Friday, 2 September 2016

#YALIYOJIRI>>>Taarifa Ya Jeshi La Ulinzi La Wananchi Wa Tanzania Kufuatia Habari Iliyoandikwa Kwenye Gazeti La Tanzania Daima.Fahamu zaidi hapa.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limesikitishwa na taarifa iliyotolewa na gazeti la Tanzania Daima toleo Nambari 4290 la tarehe 01 Septemba 2016, ikihusisha shughuli za Jeshi hilo zinazoendelea katika maadhimisho ya miaka 52 ya kuzaliwa kwake na shughuli za kisiasa.

Tunapenda  kuwataarifu wananchi kwamba kazi ya Jeshi ni kulinda na kutetea maslahi ya Taifa na mipaka ya nchi, aidha, Jeshi letu linafanya kazi kwa kufuata mila, desturi, nidhamu, kanuni na sheria za Kijeshi kwa weledi wa hali ya juu, hivyo lisihusishwe na propaganda zozote za kisiasa kwani Jeshi letu ni lenye maadili ya kitaasisi ya hali ya juu. 

Jeshi ni taasisi ya dola wala si taasisi ya kiitikadi, kwa maana uhusiano wake na wanasiasa ni wakati linapotetea na kulinda maslahi ya wananchi.  Inaombwa kuwa makini katika utoaji wa maelezo au malalamiko, iachwe mara moja vyama vya siasa kuingilia ratiba za Kijeshi.  

Ikumbukwe kwamba tarehe 25 Julai kila mwaka ni siku ya kuwakumbuka Mashujaa wetu waliolitumikia Taifa hili kwa umakini na nguvu zote kwa kuleta mafanikio tunayoyaona, na hii ilipitishwa mwaka 1979 wakati Majeshi yetu yanarudi kutoka Uganda baada ya ushindi wa vita vya Kagera. 

Sherehe ya mapokezi hayo yalifanyika mji wa Bunazi Wilaya ya Misenye wakati huo Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera ilipoanzishwa kuwa tarehe hiyo iwe siku ya Mashujaa na kupitishwa Kisheria,  ikabaki siku ya tarehe 01 Septemba kuwa ni siku ya kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, hivyo jana tulikuwa tunasherekea siku ya kuzaliwa JWTZ. Ieleweke hivyo na iachwe mara moja kuchanganya shughuli za Kijeshi na mambo ya Kisiasa, viongozi wa kisiasa wekeni kumbukumbu zenu vizuri.

Jeshi linasisitiza wanasiasa ni vizuri wakasoma vema historia ya nchi wanayotaka kuiongoza na wanayoongoza ili kuepusha upotoshaji, lugha na maneno yanayotolewa na viongozi wa kisiasa wenye matakwa binafsi kuhusisha shughuli za Jeshi na siasa zao yanatia ukakasi na kiungulia, awe makini kuongea vitu ambavyo haelewi na kutokuwa makini zaidi aelewe madhara yanayoweza kutokea kutokana na upotoshaji.

Jeshi letu linafanya shughuli zake ki weredi.

Imetolewa  na  Kurugenzi  ya  Habari  na  Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P  9203,   Dar es Salaam,  Tanzania.
Kwa Mawasiliano zaidi: 0784-477638

0 comments:

Post a Comment