WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia wakandarasi wasio na
uwezo na ambao wanapewa kazi lakini wanashindwa kuzimaliza katika muda
uliopangwa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo, jana (Alhamisi, Machi 30, 2017) wakati
akizungumza na watumishi wa Halmamshauri ya Chalinze na wale wa Mamlaka
ya Maji na Usafi wa Mazingira (CHALIWASA) katika ofisi zao, karibu na
daraja la mto Wami, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Alikuwa
ameenda kukagua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji Chalinze na ujenzi
wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza majisafi pamoja na matenki ya
kuhifadhia maji ambao umechukua muda mrefu lakini haujakamilika. Awamu
ya kwanza ilianza mwaka Septemba mosi 2001 na kukamilika Desemba mosi
2003.
Alimuagiza
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ahakikishe kuwa
kazi ya ujenzi wa mradi huo inaimarika na kufikia asilimia 80 la sivyo,
wakamilishe taratibu za kukatisha mkataba na kutafuta mkandarasi
mwingine.
Agizo
la Waziri Mkuu linafuatia taarifa aliyopewa kwamba mkandarasi wa mradi
huo, Overseas Infrastructure Alliance (OIA) Pvt Ltd ya India alipaswa
kumaliza kazi hiyo Februari 22, mwaka huu lakini hadi sasa mradi huo
umekamilika kwa asilimia 23 tu.
“Nimeelezwa
kwamba mmempatia nyongeza ya siku 100 ambayo inaisha tarehe 31 Mei
2017, kama kazi yake haitakuwa ya kuridhisha na kufikia walau asilimia
80, itabidi Mheshimiwa Waziri uendelee na taratibu zako za kukatisha
mkataba, tuanze kutafuta mkandarasi mwingine,” alisema.
“Hii
kampuni niliikuta Lindi kwenye mradi mwingine wa maji kama huu. Nilitoa
maagizo ya kuharakisha ujenzi ukamilike lakini hawakufanya hivyo hadi
Mheshimiwa Rais alipoenda na kuagiza mkandarasi anyang’anywe pasi yake
ya kusafiria mpaka atakapomalizia kazi.”
“Kwa
kifupi ni kwamba hii kampuni haina uwezo wa kufanya hizi kazi, na ndiyo
maana hadi sasa wamekamilisha asilimia 23 tu ya mradi wakati walipaswa
kuwa wamemaliza hivi sasa,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza: “Mheshimiwa Waziri endelea na utaratibu wa kuwaondoa kisheria sababu hata tukiwaongezea muda bado hawatakamilisha kazi.”
“Nimesikitika
sana kukuta mkandarasi hajafikia malengo. Mtu akipewa kazi anapaswa awe
na uwezo wa kifedha wa kuifanya ile kazi ili hata Serikali
ikichelewesha malipo yake, yeye aendelee na kazi,” aliongeza Waziri Mkuu.
Akizungumzia
kuhusu ufanisi wa mradi huo, Waziri Mkuu alimtaka Mkurugenzi Mtendaji
wa CHALIWASA, Eng. Christer Mchomba, ahakikishe kuwa wanapeleka maji
hadi majumbani mwa wateja na kuweka mita ili wananchi waweze kulipa bili
zao badala kuishia kutoa huduma hiyo kwenye vioski (viula).
“Kazi
ya kupeleka maji majumbani ni yenu CHALIWASA na siyo ya Wizara.
Pelekeni maji na mfunge mita ili watumiaji waweze kulipa bili zao. Pia
toeni elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara, waelezeni mipango
yenu na wapi mlipofikia. Kazi yenu siyo kutandika mabomba tu, bali
kutekeleza majukumu mliyopewa kwa niaba ya Serikali,” alisema.
Kuhusu
mitambo inayotumika, Waziri Mkuu alisema mashine zilizopo ni za siku
nyingi tangu 2003; hivyo amemuagiza Waziri Lwenge afuatilie upatikanaji
wa mashine za kisasa kwani hilo suala ni kubwa na haliwezi kubebwa na
CHALIWASA. “Bora mngeanza kuagiza mashine mpya hivi sasa, badala ya kusubiri zichakae kabisa, ndipo muanze kufikiria kuagiza.”
Mapema,
akitoa taarifa ya mradi huo, Eng. Mchomba alisema awamu ya tatu ya
ujenzi wa mradi huo ilisainiwa Mei 18, 2015 kati ya DAWASA na OIA yenye
ubia na kampuni ya Pratibha Industries kutoka India kwa gharama ya dola
za Marekani milioni 41.36 ambazo zilikuwa ni fedha za mkopo nafuu kutoka
benki ya Exim ya India.
“Kazi
zilizopangwa kufanyika ni upanuzi wa mtambo wa maji ili kuongeza
uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 500 hadi 900 kwa siku; ujenzi wa
mfumo wa mabomba ya kusambaza maji wenye kilometa 1,022; ujenzi wa
matenki makubwa 19 ya kuhifadhia maji; vituo tisa (9) vya kusukumia maji
(booster stations) na vioski (viula) vya kuchotea maji 351.”
Alisema
hadi sasa mkandarasi huyo amekwishalipwa dola za Marekani milioni 15.81
sawa na asilimia 38 na anaendelea na ulazaji mabomba ambapo hadi sasa
amekwishalaza mabomba yenye urefu wa km.141 sawa na asilimia 12.4.
Alisema
mradi huo umelenga kuvinufaisha vijiji 68 ambavyo 19 kati ya hivyo viko
Kaskazini mwa mto Wami na 49 viko Kusini mwa mto huo.
Akizungumzia
utendaji kazi wa mkandarasi huyo, Eng. Mchomba alisema Serikali
imechukua hatua za kimkataba dhidi yake kwa kumtoza gharama ya kuchelewa
kumaliza mradi (liquidated damages) kuanzia Februari 23, 2017.
“Pia
mkandarasi amepewa notisi ya siku 100 ya kumtaka aongeze kasi ya kazi,
vinginevyo tutasitisha mkataba ifikapo terehe 31 Mei, 2017 kulingana na
kipengele namba 8.7 cha mkataba,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 30, 2017.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment