Idadi na watu, raia na askari polisi waliouawa kwa kupigwa risasi katika
Wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga mkoani hapa imekuwa kubwa hivyo
kutia wasiwasi kwamba, maisha katika eneo hilo ni ya roho mkononi, Uwazi
limechimba na kuchimbua.
Uwazi limebaini hayo kufuatia Aprili 13, mwaka huu, askari polisi wanane
wilayani Kibiti kuuawa kwa kupigwa risasi kisha kuporwa bunduki 7 na
watu ambao jeshi hilo linasema ni majambazi.
Askari hao ni A/INCP Peter Kigugu, F.3451CPL Francis, F.6990PC
Haruna,G.3447 PC Jackson, H.1872PC Zacharia, H.5503 PC Siwale, H.7629PC
Maswi na H.7680PC Ayoub ambao wote wamezikwa Jumapili iliyopita.
KWA NINI MKURANGA, KIBITI NA RUFIJI?
Matukio ya askari kupigwa risasi wilayani humo si mageni lakini mbali na
askari, pia viongozi wa vijiji wapatao 18 katika wilaya hizo nao
wameuawa kwa kupigwa risasi. Inauma sana!
WANANCHI WA KIBITI
Wakizungumza na Uwazi baada ya mauaji ya askari hao, baadhi ya wananchi
wa Kijiji cha Mkengeni Kibiti, walisema kuwa, Mkoa wa Pwani umekuwa si
salama kwa maisha ya watu na mali zao kwani mpaka sasa, hesabu za haraka
zinaonesha kuwa, unaongoza kwa mauaji ya risasi huku viongozi na askari
wakiwa wanashika namba kubwa.
“Mimi kumbukumbu inaniambia, katika Mkoa wa Pwani na wilaya zake hizo,
tayari askari kumi na saba (17) wameshauawa kwa kupigwa risasi na
viongozi wa vijiji kama kumi na nane (18) nao pia wameuawa.
“Hii idadi ni kubwa sana, siamini kama kuna mkoa umefikia, labda Dar es
Salaam kwa sababu ya ukubwa wake wa makazi, lakini nje ya hapo sidhani,”
alisema mkazi mmoja wa aliyejitambulisha kwa jina la Masaidi Khalidi.
Anaongeza:
“Jeshi la Polisi likitaka kumalizana na hii hali ni kuingiza ushirikiano
na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waingie msituni na kufanya
kazi kama wako vitani, naamini wahalifu wote watakamatwa na itajulikana
nguvu yao ilipo.”
KUHUSU POLISI NI KWELI?
Kufuatia madai hayo, Uwazi lilichimba kwenye kumbukumbu za nyuma na
kukuta kweli idadi ya askari waliopoteza maisha Pwani inatisha, lakini
pia idadi ya viongozi wa vijiji ambao pia wameuawa kwa kupigwa risasi
pia inatisha.
WALIANZA POLISI HAWA
Juni 11, 2014, watu wenye silaha za jadi walivamia Kituo cha Polisi cha
Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga mkoani hapa na kumuua kwa kumshambulia
kwa mapanga askari Joseph Ngonyani kisha kupora bunduki tatu aina ya SMG
na risasi 50.
Mwaka 2015 nao ukaingia na balaa, matukio ya mauaji yaliendelea
kuukabili mkoa huu kufuatia askari wanne wa Kituo cha Polisi Ikwiriri
kuvamiwa na kuuawa na watu ambao jeshi hilo lilisema ni majambazi.
Askari hao ni Koplo Yahya Malima, Koplo Tito Mapunda, Koplo Gaston
Lupanga na Koplo Khatib Ame Pandu.
KIZUIZI CHA POLISI VIKINDU
Machi 30, 2015, saa 1:30 usiku wa kuelekea Sikukuu ya Pasaka, askari
wawili waliuawa kwenye kizuizi cha barabarani katika Kijiji cha Kipara,
maeneo ya Vikindu, Pwani. Waliouawa ni Sajenti Michael Aaron Tuheri na
Koplo Francis Mkinga. Mauaji hayo yaliliacha jeshi la polisi nchini
katika hali ya huzuni huku yakifananishwa na yale yaliyotokea katika
vituo mbalimbali vya polisi nchini.
IKWIRIRI TENA
Januari 21, 2016, watu wasiojulikana walivamia Kituo cha Polisi cha
Ikwiriri, Rufiji mkoani humu na kuwaua askari wawili, Koplo Edgar na WP
Judith na kupora silaha zilizokuwepo kituoni hapo.
KIJIJINI VIKINDU
Agosti 26, 2016, askari wa ngazi ya juu katika kikosi cha kupambana na
majambazi nchini, SSP Thomas Njiku aliuawa kwenye Kijiji cha Vikindu,
Mkuranga akiwa katika oparesheni ya kuwasaka watu waliodaiwa kufanya
uhalifu maeneo na Mbande, Temeke jijini Dar es Salaam.
JARIBU MPAKANI
Februari 22, 2017, taarifa kutoka Kibiti zilisema, mpelelezi wa wilaya
hiyo (OC-CID), SP Peter Kubezya aliuawa kwa kupigwa risasi ya tumboni na
watu hao wanaosadikiwa kuwa ni wahalifu. Tukio hilo lilijiri usiku wa
saa 1, ambapo watu sita wenye bunduki zinazosadikiwa kuwa ni aina ya
Sub Machine Gun (SMG) walivamia Kituo cha Kutoza Ushuru wa Mazao ya
Kilimo na Misitu Kijiji cha Jaribu Mpakani na kumuua kwa kumpiga risasi
afande huyo na raia wengine wawili.
KUHUSU VIONGOZI WA VIJIJI
Kwa upande wa viongozi wa vijiji si rahisi kuamini lakini ndiyo ukweli
ulivyo kwamba, idadi yao ilifikia kumi na nane (18) wakiwa wameuawa kwa
nyakati tofauti. Usiku wa Machi 28, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Tawi la Makondeko, Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini,
Emmanuel Lukanga aliuawa kwa kupigwa risasi.
MUDA MCHACHE KABLA
Akizungumza na Uwazi, kwenye mazishi ya kiongozi huyo, Katibu Kata wa
Ikwiriri Kaskazini, Sauda Mningi alisema saa chache kabla ya Lukanga
kufikwa na mauti walikuwa kwenye kikao cha kujadili suala la ulinzi na
usalama wa eneo hilo.
STAILI YAO YA KUUA
Staili ya watoa roho hao ni kuua kwa risasi wakitumia bunduki aina ya
SMG bila kuchukua pesa wala mali yoyote kutoka kwa marehemu huku wakiwa
wamevaa kininja na wakitumia bodaboda hali inayotafsirika kuwa, ni
mauaji ya visasi. “Huku jamani sisi wananchi, giza linapoingia wasiwasi
tupu. Tunakuwa hatujui nani atauawa. Hawa watu wameanza zamani, tangu
mwaka 2015,” alisema kiongozi mmoja huku akiomba hifadhi ya jina lake.
VIONGOZI WALIPOKEA MESEJI
Ilielezwa kuwa, viongozi mbalimbali wakitimia 18 wa vijiji vya wilaya
hizo walianza kupokea meseji za vitisho kutoka kwa kundi moja la
wahalifu wakidai roho zao ziko mikononi mwao, watawaua mmoja baada ya
mwingine.
MAUAJI YA KWANZA
Mapema mwaka 2015, kundi hilo lilidaiwa kumuua kwa kumchinja karani wa
Mahakama ya Mwanzo Mkuranga aliyetajwa kwa jina moja la Pazi.
MACHI MOSI, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana aliuawa
kwa kupigwa risasi na watu hao waliovamia nyumbani kwake. JULAI 17,
2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimanzichana, Ramadhani Mkagile naye
aliuawa kwa kupigwa risasi na watu hao waliofika nyumbani kwake kwa njia
ya bodaboda wakiwa wamevaa kininja.
AGOSTI 12, 2016 Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mkuruwili wilayani
Mkuranga, Salum Kiswamba ambaye pia alikuwa imamu wa msikiti, naye
aliuawa nje ya nyumba yake kwa kupigwa risasi.
OKTOBA 6, 2016 Katika Kijiji cha Kimanzichana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi, Bakari Simkole akiwa ofisini, alipigwa risasi ya kifuani na
kufariki dunia papohapo. OKTOBA 24, 2016 Kundi hilohilo lilimuua
Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda, Ally Omar kwa kumpiga risasi akiwa nje
ya nyumba yake.
DESEMBA 6, 2016 Mohammed Ally Thabiti ambaye alikuwa Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Nyambunda, Kijiji cha Nyang’hundu naye aliuawa kwa kupigwa
risasi na watu waliovaa kininja.
WAWILI WALIUAWA
Nyuma ya mauaji ya viongozi hao wa kijiji hicho, waliuawa viongozi
wengine wawili ambao Uwazi halikupata majina yao wala tarehe. Kijiji
kikabaki hakina viongozi. JANUARI, 2017 Mauaji ya viongozi hao
hayakuishia hapo, Januari mwaka huu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda
Wilaya ya Kibiti mkoani hapa, Said Mkandambuli naye aliuawa kwa kupigwa
risasi na kundi hilo, nyumba yake imeota majani baada ya familia yake
kukimbia.
JANUARI 19, 2017
Katibu Mtendaji wa Kijiji cha Nkwandala wilayani Kibiti (zamani kilikuwa
katika Wilaya ya Mkuranga), Oswald Mrope naye aliuawa na wauaji hao
ambao walimkuta akiwa amejipumzisha nje ya nyumba yake.
FEBRUARI 9, 2017 Saa 6 usiku, kundi hilo linaloaminika kuwa ndilo
linalotoa roho za viongozi, lilimuua Kamanda wa Mgambo Kata ya Bupu,
Mussa Koti na kuichoma moto nyumba yake.
SIKU HIYOHIYO
Wauaji hao siku hiyohiyo walimuua kwa risasi, Kamanda Msaidizi wa
Mgambo, Mohammed Cheleu na kuzichoma moto nyumba zake mbili, ya mke
mdogo na mke mkubwa na kuacha ujumbe kupitia vipeperushi kuwa, roho
zaidi zitaendelea kutolewa.
FEBRUARI 21, 2017 Watu watatu walipoteza maisha (mmoja kati yao akiwa OC
CID wa Kibiti) baada ya kuuawa na kundi la watu wanaodhaniwa ni
walewale wakiwa na silaha aina ya SMG/SAR. Mbali na OC-CID, wengine ni
Peter Kitundu aliyekuwa Mkaguzi wa Maliasili Kituo cha Jaribu Mpakani
na mgambo aliyekuwa akifanya kazi za ulinzi kwenye kizuizi hicho,
Athumani Ngambo.
MACHI 12, 2017
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kazamoyo, Hemed Njiwa naye aliuawa kwa kupigwa risasi na watu hao akiwa nyumbani kwake.
GAZETI LA UWAZI
Gazeti la Uwazi, mara kadhaa tangu mwaka 2015 limekuwa likiandika habari
za watu waliopo kwenye baadhi ya misitu kwenye wilaya hizo kwamba,
ndiyo wanaopanga mauaji ya kutisha ya polisi kwa lengo la kuchukua
silaha kwa matumizi wanayoyajua wao, ikiwemo kuwaua viongozi.
KINACHOTOKEA
Hata hivyo, licha ya mambo kuwa wazi, bado Uwazi limewahi kuitwa na
uongozi serikalini na kuhojiwa juu ya habari hizo, hasahasa habari
iliyowahi kuandikwa Julai 17, jana kwenye gazeti ndugu na hili, Amani
yenye kichwa cha habari;
WANAOJIITA AL QAEDA WAUA IMAMU WA MSIKITI.
Katika habari hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mkuruwili
Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Salum Kiswamba ambaye pia alikuwa imamu
wa msikiti wa eneo hilo, aliuawa nje ya nyumba yake kwa kupigwa risasi
na watu waliovalia kininja waliokuwa kwenye bodaboda.
Katika kusema ukweli huu, baadhi ya viongozi serikalini hutaka kuamini
kuwa, magazeti ya Global Publishers yanazua hofu huku ukweli ukiwa
unaonekana.
UWAZI NA BARUA KWA MAGUFULI
Pia, Uwazi liliwahi kumwandikia barua Rais Dk. John Pombe Magufuli
ikimweleza namna wananchi wa mkoa huo, hasa Mkuranga, Kibiti na Rufiji
wanavyoishi kwa wasiwasi wakimwomba msaada wake kwa imani kwamba,
anaweza kutuma jeshi maalum na kuwaangamiza wahalifu hao.
KAMANDA KOVA ALIWAHI KUSEMA HAYA
Kabla ya kustaafu kwake, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar
es Salaam, CP Suleiman Kova aliwahi kusema kuwa kuna mtu anaitwa Hery,
alihusika katika kufadhili matukio ya mauaji huko Amboni (Tanga),
Mkuranga (Pwani) na Stakishari (Dar) na mengineyo lakini aliongeza jeshi
la polisi kwa kutumia kikosi cha intelijensia kiliweza kubaini nyendo
zake na kuinasa picha yake.
UWAZI LILISEMA HOFU YATANDA MKURANGA
Gazeti hilihili liliwahi kuandika mwaka 2015 kuwa, hofu kubwa imetanda
wilayani Mkuranga hasa katika Kijiji cha Mamndi Mkongo kufuatia Jeshi la
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na wale wa Mkoa
wa Pwani kunasa silaha za kivita zikiwa zimefukiwa kwenye shimo
msituni. Tukio hilo la unasaji wa silaha lilifanikiwa Agosti 29, 2015
katika msitu mmoja uliopo katika kijiji hicho kilichopo umbali wa
kilomita 23 kutoka mjini Mkuranga.
SILAHA ZILIZOKUTWA
Uwazi lilizungumza na kamati ya ulinzi na usalama kijijini hapo na
kusema silaha zilizokutwa ni bunduki za kivita aina ya AK-47 (moja), SRA
(mbili), RPG (mbili) Greana (moja) na risasi 388, tambi za milipuko
mikali, kitabu cha muongozo wa kijeshi, kemikali za kutengenezea mabomu
ya kutupa kwa mkono na kitabu chenye maelekezo ya namna ya kujibadili
mwanaume kuwa mwanamke au mwanamke kuwa mwanaume.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Uwazi, wamemuomba Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest
Mangu kufuatilia kwa kina matukio hayo kwani yanawatia hofu wananchi.
KUTOKA KWA MHARIRI
Ni vyema jeshi la polisi likaongeza nguvu ya ulinzi ili kuhakikisha
watuhumiwa wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tunalaani
mauaji haya kwa nguvu kubwa tukiamini kwamba, waliouawa hawakuwa na
hatia!
Credit - Uwazi/Globalpublishers
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment