Donald
Trump ndiye rais ajaye wa Marekani, ameshinda katika uchaguzi
uliofanyika wiki hii, matokeo hayo ni kama hayakutegemewa na wengi hasa
kutokana na aina ya maisha ya mteule huyo.
Trump
anajulikana kwa kuwa ni bilionea na mfanyabiashara maarufu, amewahi
kuingia kwenye msuguano kutokana na kauli na misimamo yake kadhaa
kuonekana siyo ya kiungwana, lakini upande wa pili mkewe, Melania naye
ni ‘walewale’.
Melania ni mzaliwa wa Slovenia, aliwahi kuwa mwanamitindo ambaye alifanya kazi hiyo kwa miaka kadhaa barani Ulaya kabla ya kuhamishia makazi yake Marekani.
Aina ya maisha yake imewafanya wengi wajiulize kama kweli anastahili kuwa mke wa rais wa taifa kubwa kuliko yote kiuchumi duniani.
Linaposikika jina lake au anapotajwa wengi wanakumbuka picha zake za utupu na nyingine zinazoonyesha sehemu kubwa ya mwili wake ambazo zimesambaa mitandaoni.
Umri wake na mumewe
Melania amezidiwa miaka 24 na mumewe, Trump ambaye ana umri wa miaka 70.
Anakotokea, asili yake
Jina lake halisi ni Melania Knavs lakini kutokana na kazi ya uanamitindo alipata umaarufu kwa kutumia jina la Melania Knauss.
Kuanza mitindo
Alianza masuala ya mitindo akiwa na umri wa miaka 16. Aliyeanza kugundua muonekano wake kuwa unaweza kufaa katika mitindo ni mpiga picha Stane Jerko, Stane alikutana na ‘binti’ huyo nje ya ukumbi alipokuwa akitoka kwenye shoo ya mavazi.
Akamkaribisha kufanya majaribio ya kupiga picha za mavazi yaliyobuniwa, alionyesha uwezo mzuri na hapo ndipo alipoanza kupewa mkataba na maisha ya mitindo yakaendelea.
Kwa sasa Melania ameweka pembeni masuala ya mitindo na ni mfanyabiashara wa madini, amekuwa akiuza bidhaa zake hizo kwenye maduka makubwa.
Kuhusu madawa
Aliwahi kunukuliwa na Jarida la GQ akisema: “Kuna watu wengi wanazungumza kuhusu ngozi yangu, ukweli ni kuwa mimi siyo mtumiaji wa vitu hivyo, naijali ngozi yangu na ninapenda kuwa wa asili.”
Alivyoingia Marekani
Kufanya kazi katika nchi nyingi za Ulaya kukamfanya ajue vizuri lugha za Kingereza, Kifaransa, Kiitaliano, Kijerumani na Kiserbia. Mwaka 1996 ndiyo alihamia Marekani na kufanya kazi zake za mitindo.
Mwaka 2001 alipata hati ya makazi na mwaka 2006 akapewa uraia wa Marekani. Pamoja na hivyo amekuwa akirejea nyumbani kwao Slovenia mara kadhaa kwenda kusalimia.
Alivyokutana na Donald Trump?
Alianza uhusiano na Trump mwaka 1999 wakati huo, Melania alikuwa na umri wa miaka 28, wawili hao walikutana kwenye sherehe.
Trump akiwa ameongozana na mpenzi wake, Celina Midelfart, alipomuona Melania akapagawa kwa urembo wake, alipopata nafasi akaomba namba lakini akanyimwa.
Melania alikataa kumpa namba Trump kwa kuwa aliona yupo na mwanamke mwingine, badala yake yeye Melania akaomba Trump ampe namba yake.
Alipoulizwa juu ya hilo miaka kadhaa baadaye, Melania aliwahi kunukuliwa akisema: “Ningempa namba yangu, ningekuwa katika orodha ya wanawake zake ambao anawapigia. Nilitaka kuona nia yake. Ajabu ni kuwa alinipa namba zake zote anazotumia.”
Wiki moja baadaye ndipo bibie akaanza kumpigia tajiri huyo na kilichofuata ni historia.
Kauli tata
Kuna siku Melania alikuwa akihojiwa akanukuliwa akisema: “Huwa tuna kawaida ya kufanya mapenzi angalau mara moja kwa siku (yeye na mumewe).”
Ndoa yao
Melania ni mke wa tatu wa bilionea huyo ambaye kabla ya kufunga naye ndoa alishawahi kufunga ndoa mara mbili. Walifunga ndoa Januari 2005.
Harusi yao ilihudhuriwa na Hillary Clinton na mumewe, Bill Clinton, baadhi ya watu maarufu wengine ni Star Jones, P. Diddy na Shaquille O'Neal.
Katika ndoa yao, bibi harusi alivaa nguo yenye thamani ya dola 140,000 (Sh milioni 300) wakati bwana harusi alivaa nguo zenye thamani ya dola 200,000 (Sh milioni 428).
Kuhusu watoto
Wawili hao wana mtoto mmoja wa kiume, Barron William Trump ambaye alizaliwa mwaka 2006.
Mbali na hapo mumewe pia ana watoto wakubwa ambao ni Donald Jr (38), Ivanka (34), Eric (32), Tiffany (22) aliowapata katika ndoa zake zilizopita.
Picha za utupu
Katika ‘mishe’ zake za mitindo aliwahi kupiga picha akiwa mtupu kwenye Jarida la GQ la Uingereza.
Siku Trump alipoulizwa juu ya suala hilo alisema: “Ulaya picha kama hizo huwa ni vitu vya kawaida na zinatumika kwenye masuala ya mitindo."
Mbali na hapo ilikuwa ni kawaida yake kupiga picha zinazoonyesha umbo lake kwa kiwango kikubwa kutokana na kazi yake ya mitindo.
Maarufu kuliko Hillary Clinton
Inadaiwa
kuwa huyu atakuwa mke wa rais maarufu zaidi, hivyo kumshinda Hillary
Clinton aliyekuwa maarufu wakati Bill Clinton alipokuwa rais wa nchi
hiyo. Kwa sasa Trump anasubiri kula kiapo cha kuwa rais wa taifa hilo Januari 20, 2017 ambapo ndipo Melania ataanza kutambulia rasmi kuwa ni mke wa rais.
Melania Trump
Urefu: Futi 5 inchi 11
Mtoto: Mmoja
Chama: Republican
0 comments:
Post a Comment