Jumla ya tani 35,491 za chakula zinahitajika ili kukabiliana na hali ya
upungufu wa chakula na lishe kati ya mwezi Februari na mwezi Aprili
mwaka huu unaowakabili watu 1,186,028.
Taarifa hiyo ya serikali imetolewa bungeni leo na Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba wakati akitoa kauli ya serikali
kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula nchini huku akisisitiza kuwa hali
ya upatikanaji wa chakula nchini bado ni wa kuridhisha pamoja na kuwa
baadhi ya maeneo yenye upungufu wa chakula.
Tizeba amesema taarifa hiyo ni kwa mujibu wa matokeo ya tathmini ya
serikali iliyobaini kupungufu huo katika halmashauri 55 nchi nzima.
Aidha amesema kuwa jumla ya watu 118,603 wasio na uwezo wa kupata
chakula watahitaji tani 3,549 za chakula cha bei nafuu kwa haraka na
tayari serikali imeanza kuchukua hatua za kushusha bei ili wananchi
waweze kumudu bei zake.
Amesema kutokana na kuchelewa kwa mvua na mtawanyiko usioridhisha katika
maeneo mengi nchini athari zinazotarajiwa kutokea ni pamoja na
matarajio ya malengo ya uzalishaji wa mazao ya chakula huenda
yasifikiwe, uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo utapungua, uwezekano
wa kuongezeka kwa bei za baadhi ya mazao ya chakula upo, kupungua kwa
mapato yatokanayo na ushuru wa mazao kwa baadhi ya halmashauri.
Athari nyingine ni pamoja na kuongezeka kwa migogoro baina ya wakulima
na wafugaji kutokana na uhaba wa malisho na maji na uwezekano wa
kupungua kwa mapato yatokanayo na mazao ya kilimo yanayouzwa nje ya
nchi, uwezekano wa kuwa na maeneo mengi yenye upungufu wa chakula na
hivyo kuongezeka kwa kiwango cha utapia mlo.
Dkt.Tizeba amesema kuwa ili kukabiliana na athari za ukame tathmini
imebainisha kuwa halmashauri za wilaya hizo 55 zinahitaji jumla ya tani
1,969 za mbegu bora za mahindi, mtama na mizizi inayokomaa kwa muda
mfupi na kustahimili ukame na mbegu hizo zinahitajika ziwafikie mwezi
Februari mwaka huu ili ziweze kupandwa katika msimu wa mwaka 2016 /2017
katika maeneo yanayoendelea kupata mvua wakati huu wa mwaka.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment