Friday, 11 November 2016

#MICHEZO>>>>BONDIA MTANZANIA, DULLAH MBABE ASIMULIA ALIVYONASWA AIRPORT KISA MADAWA YA KULEVYA.FAHAMU ZAIDI HAPA.

Usiku wa Jumatano ya wiki jana almanusura uwe mbaya kwa bondia Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’, hiyo ni baada ya kushikiliwa na jeshi la polisi kitengo cha kupambana na madawa ya kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa tuhumu za kubeba madawa ya kulevya ‘unga’ alipokuwa akijiandaa kwa safari ya kwenda Ujerumani.

Dullah Mbabe alikuwa akielekea Ujerumani kuwania mkanda wa ubingwa wa dunia wa WBC dhidi ya Mjerumani, Toni Kraft, pambano lililopangwa kufanyika Novemba 5, 2016 jijini Munich.


Siku hiyo ya safari aliwekwa chini ya ulinzi kwa zaidi ya saa 14, baadaye akaachiwa huru kuendelea na safari kutokana na kutokutwa na kosa lolote. Championi Ijumaa limezungumza naye kuhusu kilichotokea kwa urefu.

Dullah Mbabe
 
“Kabla ya kupata pambano la Ujerumani kuna mtu ambaye alikuwa ni mwalimu wangu msaidizi anaitwa (anamtaja jina) aliniletea ofa ya dola 4,000 (Sh milioni 8.5) kwenda kucheza Urusi, kisha katika fedha hiyo akataka nimpe dola 1,000 (Sh milioni 2.1) halafu dola 500 (Sh milioni 1) wapewe watu wa vyama na mimi nibaki na dola 2,500 (Sh milioni 5).

“Mimi na uongozi wangu chini ya meneja, Chifu Kiumbe tulipinga kwa kuwa fedha hiyo haikuwa na maslahi, baada ya hapo kuna mtu mwingine, Ibrahim Marsh akaleta ofa ambayo ni hiyo ya Ujerumani, uongozi ukaona ina maslahi mazuri kwetu, wote tukakubali, kumbe yule jamaa wa awali baada ya kuona hivyo akawa amechukia.

“Ilifikia wakati alimueleza kocha wangu mkuu, Omari Dame kuwa atahakikisha safari yangu ya Ujerumani haifanikiwi, mara nyingi akawa anamuuliza maswali mtoto wa bosi wangu anaitwa Dulla Spartan akitaka kujua naondoka lini.

“Nadhani baada ya kujua siku nitakayoondoka, moja kwa moja tunahisi ndiye atakuwa amehusika kunifanyia huo mchezo maana baada ya kufika airport nikiwa na Ibrahim Marsh na Dullah Spartan, ofisa mmoja aliyekuwa akikagua hati yangu akasema mimi ninatafutwa na polisi pale uwanjani.

“Sikujua kuna nini kinachoendelea, tukakubali kwenda kuwasikiliza hao polisi, wakati huo Spartan alikuwa ameondoka kwa kuwa yeye alitusindikiza na nilitakiwa kusafiri mimi na Marsh.

                                           Dullah na familia yake.
 
“Tukafanyiwa ukaguzi mimi na mizigo kwa pamoja lakini hakuna kilichoonekana. Tulipofika sehemu ya ukaguzi wa mwisho wa hati ya kusafiria ndiyo nikazuiwa, polisi wakanitaka niwape ushirikiano kwa madai ya kupewa taarifa kwamba kuna mzigo nilikuwa nasafirisha, nikafanyiwa upekuzi tena, napo hawakufanikiwa.

“Walipoona hivyo wakaniletea kahawa ya moto, wakaniambia nichague moja, niwaambie ukweli kuwa nimebeba unga ili nisinywe au ninywe nife kama kweli nimebeba, kwa kuwa nilijua sina kitu chochote nikanywa kahawa yao vikombe nane mpaka wakawa wanashangaa.

“Niliwaomba wanipe na maandazi kabisa kwa kuwa nilijua ninachokifanya, maana mimi huo unga wenyewe siujui hata rangi yake.

“Nikaendelea kuwekwa chini ya uangalizi hadi asubuhi ambapo wakanipeleka Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kunifanyia vipimo vya kina kuangalia kama nilikuwa na madawa, huko nako hawakuona kitu, wakaturudisha airport kutoa maelezo ya mwisho kisha niendelee na safari yangu.

“Nilipomaliza kila kitu ikanibidi nirejee nyumbani kwa ajili ya kuondoka usiku wa siku hiyo, nikalazimika kulipia faini ya tiketi ya ndege dola 130 (Sh 277,960) tena kwa fedha kutoka mfukoni mwangu.

“Nilipofika Ujerumani nikapelekwa katika hoteli ambayo pia kulikuwa na wachezaji wa Bayern Munich wameweka kambi na hata chumba changu kilikuwa kinaangaliana na chumba cha Robert Lewandowski na pembeni yake ni cha Arjen Robben, pia nilipata nafasi ya kwenda uwanjani kuangalia mechi yao dhidi ya Hoffenheim.

“Kutokana na mkanda tuliokuwa tunaushindania kuwa mkubwa, vipimo vilikuwa ni vingi mno lakini vyote nilionekana kuwa safi, mwangalizi wa pambano lenyewe alikuwa mkongwe wa ngumi, Mike Tyson ambaye ndiye aliyesaini glovu zangu muda mfupi kabla ya kupanda ulingoni.

“Nilipania sana hilo pambano sababu huyo Mzungu hakuwa na uwezo wa kuhimili kasi yangu, nilimuangusha katika raundi ya tatu akaokolewa na kengele ya mapumziko, baada ya hapo nilikuwa nikimpiga takribani raundi zote.

                                   Dullah akiwa kwenye gari lake.
 
“Katika raundi ya nane kuna mtu alipewa dola 1,000 aniletee kwenye kona ili niachie pambano, nilikataa sababu niliamini mpinzani wangu hafiki raundi 12, sababu tayari alishalegea.

“Walipoona nimegoma, wakatangaza raundi ya 10 itakuwa ya mwisho tofauti na makubaliano ya mkataba, sikuwa na ujanja, nikamaliza pambano lakini ajabu wakampa mpinzani wangu ushindi kwa pointi. Mashabiki wengi pale ukumbini walipinga kwa kuwa waliona bondia wao hakustahili kupewa ule mkanda.

Kufungua kesi dhidi ya aliyemchomesha
“Mpango huo upo na uongozi wangu unashughulikia japo kwa upande wangu nimeshamsamehe, mimi ni bondia, hivyo sipaswi kujiingiza katika migogoro sababu hujui adui yako anatumia mbinu gani dhidi yako, najua alitaka kunipoteza kabisa kwa maslahi yake binafsi,” anasema Dullah Mbabe.


SOURCE: CHAMPIONI

0 comments:

Post a Comment