Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mkoa wake hauko
salama kama watu wanavyodhani kwa sababu silaha nyingi zinamilikiwa
kiholela na mafunzo ya matumizi ya silaha hizo hutolewa hata kwa watoto.
Makonda alisema hayo jana wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika katika
Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano na kuwataka wakazi wa Dar es
Salaam kujitokeza kuhakiki silaha zao na kusalimisha zile zinazomilikiwa
kinyume cha sheria.
Alisisitiza kwamba ifikapo Julai Mosi, operesheni maalumu ya kukamata
silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria itaanza na yeye mwenyewe ndiye
atakayeiongoza.
“Tumegundua kwamba kwenye bonde la mto unaotenganisha Mkoa wa Dar es
Salaam na Pwani, kuna mafunzo yanatolewa kwa watoto. Wazazi wanadhani
watoto wao wamekwenda shule kumbe wamechukuliwa huko. Hatuwezi kukubali
hali hiyo iendelee,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa aliwataka waumini waendelee kumwombea ili aifanye kazi
yake vizuri kwa kutenda haki na aliwataka pia kumwombea pia Rais John
Magufuli kwa sababu kazi anayoifanya ni kubwa.
Alisema Rais anapotumbua jipu moja, ndani yake kuna kundi la watu
wanaoathirika na hatua aliyoichukua hivyo, alisema watu wa aina hiyo
hawawezi kumpenda kwa sababu amevunja mtandao wa masilahi yao.
“Ninaomba kanisa pamoja na viongozi wote wa dini mnisaidie katika
kuhimiza suala la ulinzi na usalama ili amani yetu iendelee kudumu.
Ninaomba tushirikiane katika hilo, Dar es Salaam haiko salama kama
mnavyodhani, mengine siwezi kusema kwa sababu sijaruhusiwa na Rais,”
alisema.
Migogoro kanisani
Akizungumzia migogoro makanisani, Makonda alisema hataki kusikia
kiongozi yeyote wa dini anakimbilia polisi au mahakamani kutaka
suluhisho la matatizo yao ya ndani na kuwa atamweka ndani atakayejaribu
kufanya hivyo.
Alisema ni aibu kubwa kwa kanisa kukimbilia kwenye vyombo vya dola
badala ya polisi na Serikali kukimbilia kanisani kuomba ushauri. Alisema
kanisa ndicho chombo cha usuluhishi wa matatizo mbalimbali ya jamii.
“Serikali inahitaji msaada wa kanisa na viongozi wa dini ili iweze
kufanya kazi vizuri. Sitaki kusikia polisi wanakwenda kanisani (kukamata
watu) katika mkoa wangu na wale wanaotoa taarifa kutaka polisi
nitawaweka ndani,” alisema Makonda ambaye kabla ya kuwa mkuu wa mkoa,
alikuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
Askofu Mokiwa
Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam,
Valentino Mokiwa alibainisha mambo mbalimbali aliyoyaita majipu ambayo
yanafanya kanisa hilo lisiendelee katika kufundisha waumini wake yaliyo
mema.
Mokiwa alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na mashindano ya kimadhehebu.
Alisema madhehebu mbalimbali yanashindanishwa kupima kanisa lipi ni
kubwa, lina waumini wangapi, linamilikiwa na nani na nguvu yake ni ipi.
Jambo jingine alisema ni maaskofu wenyewe kupigana vita. Alisema sasa ni
kawaida kwa askofu mmoja kumchimba mwingine, askofu mmoja kupanga
mapinduzi dhidi ya mwingine na baadhi ya maaskofu kutukanana waziwazi.
“Maaskofu wanasemana na kusingiziana mambo ya uongo, injili haiwezi
kwenda mbele. Wengine wanatumia fedha na vyombo vya habari ili kutukana
wengine. Kanisani pia kuna walaghai na wezi ambao wanavaa kanzu,”
alisema Askofu Mokiwa.
Alisisitiza kwamba waumini wanapaswa kuogopana wao kwa wao kwa sababu ndiyo vikwazo vya wao kwenda mbinguni.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment