Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
ameendelea kupingwa ndani ya chama hicho, na safari hii jumuiya ya
wanawake wa chama hicho ikiibuka na kumtaka ajiweke kando ili kuepusha
mpasuko zaidi.
Aidha,
wamewataka wanawake wafuasi wa chama hicho kote nchini, kuunga mkono
uongozi wa muda uliowekwa na Baraza Kuu la Uongozi wa CUF hivi karibuni,
ambao ulimtangaza Julius Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya
Uongozi ndani ya chama hicho kilichowahi kuwa kikuu cha upinzani
Tanzania.
Akizungumza
na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma jana, Makamu Mwenyekiti wa
Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF, Savelina Mwijage ambaye pia ni
Mbunge wa Viti Maalumu, alisema kauli yao imelenga kuunga mkono hatua
iliyochukuliwa na Baraza la Uongozi dhidi ya wanaotajwa kukiuka Katiba.
Baraza
hilo lilikutana Agosti 28, mwaka huu mjini Zanzibar ikiwa ni hatua ya
kukabiliana na hali ya hewa iliyochafuka baada ya kundi la wanachama
kuvamia Mkutano Mkuu Maalumu wa uchaguzi Agosti 21, mwaka huu jijini Dar
es Salaam.
Mwijage
aliyefuatana na wabunge wengine wanne wa viti maalumu, amesema wanawake
ndani ya CUF wamefedheheshwa na wafuasi wa Profesa Lipumba kwa kufanya
vurugu, kudhalilisha wanawake wakati wa mkutano wa Dar es Salaam na pia
kukisababishia chama hasara ya Sh milioni 600 zilitozumika kugharamia
mkutano huo.
“Tunalaani
kwa nguvu zote vitendo vya baadhi ya watu wanaotaka kukivuruga chama,
lakini pia kuiingiza nchi katika migogoro ya udini, ukabili, ubara na
Uzanzibari. Mbinu hiyo imepitwa na wakati, tunawaomba Watanzania wote
wapuuze siasa hizo za uchochezi,” alisema.
Akizungumza
hatua ya kusimamishwa kwa baadhi ya viongozi 11 wa juu wa chama hicho,
wanaodaiwa kushiriki kukivuruga chama, alisema ni hatua sahihi na kwamba
hata Profesa Lipumba hapaswi kuwa nyuma ya vurugu hizo, kwani aliachia
madaraka kwa hiyari yake wakati chama kikielekea katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka jana.
Kauli
ya wanawake hao wa CUF ilikuja saa chache baada ya Mbunge wa Kaliua,
Magdalena Sakaya ambaye ni mbunge pekee wa kike mwenye jimbo kutoka
chama hicho, kuliambia Bunge kuwa hajatikiswa na uamuzi wa kumsimamisha
uanachama na kwamba anaendelea kutimiza majukumu yake ndani ya chama,
ambacho kabla ya mpasuko wa hivi karibuni, ndiye aliyekuwa Naibu Katibu
Mkuu Tanzania Bara.
Mbali
ya Lipumba na Sakaya, wengine waliositishiwa uanachama ni Abdul Kambaya
ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Ashura
Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib
Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.
Ashura
ni mjumbe wa Baraza Kuu na aliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na
Mawasiliano ya Umma CUF wakati Mnyaa na Kombo, walikuwa wabunge kipindi
cha 2010-2015; Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na Kombo Jimbo la
Chake Chake, kisiwani Pemba.
Kutokana
na kusimamishwa kwa viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar,
Nassor Ahmed Mazrui alimtangaza Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu
Bara kuwa kiongozi wa kamati ya uongozi wa muda, inayowajumuisha pia
Ahmed Katani na Mwijage ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa.
Katani
ni Mbunge wa Tandahimba, Mtwara wakati Severina alikuwa mjumbe wa
kamati kama hiyo ilipoteuliwa Agosti mwaka jana baada ya Profesa Lipumba
kujiuzulu uenyekiti kwa barua ya Agosti 5, mwaka jana.
Baraza
hilo lilimteua pia Joram Bashange kukaimu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu
Bara na Mbaraka Maharagande kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Mawasiliano kwa Umma hadi hapo nafasi hizo zitakapojazwa rasmi
kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Chama hicho.
0 comments:
Post a Comment