Mahakama
Kuu imewapa siku saba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake kujibu
madai ya chama hicho.
Msajili,
Lipumba na wenzake walipewa muda huo jana na Jaji Sekieti Kihiyo
kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa CUF
mahakamani hapo.
Katika
kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016, bodi ya wadhamini CUF inaiomba
mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa
Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti wa chama hicho.
Pia,
wanaiomba mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili kufanya kazi nje ya
mipaka yake ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yake na pia itoe
amri ya kumzuia Msajili kuingilia masuala ya kiutawala ndani ya chama
hicho.
Mbali
na Msajili na Profesa Lipumba, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wanachama wengine tisa
waliosimamishwa uanachama wa chama hicho, akiwamo Naibu Katibu Mkuu Bara
ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua (Tabora), Magdalena Sakaya.
Kesi
hiyo ilitajwa jana mahakamani hapo kwa mara ya kwanza tangu
ilipofunguliwa Oktoba 19, mwaka huu na mahakama ikataka wadaiwa
kuwasilisha majibu ya madai hayo ya CUF, Novemba 17, mwaka huu.
Pia,
Mahakama ilielekeza upande wa Maalim Seif kuwasilisha majibu ya hoja za
wadaiwa Novemba 23 na ikapanga kesi hiyo itajwe tena Novemba 24, kwa
ajili ya kuendelea na hatua nyingine.
Wadai
katika kesi hiyo wanawakilishwa na mawakili Juma Nassoro na Halfani
Daim wakati Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanawakilishwa na
Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Obadia Kameya na Lipumba na wenzake
wakiwakilishwa na Mashaka Ngole.
Katika
hati ya Kiapo kinachounga mkono maombi hayo, Maalim Seif anadai kuwa
Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia utendaji wa ndani
wa Vyama vya Siasa.
Anadai
kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya nchi haimpi mamlaka Msajili
wa Vyama vya Siasa kuwa chombo cha rufaa wala kurejea mambo ya utawala
ndani ya chama cha siasa.
Badala
yake anadai mamlaka hayo yako kwa vyombo vya juu vya chama na Mahakama
na kwamba jukumu la Msajili ni kusajili vyama na kuweka kumbukumbu za
vyama hivyo.
CUF
kimekuwa na mgogoro wa kiuongozi baada ya Profesa Lipumba kuandika
barua ya kutengua uamuzi wake wa awali wa kujiuzulu ambao Msajili
alikubaliana naye na alikiandikia barua chama kuendelea kumtambua
mwenyekiti huyo. Hata hivyo, CUF ilimfukuza uanachama Lipumba.
0 comments:
Post a Comment