Saturday 24 March 2018

Okwi,Bocco Waahidi Kupata Ubingwa wa Ligi Kuu.

BAADA ya Simba kutolewa katika Kombe la Shirikisho Afrika, mastraika wa timu hiyo John Bocco na Emmanuel Okwi kwa pamoja wameapa kufia uwanjani ili Wekundu wa Msimbazi wabebe ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Simba iliondolewa na Al Masry ya Misri katika Kombe la Shirikisho baada ya awali kutoka sare ya mabao 2-2 jijini Dar es Salaam halafu ugenini wakatoka suluhu.

Kutokana na hali hiyo, Okwi na Bocco wamesema lengo lao sasa ni kuhakikisha wanapambana kufa na kupona kwenye Ligi Kuu Bara ili waweze kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa.

Simba inaongoza katika ligi kuu ikiwa na pointi 46 sawa na Yanga, inayoshika nafasi ya pili, lakini wenyewe wana tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Okwi alisema, mipango yao ya kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho imekwama, sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye ligi kuu.

“Tunarudi kujipanga kwenye ligi kuu, kwani ndiyo sehemu pekee tunapotakiwa tupambane kufa na kupona ili mwakani tuweze kushiriki tena michuano ya kimataifa, tutapambana tuwe mabingwa,” alisema Okwi.

Kwa upande wake, Bocco ambaye pia ni nahodha wa Simba, yeye alisema; “Kiu yangu na wachezaji wenzangu ni kuhakikisha tunatwaa taji la Ligi Kuu Bara, maana ndiyo silaha pekee tuliyonayo kwa sasa, hiyo ndiyo tiketi ya sisi kucheza mechi za CAF mwakani.

“Pia tunajua furaha ya mashabiki wa Simba kwa sasa ni kuona tunatwaa ubingwa na siyo kitu kingine, hivyo tumejipanga kuhakikisha hilo linatokea bila tatizo.”

Simba leo Jumamosi inatarajiwa kuanza mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya Njombe Mji, Aprili 3, mwaka huu. 

Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment