Friday, 31 March 2017

Kudadeki..Hivi Ndivyo Tundu Lissu Alivyopambana Kisheria Mahakamani Hadi Mbunge wa Chadema Lijualikali Akaachiwa Huru.Fahamu zaidi hapa.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana ilitengua hukumu ya kifungo cha miezi sita jela iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero Januari 11 dhidi ya Mbunge wa jimbo hilo, Peter Lijualikali.
Jaji Ama-Isaria Munisi alitengua hukumu hiyo dhidi ya Lijualikali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kukubaliana na warufani kwamba hati ya mashtaka iliyomtia hatiani ilikuwa na upungufu.
Lijualikali na dereva wake ambaye alihukumiwa kifungo cha nje waliwakilishwa mahakamani hapo na mawakili Tundu Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Fred Kiwelo na Enock Edwin.
Upande wa wajibu rufani - Jamhuri - uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi.
Adhabu ya dereva wa Lijualikali aliyehukumiwa kifungo cha nje, Stephani Mgatta pia imetenguliwa.
“Mahakama hii imeona maelezo ya hati ya mashtaka na vifungu vilivyotumika vina mapungufu na kwamba washtakiwa walishtakiwa pasipo kuwepo na hati ya mashtaka dhidi yao… mahakama hii inawaachia huru washtakiwa na inatengua adhabu ya kifungo” alisema Jaji Munisi.
Akifafanua zaidi alisema ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri katika mahakama ya chini ulikuwa haujitoshelezi kuweza kuwatia hatiani washitakiwa hao.
Alisema kutokana na mapungufu hayo makubwa mahakama hiyo inatengua adhabu za vifungo walizopewa washitakiwa hao na kuwaachia huru.
Baada ya kutolewa hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, alisema anasubiri kupitia hukumu hiyo ili aamue kama anakata rufani au la.
Mahakama ya Wilaya ya Kilombero ilimuhukumu Lijualikali (30) kwenda jela miezi sita licha ya kosa lake kuwa na adhabu ya faini, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa ni mkosaji mzoefu.
Alidaiwa kufanya fujo na kusababisha taharuki katika maeneo ya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Mwendesha mashtaka, Inspekta wa Polisi, Dotto Ngimbwa aliiambia Mahakama hiyo kuwa Lijualikali aliyekuwa mshtakiwa namba moja na Mgata (35) walitenda kosa hilo Machi mosi, 2016 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katika eneo la Kibaoni; ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Hakimu Mkazi, Timothy Lyon aliwatia hatiani washtakiwa hao baada ya kuridhika kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka haukuacha shaka.
Hakimu huyo alisema mshtakiwa wa kwanza Mbunge ambaye alikuwa na kesi tatu huko nyuma, atatumika kifungo cha miezi sita jela.
GEREZA LA UKONGA
Mgata alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita baada ya hakimu kuona hilo lilikuwa kosa lake la kwanza.
Baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, Lijualikali alipelekwa katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Lissu, alipozungumza na Nipashe kwa simu miezi miwili iliyopita.
Lissu aliiambia Nipashe siku hiyo kuwa alimtembelea mbunge huyo kwenye Gereza la Ukonga.
"Baada ya kuhukumiwa, walimpeleka Gereza la Ukonga," Lissu alisema. "Jumapili nilikwenda kumtembelea na kumweleza kuhusu mipango ya chama kumuombea dhamana na kukatia rufani hukumu iliyotolewa dhidi yake.
"Aliniambia hatayumba, ataendelea kupambana kutetea haki za wananchi wa jimbo lake na Watanzania kwa ujumla."


Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment