Siku 155 baada ya Dk John Magufuli kuapishwa kuwa Rais, aliyekuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi huo, Edward Lowassa
ametaja mambo matano yanayomfanya autilie shaka mustakabali wa Taifa
chini ya uongozi wa Rais huyo wa Awamu ya Tano.
Akizungumza na
wanazuoni wa ndani na nje ya nchi wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala nyumbani kwake
Masaki Dar es Salaam, Lowassa alisema: “Hali ya siasa nchini ni ya
hamasa lakini isiyo na msingi endelevu.”
Lowassa, ambaye
alishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo baada ya kupata kura milioni
6.07 sawa na asilimia 39.97 aliyataja mambo hayo kuwa ni Rais kugawa
fedha wakati chombo cha kufanya hivyo kipo, watumishi kuachishwa kazi,
upitishaji mizigo Bandari ya Dar es Salaam kushuka, nchi kunyimwa
misaada na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi hivi sasa.
Katika
uchaguzi huo, Rais Magufuli alipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia
58.47 na kumshinda Lowassa ambaye alikuwa amejiunga Chadema Julai mwaka
jana akitokea CCM ambako jina lake lilikatwa katika mchakato wa chama
hicho kupata mgombea urais.
Tangu aingie Ikulu, Rais Magufuli
amekuwa akichukua hatua mbalimbali za kutengua uteuzi au kuwasimamisha
kazi watendaji mbalimbali wa Serikali, kufuta maadhimisho ya sherehe
mbalimbali na kuagiza fedha zitumike kutekeleza miradi mingine huku
akiwabana wafanyabiashara kulipa kodi.
Uamuzi wake huo
unaofanywa pia na mawaziri wake umekuwa ukipongezwa na kukosolewa na
watu wa kada mbalimbali na jana Lowassa alikuwa miongoni mwa wakosoaji
hao ikiwa ni mara yake ya pili tangu Dk Magufuli aingie madarakani.
Mara
ya kwanza, Lowassa alikosoa sera ya elimu bure, alipoitofautisha na ile
aliyokuwa ameahidi ya kuanzia awali hadi chuo kikuu na kuhoji iwapo
Rais Magufuli mbali na ada angefuta pia michango mingine, jambo ambalo
lilifanyiwa kazi.
Alipoulizwa kuhusu mazungumzo hayo, Profesa
Mukandala alisema: “Tunafanya utafiti kuhusu masuala mbalimbali ya
kisiasa, uchumi, utawala bora na ushindani wa siasa na tunazungumza na
watu kutoka vyama mbalimbali na viongozi wa Serikali.”
Waziri wa
Habari, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Lowassa alisema
waziri mkuu huyo wa zamani anapingana na viongozi wa Chadema wanaokiri
wazi kuwa Rais Magufuli anatekeleza sera na mikakati ya upinzani.
Taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya Lowassa ilisema
mwanasiasa huyo aliwaeleza wanazuoni hao kuwa; “hali ya siasa hivi sasa
ni ya hamasa kutokana na Serikali mpya na ‘style’ mpya. Kwa kipindi
kifupi atakuwa lakini hakuna mafanikio ya kiuchumi mbele ya safari.”
Alisema Rais amekuwa akigawa fedha wakati chombo cha kufanya hivyo kipo ambacho ni Bunge.
Rais
Magufuli amekuwa na utaratibu kuidhinisha fedha zilizotengwa kwa ajili
ya sherehe mbalimbali kutumika katika shu ghuli nyingine. Juzi, aliagiza
Sh2 bilioni zilizokuwa zitumike katika Siku ya Muungano zitumike
kupanua barabara inayokwenda Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Pia,
amewahi kuamuru Sh4 bilioni za Siku ya Uhuru kupanua Barabara ya Morocco
– Mwenge, Dar es Salaam.
Aliagiza pia fedha za maadhimisho ya siku ya
Ukimwi kutumika kununua vifaatiba na Sh225 milioni zilizotengwa kwa
ajili ya hafla ya uzinduzi wa Bunge zilinunulia vitanda Hospitali ya
Taifa Muhimbili.
Lowassa pia alieleza kusononeshwa na hali ngumu ya maisha na idadi kubwa ya watu kuachishwa kazi.
“Nasononeshwa
ninapoona watu wanaachishwa kazi na mashirika mbalimbali kwa sababu ya
hali ngumu ya uendeshaji wa mashirika hayo.
“Bandarini sasa hivi
nasikia uingizaji mizigo umeshuka kwa asilimia 50, kampuni nyingi za
mizigo zimefunga shughuli zake na pale kulikuwa na vijana wetu wengi
wana ajira, sasa hivi wako mitaani, hali inatisha maisha ya mwananchi
yanazidi kuwa magumu,” alisema.
Lowassa aligusia uamuzi wa
Marekani kupitia bodi yake ya Changamoto za Milenia (MCC) kusitisha
msaada wa zaidi ya Sh1 trilioni.
“Ni pigo kwa mustakabali wa uchumi.
Halafu tunasema tunataka nchi ya viwanda, hela tutatoa wapi kama si hawa
wafadhili wa ndani na nje kusaidia katika hilo?” alihoji.
Lowassa
ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema: “Hawa wafadhili
siyo watu wa kuwabeza wataturudisha nyuma. Jakaya (Kikwete- Rais mstaafu
wa Awamu ya Nne) kwa kiasi kidogo alijitahidi kuvutia wawekezaji, japo
kulikuwa na uzembe na ufisadi katika kuwasimamia.
“Hapa kinachotakiwa ni kufanya mabadiliko katika mfumo na kuufanya kuwa endelevu,” alisema.
Alisema
si kweli kuwa kila mtu katika Serikali ya Awamu ya Nne alikuwa mla
rushwa huku akikiri kuwa mfumo wa Serikali hiyo ulikuwa mbovu na wa
kifisadi.
Aliwaeleza wanazuoni hao kuwa: “Uchaguzi ule
tulishinda (upinzani) na kila mtu anajua hivyo. Hata Magufuli anajua
hilo...,” alisema.
Akizungumzia mikakati ya upinzani, Lowassa
alisema wamejipanga kuhakikisha hawaporwi tena ushindi na kusisitiza
kuwa joto la kutaka mabadiliko bado ni kubwa na Watanzania wameichoka
CCM.
Akijibu hoja zilizotolewa na Lowassa, Nape
alisema, “Anajichanganya tu, maana Mbowe (Freeman – Mwenyekiti wa
Chadema) amenukuliwa akisema Rais Magufuli anaiga kila kitu cha Chadema,
sasa yeye (Lowassa) anaposema hayo maana yake haelewani na Mbowe.”
Alisema
litakuwa jambo la ajabu kama Lowassa atakubali kila jambo linalofanywa
na Serikali iliyopo madarakani kwa kuwa ndivyo alivyo.
“Katika
Uchaguzi Mkuu Lowassa hakuchaguliwa na wananchi ila Magufuli
alichaguliwa kwa sababu wananchi walifurahishwa na sera zake, hivyo
amuache mwenzake atekeleze ahadi zake kwa wananchi,” alisema Nape.
“Kwanza
Lowassa amekuwa mtetezi wa wezi, mafisadi na wala rushwa. Unawateteaje
watu wa aina hii wanapofukuzwa kazi. Amebanwa tu na kwake kazi
inayofanywa na Magufuli inampa maumivu.”
0 comments:
Post a Comment