Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuamuru msanii wa muziki wa kizazi
kipya, Emmanuel Elibariki maarufu ‘Ney wa Mitego’ kuachiwa huru na
baadaye kusema ameitwa Ikulu, rapa huyo amefunguka na kueleza
kilichojiri katika saa 36 alizokuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Ney wa Mitego alikamatwa Machi 26 alfajiri huko Turiani mkoani Morogoro,
akikabiliwa na tuhuma za kusambaza wimbo wenye maudhui ya kuitukana
Serikali. Hata hivyo, aliachiwa huru juzi alasiri katika Kituo cha Kati
jijini Dar es Salaam.
Saa chache baada ya kuachiwa huru juzi, taarifa za Ney kuitwa Ikulu zilienea na kuthibitishwa na msanii huyo jana.
Pia, alihojiwa na kituo cha Televisheni cha Azam ambako alikiri kupata
mwaliko wa kwenda Ikulu kesho kutwa kwa ajili ya mazungumzo na Rais
Magufuli.
“Ni kweli kuna taarifa kama hizo, ila siwezi kuzungumza sana kwa sasa kwa kuwa masuala haya yapo chini ya sheria,”alisema.
Afunguka saa 35 alizoshikiliwa
Akisimulia tangu alivyokamatwa saa 10 alfajiri ya Jumapili hadi
alipoachiwa Jumatatu ya Machi 27, Ney alisema alifuatwa na polisi katika
hoteli ya Premier Lodge mara baada ya kumaliza shoo aliyokuwa akiifanya
huko Turiani.
“Asubuhi nikapelekwa Kituo cha Dakawa, Mvomero huko nilikaa kwa saa
chache kisha wakanipeleka kituo kikuu cha Morogoro mjini. Nilichoambiwa
huko ni kwamba ninatakiwa kujibu tuhuma za kesi ya matusi kuhusu wimbo
wangu mpya ‘Wapo’,” Alisema.
Alisema baada ya kukaa mahabusu kwa saa kadhaa walifika askari kutoka
Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam na kumchukua akiongozana na polisi
kutoka Morogoro saa nane mchana, tayari kwa safari ya Dar es Salaam.
“Jioni tulifika na hapa nilipokelewa na kuingizwa tena mahabusu, huko nilikaa na nikalala bila kuambiwa chochote,” alisema.
Hata hivyo, alisema alishangazwa na namna askari walivyokuwa wakiendesha
shtaka lake, kwani hawakutaka kumuuliza chochote hata siku ya pili
ndugu zake walipofika kumuulizia waliambiwa hayupo.
‘Mpaka sasa sijui ni kwanini ndugu, watu wa karibu na jamaa walipokuwa
wakija kuniulizia waliambiwa sijafikishwa kituoni hapo, wakati huo wote
mimi nipo mahabusu hapa Dar” alisema.
Alisema hata polisi walipoanza kumuhoji, walimuhoji kwa makosa ya
mtandaoni huku wakidai kosa kubwa ni wimbo ulioikashfu Serikali.
Hata hivyo, alisema muda huo wote hakukuwa na Ofisa yeyote wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Nilihojiwa kwa takribani saa mbili na nusu hivi, wakati huo wote
nilikuwa na maofisa upelelezi wawili pekee na baadaye nilirudishwa
mahabusu,” alisema.
Licha ya mikiki hiyo yote, Ney alisema mpaka anaondoka Kituo cha Kati hakuambiwa kwa nini aliruhusiwa:
“Haya ni masuala ya kisheria zaidi hivyo siwezi kuhoji sana niliondoka baada ya wao kunishikilia kwa saa 30 na zaidi” alisema
Kuhusu kuboresha ‘Wapo’
Kuhusu kuboresha wimbo wake kama alivyoambiwa na Rais, Ney wa Mitego
alisema amepokea maoni hayo na kwamba yupo katika mchakato wa kuuboresha
na kuahidi hatavuka mipaka.
“Ninalifanyia kazi mheshimiwa amesema anaupenda wimbo wangu na
anausikiliza, yeye mwenyewe amewekwa kwenye huu wimbo ni jambo ambalo
hawezi kupuuzia na hiki kinachoendelea labda amefurahishwa, hivyo
nitaifanyia kazi kwa kuongeza mengi makubwa na kwa mapana zaidi bila
kuvuka mipaka,” alisema.
Alisisitiza kuwa yeye ni mwanamuziki na si mwanasiasa, hivyo kwa yeyote akitaka kumhukumu anatakiwa amhukumu kama mwanamuziki.
“Naona Rais ni mwelewa, tukimwambia tunahitaji nini atatuelewa ingawa
inatakiwa tusivuke mipaka na wananchi pia wanatakiwa kuzungumza vikiwemo
vyombo vya habari,” alisema.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment