MATUKIO mawili ya mama
kutupa vichanga chooni baada ya kujifungua, yametikisa katika wilaya za
Sikonge na Shinyanga. Katika tukio la wilayani Sikonge, mama akichukua
uamuzi huo ili kulinda ndoa isivunjike, baada ya kupata ujauzito nje ya
ndoa.
Katika tukio jingine, mtoto wa siku moja mwenye jinsia ya kiume, amekutwa ametupwa kwenye tundu la choo la Kanisa la African Inland Tanzania (AICT) lililopo Kitangiri Manispaa ya Shinyanga na kutofahamika mara moja mtu aliyefanya kitendo hicho.
Kutoka Sikonge inaelezwa kuwa Polisi wilayani humo mkoani Tabora, inamshikilia mkazi wa kitongoji cha Ukanga katika kijiji cha Sikonge mjini, Paulina Mussa (21) kwa tuhuma ya kumtupa mtoto aliyejifungua kwenye shimo la choo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Sikonge, Mselemi Maulidi akizungumza na waandishi wa habari, alisema kwamba tukio hilo ni la Januari 19, saa 10 usiku katika Kitongoji cha Ukanga wilayani Sikonge.
Maulidi alisema mtuhumiwa, Paulina Mussa alishikwa na uchungu majira ya usiku wa saa 10, ambapo alitoka nje na kumuacha mume wake akiwa amelala ndani, lakini baada ya muda alirudi ndani.
Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa akiwa ndani, alimueleza mume wake, Saulo Kaombwe kuwa mimba aliyokuwa amebeba, imeharibika huku akimuomba ampeleke hospitali akatibiwe, ambapo mume wake alikubali kumpeleka.
Alisema akiwa Hospitali ya Wilaya, mama mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwenye gazeti, alikwenda kujisaidia katika choo hicho cha jirani yake, ambapo alisikia kichanga kikiwa kwenye shimo la choo kikilia .
Kutokana na hali hiyo, alitoka haraka chooni na kuomba msaada kwa majirani, ambao walifika katika choo hicho na kuamua kukivunja na kukikuta kichanga hicho, kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa saruji uliokuwa tupu.
Baada ya kukitoa kichanga hicho, walikipeleka katika Hospitali ya Wilaya, alipokwenda kutibiwa mama wa kichanga hicho, na walipomhoji alikiri kujifungua na kukitupa kichanga kwenye shimo la choo, jambo ambalo baadhi ya akinamama liliwakera na kuanza kumtembezea kipigo mama huyo, huku baadhi ya wananchi wakituliza ghasia hizo.
Alipoulizwa kwa nini alifanya hivyo, alidai alikuwa anaokoa ndoa yake, kwa kuwa mimba aliyobeba, ilikuwa si ya mume aliyekuwa akiishi naye.
Mmoja wa majirani wa mama huyo, Lameck Benjamin alisema jambo hilo ni la aibu na kuiomba serikali ichukue hatua kali dhidi ya akinamama, wanaofanya tabia ya kutupa watoto huku akiwataka kuacha kubeba mimba, endapo hawataki kuzaa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Hamisi Selemani Issa, alithibitisha kutupwa kwa kichanga hicho na kusema kuwa tayari mtoto huyo, anaendela kupatiwa huduma na mama yake huku wakisubiri kuchukua hatua za kisheria.
Kamanda Issa alitoa wito kwa akina mama, kuacha tabia hiyo ya kuwatupa watoto pasipo kuwa na sababu ya msingi kwani nao wana haki ya kuishi.
Mwingine atupwa kwenye choo cha kanisa Katika tukio jingine, mtoto wa siku moja mwenye jinsia ya kiume, amekutwa ametupwa kwenye tundu la choo la Kanisa la African Inland Tanzania (AICT) lililopo Kitangiri Manispaa ya Shinyanga na kutofahamika mara moja mtu aliyefanya kitendo hicho.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitangiri, Habiba Jumanne aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa majira ya saa 11 jioni ya Januari 20, mwaka huu, alipigiwa simu na baadhi ya waumini wa kanisa hilo, kuwa kuna mtoto mchanga wanasikia sauti yake ndani ya tundu la choo.
Jumanne alisema kuwa mtoto huyo mwenye siku moja, alikutwa kweli kwenye tundu la choo akiwa hai, huku waumini wa kanisa hilo na askari walibomoa choo na kumtoa mtoto huyo, kisha kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
“Tulifanya jitihada za kuvunja choo na kumtoa mtoto akiwa hai, tukamkimbiza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Chakusikitisha
leo asubuhi tumekwenda kuona hali ya mtoto, daktari ametueleza mtoto
amefariki dunia, hatuna jinsi aliyefanya kitendo hicho hafahamiki.
Tunachotaka ni kuomba kibali cha polisi na kwenda kumzika kwa kushirikiana na Kanisa la AICT,” alisema Jumanne.
Mzee wa Kanisa la AICT, David Madata alisema kuwa wakati alipokuwa akifundisha watoto somo la Injili, alimuona mwanamke mmoja akiwa amelala karibu na choo hicho, lakini hakumdhania kama alikuwa na nia ovu.
Alisema baada ya muda, mwanamke huyo aliondoka na kuelekea mahali kusikojulikana na baadaye watu waliokuwa wanaenda chooni, walianza kusikia sauti ya mtoto mchanga akilia chooni, hivyo waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi na serikali ya mtaa.
Kaimu Kamanda Polisi Mkoa wa Shinyanga, Elias Mwita alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo alieleza kuwa mtoto huyo alitupwa kwenye tundu la choo la Kanisa la AICT na mtu ambaye hajafahamika.
Alisema bado wanaendelea na uchunguzi kumbaini aliyehusika na kitendo hicho. Habari hii imeandikwa na Lucas Raphael, Sikonge na Kareny Masasy, Shinyanga.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment