RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Tundu Lissu, ambaye pia ni
Mbunge wa Singida Mashariki, amesikitishwa na hatua ya Jeshi la Polisi –
kitengo cha Bandari kuendelea kumshikilia Ramadhani Mussa Hamisi
Ukwaju, bila kumfikisha mahakamani ama kumwachia kwa dhamana.
Ramadhani ndiye anayehusishwa na tukio la kusafirisha magari matatu ya
kifahari aina ya Range Rover katika makontena ambayo taarifa zake
zilionyesha mzigo huo ni nguo za mitumba, tukio lililofichuliwa na Rais
Dk. John Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar e
s Salaam takriban wiki moja iliyopita.
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) na pia Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
aliweka bayana hayo jana, Machi 27, 2017. Kwa mujibu wa taarifa ya Lissu
ambayo ‘tovuti’ hii imeinasa, Ramadhani amekuwa mahabusu kwa wiki
kadhaa sasa.
“Nimetoka Polisi Bandari muda huu. Nilikwenda kumwona mtu aitwaye
Ramadhani Mussa Hamisi Ukwaju ambaye yuko mahabusu ya Polisi Bandari
tangu tarehe 4 ya mwezi huu. Ukwaju anatuhumiwa kuhusika na mzigo wa
magari ya kifahari yaliyokamatwa na Bwana Mkubwa Rais siku chache
zilizopita. Leo ni siku ya 23 yuko mahabusu. Hajapelekwa kwenye mahakama
yoyote na hajashtakiwa kwa kosa lolote lile,” anaeleza Lissu
Anaendelea; “Suala lake limeshafika kwa DPP (Mwendesha Mashitaka) na kwa
RPC Simon Sirro tangu siku kadhaa zilizopita lakini kila mkubwa
anayehusika anaogopa kutoa maamuzi ya kumpeleka mahakamani au hata
kumwachia kwa dhamana ya polisi.”
Kwa mujibu wa Lissu, hayo ndiyo madhara ya rais kuingilia majukumu ya
kisheria yasiyomhusu. Anasisitiza; “Rais wetu anaweza kuwa Amiri Jeshi
Mkuu lakini yeye sio askari polisi mwenye jukumu la kukamata wahalifu au
kupeleleza makosa wanayotuhumiwa nayo.”
Anasema japokuwa ni Rais ndiye anayemteua DPP, lakini yeye si DPP na
hana mamlaka ya kuamua nani apelekwe mahakamani na nani asipelekwe.
“Sasa inapotokea Rais anakwenda kwenye matukio ya uhalifu, kama
ilivyokuwa kwenye suala la Ukwaju, anawafanya watendaji wanaohusika nayo
washindwe kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.
“Katika mazingira ya sasa ya 'utumbuaji majipu', watumishi wa umma
wanaogopa kufanya maamuzi kwa hofu ya kutumbuliwa majipu, hasa kwa
masuala ambayo yameshafikishwa kwa Rais kwa njia extra-legal kama hili
la Ukwaju. Matokeo yake haki za wananchi za kuwa huru zinakiukwa bila
sababu za msingi.”
“Haya ni masuala ambayo TLS chini ya uongozi wangu inatakiwa
kuyashughulikia. Hii ni sehemu ya agenda tutakayompelekea Rais na IGP
(Mkuu wa Jeshi la Polisi) na AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) pamoja na
Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi
tutakapoenda kuonana nao kama tulivyokwishawaomba. Kila mmoja wetu,
mawakili na wasiokuwa mawakili tuyapigie kelele matumizi mabaya ya
mamlaka ya kiupelelezi na ya kipolisi yanayopelekea haki za wananchi
wetu kuvunjwa namna hii,” anasema Lissu na kuongeza kuwa kelele
zitasaidia, ukimya ni sawa na kuyaunga mkono matendo hayo aliyoyaita
mabaya.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment