KIPA namba moja wa Kagera Sugar, Juma Kaseja, ametamka kuwa maisha yake
anategemea soka, hivyo hatasita kurejea kuichezea klabu yake ya zamani
ya Simba kama ikimhitaji.
Kauli hiyo, aliitoa hivi karibuni mara baada ya kumalizika kwa mechi ya
Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba iliyopigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja
wa Kaitaba, Kagera, matokeo yaliyomalizika kwa Kagera Sugar kushinda
mabao 2-1.
Kipa huyo aliwahi kuichezea Simba na kuipa mataji kadhaa akiwa kama
nahodha mkuu wa timu hiyo kabla ya kutimkia Yanga, Mbeya City na hivi
sasa Kagera.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kaseja alisema umri wake wa kustaafu
kucheza soka bado, hivyo basi ataendelea kucheza hadi pale atakapoona ni
muda mwafaka kwake kustaafu.
Kaseja alisema anashangazwa na maneno ya mashabiki wa soka wanaodai yeye
ni mzee lakini hivi sasa ni tegemeo na mwezi Januari, mwaka huu
alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi.
“Bila ya kuwa mvumilivu basi ningepotea kwenye soka muda mrefu kutokana
na maneno ya mashabiki, lakini nilijitahidi kuyaweka kando maneno yao na
badala yake kupiga kazi ambayo leo hii naonekana kijana.
“Kama unakumbuka niliwahi kuitwa mzee, nauza mechi lakini kama ningekuwa
ninauza mechi, basi ningewauzia hao Simba tuliocheza nao katika mechi
hiyo ili wapate ushindi, maana si walikuwa wanataka ushindi ili wachukue
ubingwa.
“Nikwambie tu, soka halipo hivyo kama wanavyofikiri, mimi maisha yangu
ninayaendesha kwa ajili ya soka, na kuhusiana na taarifa za kurudi, mimi
sina tatizo, hiyo ndiyo ajira yangu Simba wakinitaka narudi tu,”
alisema Kaseja.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment