Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amesema
uongozi wa chama hicho umemwandikia Rais John Magufuli kutaka kukutana
naye Ikulu ya Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha rasmi na kufanya
mazungumzo.
“Ni mkutano baina ya Rais na rais,” alisema Lissu katika mahojiano na
gazeti hili alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited
(MCL) inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Lissu, ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alichaguliwa kuwa rais
wa chama hicho mapema mwezi huu, na Rais ni mmoja kati ya viongozi
kadhaa waliowaandikia kuomba kukutana nao.
Aliwataja wengine kuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu, Mkuu
wa Jeshi la Polisi na marais wawili wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya
Kikwete.
Alisema tayari Jaji Mkuu ameshakubali ombi lao.
Kuhusu ombi lao kwa Rais Magufuli, Lissu alisema atatumia fursa hiyo vizuri, iwapo watakubaliwa.
“Nikifika nitaanza kwa kumshukuru Rais kwa kuwafundisha Watanzania maana
ya utawala wa sheria, uhuru wa mawazo, uhuru wa vyombo vya habari na
uhuru wa Mahakama na Bunge,” alisema Tundu Lissu.
Lissu alifafanua baadaye kuwa Rais Magufuli amefumbua wengi macho kujua
vitu hivyo kutokana na jinsi anavyoendesha nchi, ndio maana atamshukuru.
“Tumeomba appointment na Rais Magufuli tuzungumzie utawala wa sheria,” alisema Lissu.
“Leo ni Jumatano? Barua tulimpelekea Jumatatu. Tutaenda kujitambulisha
na kuzungumzia utawala wa sheria na mwelekeo wa taifa hili. Ni between
presidents. Tuna imani kwamba atatukaribisha. Tutamweleza maoni yetu,
pale tunapoona amekosea tutamweleza na pale anapoona tuna matatizo
atatueleza.”
Alisema wanajua kuwa Rais ana shughuli nyingi, lakini wanatarajia atatenga muda kwa ajili yao.
“Tunafahamu yuko busy, lakini kama anaweza kuangalia Shilawadu, atakuwa
na muda hata nusu saa au saa nzima ya kuongea na kiongozi wa chama cha
mawakili wa Tanganyika,” alisema.
Lakini akaonyesha jinsi alivyopania kueleza matatizo anayoyaona katika utawala wa sasa.
“Nakwenda kumpa vidonge vyake, kabisa! Wala sitammezea. Nitamwambia kwa
heshima zote kwamba Mheshimiwa Rais, sisi kama mawakili wa Tanganyika
tuna wasiwasi mkubwa na mwelekeo wa Serikali yako,” alisema.
“Wamenituma nikueleze mwelekeo na matendo ya Serikali yako. Unatawala
vibaya, nje ya Katiba, wameniambia nije nikwambie ujirekebishe. Nakwenda
kumsimanga tu. Halafu tukitoka pale namwambia Mheshimiwa Rais tupige
picha, wajue nilikuja.”
Alisema iwapo Rais hatakubali kuwaalika, ataueleza umma.
“Atakuwa amenirahisishia, nawaita waandishi wa habari nawaambia.
Tulimwambia Bwana mkubwa tumsalimie na tumweleze kwamba haturidhiki na
utawala wake, yeye amekataa amekimbia,” alisema Lissu.
Hata hivyo, mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa amemtaka Lissu kusubiri taratibu za kiutawala.
Msigwa alimshangaa Lissu kwa kitendo chake cha kuzungumza katika vyombo vya habari ilhali anajua utaratibu wa kiutawala.
“Yeye kama ameandika barua barua si asubiri majibu? Muulizeni inakuwaje
kabla hajapewa majibu anaenda kutangaza katika vyombo vya habari? Si
asubiri utaratibu wa kiutawala,” alisema Msigwa.
Lissu alisema ofisi nyingine walizopeleka maombi kama hayo ni ya Makamu
wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi na marais
wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Paramagamba Kabudi
alisema hana taarifa juu ya barua hiyo kwa kuwa tangu ateuliwe hajaingia
ofisini.
“Nimekuwa katika vikao vya Kamati za Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma, hivyo sina habari hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Profesa Kabudi alisema inawezekana ni kweli rais huyo wa TLS
amewasilisha barua hiyo ofisini kwake lakini yeye bado haijamfikia.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment