wasio askari. 
Kutokana na hilo, Rais Magufuli alisema kama wanafikiri kuwa na raia kwenye Jeshi la Polisi wanaliharibia jeshi, wahamishwe na wapelekwe utumishi. 

“IGP kaorodheshe raia wote wanaofanya katika Jeshi la Polisi watoke. Tuwapangie kazi nyingine kazi za kiraia. Ili kusudi hawa raia wanaokaa kwenye nafasi za jeshi waondoke. Bila kufanya hivyo inawezekana wataendelea kuwachafulia. Naomba hilo lishughulikiwe,” alisema. 

Mbali na agizo hilo, alimtaka IGP kufuatilia mtu aliyelipwa kati ya Sh20 bilioni hadi Sh60 bilioni kwa ajili ya kutengeneza sare za polisi tangu mwaka jana, lakini hadi sasa bado hajakabidhi sare hizo. 

“Tupate hizo fedha zetu ili mkakomboe magari yenu. Ninategemea siku moja waliohusika na hilo watapelekwa mbele ya haki,” alisema. 

Mwigulu Nchemba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliwataka walioapishwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu. “…Sheria isipofuata mkondo wake wananchi wanachukua sheria mkononi. Tuzuie hilo na kuhakikisha sheria zinafuatwa,” alisema. 

Kamishna wa maadili, Jaji mstaafu Salome Kaganda aliwashauri maofisa hao wa Jeshi la Polisi kuunda kamati za maadili kwa ajili ya kusikiliza manung’uniko yao. 

IGP, Mangu alimshukuru Rais kwa kupokea mapendekezo yao na kuahidi kuwa atahakikisha maofisa hao wanatekeleza kiapo walichokula.

0 comments:

Post a Comment