Askari
wawili wanaotuhumiwa kuiba mafuta ya ndege ya Kampuni ya ATCL, kwa
kushirikiana na walinzi, wameondolewa kazini na kufikishwa mahakamani
kwa tuhuma za uhujumu uchumi.
Washtakiwa
hao na wenzao wawili walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Victoria Nongwa.
Akisoma
mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliwataja
washtakiwa hao kuwa ni Koplo Bahati Msilimini (33), PC Benaus (34), Iddi
Nyangasa (42) na fundi wa ndege, Ramadhani Mwishehe (52).
Katuga
alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili, shtaka la
kwanza kula njama na shtaka la pili hujuma dhidi ya Serikali.
Alidai
katika shtaka la kwanza washtakiwa wanadaiwa kati ya Machi mosi na
Machi 17 mwaka huu maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere walikula
njama ya kutenda kosa la uhujumu uchumi.
Katika
shtaka la pili washtakiwa wote wanadaiwa kati ya tarehe hizo, wakiwa na
nia ya kuhujumu manufaa ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, bila
uhalali walitoboa na kuchota mafuta ya ndege lita 280.6 kutoka kwenye
ndege JET A1 ya ATCL yenye namba za usajili 5H\MWF-8Q-300.
Katuga alidai kitendo hicho kilizuia utoaji wa huduma muhimu ya usafiri wa ndege.
Hata hivyo wakili huyo alidai upelelezi haujakamilika na hakuna kibali chochote kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Wakili
wa utetezi, Martin Rwehumbiza aliiomba mahakama ikubali kuwapa dhamana
wateja wake kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhamana.
Alidai thamani ya mafuta wanayodaiwa kuchota haizidi Sh milioni 10 hivyo mahakama hiyo ina mamlaka ya kutoa dhamana.
Akijibu
hoja hiyo Katuga alipinga washtakiwa hao kupewa dhamana kwa madai
kwamba wataingilia upelelezi hivyo aliomba wakae ndani kwa muda.
Akitoa
uamuzi Hakimu Nongwa alisema sheria inaruhusu Mahakama ya Kisutu
kushughulikia dhamana kwa makosa ambayo thamani yake haizidi Sh milioni
10.
“Sirahisi
kujua mafuta yalikuwa na thamani gani sababu hayakuwekwa katika hati ya
mashtaka, hakuna hati ya kuzuia dhamana kutoka kwa DPP, wangeona
washtakiwa wakiwa nje kwa dhamana wataingilia upelelezi wangeweka hati
ya kuzuia dhamana zao.
“Dhamana
ni haki ya washtakiwa hakuna zuio lolote, mahakama inaona ni vyema
washtakiwa wakapewa dhamana, hawawezi kuingilia upelelezi sababu
walishaondolewa kazini,”alisema Hakimu Nongwa.
Washtakiwa
wote walipata dhamana na wadhamini walitakiwa kuhakikisha washtakiwa
hao wanafika mahakamani kila kesi itapokuwepo. Kesi hiyo iliahirishwa
hadi Aprili 27 mwaka huu kwa kutajwa.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment