Kamishna
wa Polisi Kanda Maalum Dar Es Salaam anatoa rai kwa wakazi wa Jiji la
Dar Es salaam na wageni wanaoingia jijini wakitokea mikoani kupuuza
taarifa za sauti zinazozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa Polisi
wanawakamata ovyo watu wanaolala kwenye nyumba za kulala wageni.
Taarifa
hizo za uvumi zinazoendelea kuzagaa kwenye mitandao ya Kijamii kama
WHATSAPP, TELEGRAM na pia zimechapishwa kwenye baadhi ya magazeti kwamba
Askari Polisi wanawakamata watu ovyo mchana wakiwa kwenye nyumba za
kulala wageni kwa madai ya kukamata kwa makosa ya uzembe na uzururaji
na pia kutimiza kauli ya Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ‘HAPA
NI KAZI TU’.
Kimsingi
niwatoe hofu raia wema kuwa tunaendelea na oparesheni za kuwasaka
watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba
za kulala wageni kinyume cha sheria (guest bubu), majambazi na wahalifu
wengine wa makosa mbalimbali.
Aidha
taarifa za kuaminika zimebaini kuwa baadhi ya nyumba za kulala wageni
zimekuwa zikitumika kuhifadhi magenge ya wahalifu, dada poa na kaka poa,
hivyo Jeshi la Polisi tunawajibika kufuatilia na kuwakamata wahalifu.
Niwajibu
wa Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye nyumba za kulala
wageni, Hoteli, migahawa, Vilabu vya vileo, kumbi za starehe
zinazokesha na zisizokesha na watakaobainika kuvunja sheria, hatua kali
za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.
Sheria
ya Mwenendo ya makosa ya jinai kifungu cha 60(1) (sura ya 77
iliyofanyiwa marekebisho 2002) kinampa nguvu askari kufanya ukaguzi wa
maeneo yote yaliyotajwa hapo juu na kumkamata mtu yeyote anayetiliwa
shaka akienda kinyume na utaratibu wa biashara hizo.
Sambamba
na hayo nawatahadharisha wafanyabiashara wote wa nyumba za kulala
wageni wafuate taratibu za kupokea wageni kwa kuandika kwenye vitabu,
kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanayotoka, na pale
watakapomtilia mashaka mteja yeyote watoe taarifa kituo chochote cha
polisi.
Pia
wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wa nyumba kumi wanawajibika
kuwatambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na kuwachukulia
hatua stahiki ili kuimarisha usalama katika jiji letu la Dar Es salaam.
DAR ES SALAAM BILA UHALIFU INAWEZEKANA, TUSHIRIKIANE KUISAFISHA JIJI LETU
S.N.SIRRO - CP
KAMISHNA WA POLISI
KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment