Tuesday, 13 February 2018

Ngoma, Yanga Mambo Safi Wamalizana.

SIKU chache baada ya uongozi wa klabu ya Yanga kutamka hatua yao ya kufikiria kuvunja mkataba na mshambuliaji wake, Donald Ngoma, kufuatia majeraha sugu, suala hilo sasa halipo, imeelezwa.

Ngoma, ambaye anaendelea kuuguza majeraha yake ya goti, anategemewa kuanza mazoezi wiki hii baada ya kudaiwa kupona.

Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, kwa sasa inaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini ikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara.

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo aliliambia Nipashe jana kuwa, Ngoma anajiandaa kurejea uwanjani hivi karibuni, hivyo suala la kukatishwa mkataba wake limesitishwa.

"Hayo yalikuwa mapendekezo, kwamba kama hatorejea uwanjani kwa muda mrefu ni vyema mkataba wake ukakatishwa, lakini Ngoma ameanza kupona na hivi karibuni ataanza mazoezi mepesi kabla ya kuungana na wenzake," alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Kwa upande wake, Meneja wa klabu hiyo, Hafidh Saleh, alimwambia mwandishi wetu kuwa taarifa alizonazo juu ya mshambuliaji huyo ni kuwa anaendelea kupona na hivi karibuni atarejea uwanjani.

"Hayo masuala ya mkataba ni ya uongozi zaidi, mimi binafsi sifahamu, ninachojua Ngoma anaendelea kupona na mwenyewe amesema anakaribia kurejea uwanjani," alisema Saleh.

Alisema amewasiliana na mchezaji huyo na kumhakikishia kuwa taratibu ameanza kupona na anatarajia kuanza mazoezi hivi karibuni.

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alikaririwa akisema kuwa wanafikiria kuuvunja mkataba na nyota huyo kwa kuwa amekuwa na majeraha ya muda mrefu.

Katika hatua nyingine, Yanga imepanga kuelekea Shelisheli mapema zaidi kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya klabu ya St Louis ya nchini humo.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumamosi iliyopita, Yanga ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0.

Ili kusonga mbele, wawakilishi hao wa Tanzania Bara wanahitaji ushindi ama sare ya aina yoyote katika mechi hiyo ya marudiano.

Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment