Watumishi 34 wa mahakama wakiwemo mahakimu 11, wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ya kinidhamu.
Aidha, Tume ya Utumishi wa Mahakama inaendelea kujadili hatma ya mahakimu 30, waliokuwa wanatuhumiwa kuhusika na rushwa na kushinda zao mahakamani ili kuangalia kama walifanya makosa ya kinidhamu.
Jaji
Mkuu, Mohammed Chande Othman alisema hayo Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea taarifa za ukaguzi
wa mahakama pamoja na uendeshwaji wa mashauri.
Othman
alisema watumishi hao, wamefukuzwa kutokana na uamuzi wa kikao cha Tume
ya Mahakama, kilichofanyika Agosti 18, mwaka huu baada ya kushughulikia
masuala mbalimbali ya kinidhamu.
“Tumewafukuza
mahakimu wakazi wafawidhi, mahakimu wa mahakama za Mwanzo za Rombo,
Temeke, Bahi na Chamwino na watumishi wengine 23. Hii ni idadi ndogo
ambayo ni sawa na asilimia 0.005 ya wafanyakazi wote lakini kwa mahakama
ni doa kubwa,” alisema Jaji Mkuu.
Alisema
mahakimu hao wamefukuzwa kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu, ikiwemo
kutumia muhuri wa mahakama kinyume cha taratibu, kuathiri utendaji wa
haki kwa kumsaidia mtu kufungua kesi moja katika mahakama mbili pamoja
na kufungua kesi ya mirathi bila kuwa na hati ya kifo.
Aliongeza
kuwa kuna makosa ya kisheria ambayo jaji au hakimu akikosea kutumia
kifungu cha sheria hawajibishwi, lakini kuna makosa ya kinidhamu ambayo
yanaondoa sifa ya kuwa hakimu au jaji.
Kuhusu
mahakimu walioshinda kesi za rushwa mahakamani, Jaji Chande alisema
mahakama inaweza isiwakute na hatia, lakini Tume itaangalia kama
walifanya vitendo vya ukosefu wa nidhamu na kuwawajibisha.
Aidha,
alisema mahakimu wengine 32 waliokuwa wanakabiliwa na kesi za jinai na
kushinda kesi mahakamani, wanafunguliwa mashitaka ya kinidhamu katika
Kamati ya Maadili ya Maofisa wa Mahakama kwa sababu inawezekana
hawajapatikana na hatia ya kosa la jinai, lakini kama kuna vitendo vya
ukosefu wa maadili watawawajibisha kimaadili.
Mahakama Maalumu ya Ufisadi
Katika
hatua nyingine, Mahakama Maalumu ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi imeanza
rasmi na wiki ijayo Kanuni za Uendeshaji wa mahakama hiyo, zinatarajiwa
kuchapishwa.
Jaji
Mkuu Othman alisema mahakama hiyo, imeanza rasmi Julai 18 mwaka huu
baada ya Rais John Magufuli kusaini sheria ya uanzishwaji wa mahakama
hiyo.
“Wiki
ijayo tutachapisha kanuni mbalimbali za uendeshwaji wa mahakama hiyo,
ikiwemo jinsi ya kulinda mashahidi pamoja na taratibu za ufunguaji wa
kesi,” alisema Othman.
Alisema
mahakama hiyo itakuwa na majaji wa kutosha ili kufanya kazi kwa
uadilifu na kumaliza kesi kwa wakati, pia haitakuwa ikiahirisha kesi
mara kwa mara.
Kuhusu
utendaji kazi wa mahakama, Jaji Mkuu alisema mahakama haiwezi kutoa
haki kama itakuwa inajificha au kuendeshwa kwa siri, ndiyo maana kwenye
maboresho ya mahakama, wameamua kuwapa fursa wananchi kutoa mapendekezo
au kero zao kupitia namba za simu pamoja na barua pepe.
Kesi za uchaguzi
Awali
akiwasilisha taarifa za utendaji wa Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu
Mkazi, Wilaya na za Mwanzo, Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta
alisema baada ya uchaguzi, walipokea kesi 247 za uchaguzi, 53 za kupinga
matokeo ya ubunge na 194 za udiwani.
Mugeta
alisema tayari wameshamaliza kesi 234, zimebaki 13, lakini hadi kufikia
Desemba mwaka huu kesi zote zitakuwa zimemalizika.
Aidha,
alisema tathmini waliyoifanya inaonesha kesi zilizopo zinawiana na
mahakimu, na kama watawezeshwa kwa vifaa vya kutendea kazi hadi Desemba
mwaka huu watamaliza kesi zote zilizofunguliwa mwaka huu.
Mahakama ya Rufaa
Kwa
upande wake, Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Kahyoza alisema kiwango
cha kumaliza mashauri katika Mahakama ya Rufaa kimeongezeka, pia wana
lengo la kuhakikisha nakala za hukumu zinapatikana siku hukumu na ndani
ya siku tatu zitapatikana kwenye tovuti ya Mahakama ya Tanzania.
Aidha,
aliwaomba wananchi watoe ushirikiano ili rufaa zisikilizwe na kuisha
mapema, kwa sababu kuna watu wanashindwa kufika mahakamani bila sababu
za msingi au kutoa visingizio jambo linalosababisha rufaa zao kuchelewa.
Umuhimu wa mahakama
Katika
hotuba yake kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4, mwaka huu,
Rais Magufuli alisema anaitegemea sana Mahakama na aliwaambia majaji na
mahakimu nchini kuwa:
“Nawaomba
waheshimiwa majaji na waheshimiwa mahakimu, muitangulize Tanzania
kwanza. Mkiitanguliza Tanzania kwanza tutaweza kufika mbali na tutaweza
kuwasaidia watanzania wengi.
"Nimeamua
nchi iende, na itaenda. Anayefikiri ataikwamisha, atakwama yeye kwa
sababu Mungu yuko pamoja na mimi. Na watu ninaowategemea sana ni
Mahakama. Mahakama unafunga kila mmoja. Hata Rais nikitaka kufungwa na
Mahakama, nafungwa. Mbunge anafungwa, nani anafungwa, nyinyi ndio
wenyewe”.
0 comments:
Post a Comment