Asasi za kiraia 33 barani Afrika zimelaani kitendo cha kuvamiwa kwa
studio za televisheni ya Clouds na kulazimisha maudhui yasiyostahili
yarushwe hewani.
Tamko la asasi hizo limetolewa ikiwa ni siku chache baada ya Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora, (THBUB), Jukwaa la Wahariri (TEF) na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kulaani kitendo hicho
kinachodaiwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
Asasi hizo zinazohusika na utawala bora, demokrasia, haki za binadamu na
uhuru wa habari zilikutana hivi karibuni mjini Kampala nchini Uganda
katika mkutano uliokuwa ukizungumzia uhuru wa kujieleza na kupata
habari.
Tanzania kwenye mkutano huo iliwakilishwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki
za Binadamu (THRDC) , miongoni mwa mijadala iliyotawala ni kukemea
vitisho na vitendo vya kunyanyasa waandishi.
Pia, wajumbe katika mkutano huo waligusia mabadiliko madogo ya baraza la
mawaziri yaliyofanywa na Rais John Magufuli kwa kumtoa Nape Nnauye
kwenye nafasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Asasi hizo zilimpongeza Nape ambaye kabla ya kuondolewa kwenye nafasi
hiyo aliunda kamati iliyochunguza tukio la uvamizi wa studio za Clouds,
wakisema uamuzi huo ulionyesha ujasiri wa kusimamia uhuru wa vyombo vya
habari na uhuru wa kujieleza.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na asasi hizo, ilidai kwa siku
za karibuni Tanzania imekuwa na matukio zaidi ya 40 yanayolenga
kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
“Waandishi wamekuwa wakizuiwa au wakati mwingine kubughudhiwa ili
wasifanye kazi yao. Vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa hasa na wakuu wa
wilaya na polisi,” ilibainisha taarifa hiyo.
Wajumbe walikumbusha kifungu cha pili cha Azimio la kanuni za uhuru wa
kujieleza Afrika la mwaka 2002, kinachoelekeza Serikali ihakikishe
inachukua hatua stahiki kuzuia uvamizi kwenye vyombo vya habari.
Kifungu hicho kinaelezea endapo uvamizi huo utatokea, Serikali ina
wajibu wa kuchunguza na kuwaadhibu wahusika kwa mujibu wa kosa lao.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment