MAKAMU wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, ameonekana
kuwaweka gizani mashabiki wa Yanga kutokana na kitendo chake cha kila
wakati kumtaja Mganda Emmanuel Okwi.
Okwi ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwatia tumbo joto Yanga,
zaidi ikiwa ni kutokana na kile alichowafanyia wakali hao wa Jangwani
Septemba 2012 alipoiongoza Simba kuwapiga watani wao hao wa jadi mabao
5-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa kufahamu hilo, kwa muda wote ambao Okwi amekuwa nje ya kikosi
cha Simba, mabosi wa klabu hiyo wamekuwa wakilitaja jina lake kwamba
wapo mbioni kumrejesha kama sehemu ya kuwatisha Yanga.
Hali hiyo ilijirudia kwa mara nyingine juzi kupitia kwenye mitandao
ya kijamii, ambapo Kaburu aliposti video ya mechi waliyoichapa Yanga
mabao 5-0 na kuweka ujumbe uliosomeka: ‘Usiyemtaka anakuja’.
Ujumbe huo ulionekana kama kutuma salamu Yanga kwa wakati huu ambao
timu hizo zinafukuzana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba
ikiwa kileleni kwa pointi zake 55, huku wapinzani wao hao wakifuatia na
pointi 53.
Kwa muda mrefu kumekuwa na tetesi kuwa Okwi anatarajiwa kurejea
Msimbazi baada ya klabu yake hiyo ya zamani kumalizana na SC Villa ya
Uganda anayochezea kwa sasa.
BINGWA lilizungumza na Kaburu kuhusu mchezaji huyo ambapo alisema,
Kamati ya Utendaji ya Simba haina pingamizi kuhusu usajili wa Okwi kama
benchi la ufundi litahitaji huduma yake.
Alisema kwa muda ambao Okwi ameishi na kutumikia kikosi cha Simba,
hawana wasiwasi naye na kwamba Msimbazi ni sawa na nyumbani kwa Mganda
huyo.
“Okwi, Simba ni nyumbani kwake, kama kocha atahitaji huduma yake, basi hatuna pingamizi,” alisema Kaburu.
Credit – Bingwa
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment