Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema hana hofu ya
kuchafuliwa kutokana na tuhuma zinazotolewa dhidi yake, huku akisema
msimamo wake uko palepale na kwamba anamtambua Profesa Ibrahim Lipumba
kama Mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif ni Katibu Mkuu.
Kauli
ya Jaji Mutungi imekuja baada ya taarifa na kauli za matusi na kejeli
zilizomuhusisha yeye na ofisi yake kusambaa kwenye mitandao mbalimbali
ya kijamii baada ya kuidhinisha zaidi ya Sh300 milioni za ruzuku kwenda
kwenye akaunti ambayo kamati ya uongozi ya CUF ilidai siyo ya chama
hicho.
Taarifa
za msajili kuingiza fedha hizo kwenye akaunti hiyo na baadaye kutolewa
kwa njia ambayo inaonekana kutia shaka zilitolewa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ambaye alilinganisha suala hilo
na uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni zilizokuwa kwenye akaunti ya
Tegeta Escrow.
Kupitia
taarifa yake jana, Jaji Mutungi alisema kuna mbinu zinazopangwa na
wanaojiita Kamati ya Uongozi ya CUF ambayo ofisi yake haiitambui, huku
akisisitiza kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF na Maalim
Seif kuwa Katibu Mkuu.
Jaji
Mutungi ambaye mwishoni mwa mwaka jana alifunguliwa kesi Mahakama Kuu
na bodi ya wadhamini wa CUF ikiiomba itoe amri ya kubatilisha barua ya
mlezi huyo wa vyama vya siasa inayomtambua Profesa Lipumba kuwa
mwenyekiti wa CUF, alisema kauli zinazotolewa mitandaoni zina lengo la
kuchafua ofisi yake.
“Tayari
mbinu hizo zimeanza kutekelezwa na viongozi wa kamati hiyo kwa
kusambaza habari za kudhalilisha katika vyombo mbalimbali vya habari na
mitandao ya kijamii kama Facebook na mingineyo,” alisema.
Msajili
huyo alisema moja ya mkakati huo ni taarifa iliyosambazwa juzi na Kaimu
Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF,, Mbarala Maharagande ya kejeli,
matusi, tuhuma na dhihaka kwake.
Jaji
Mutungi alisema hivi karibuni, Maharagande alizungumza na waandishi wa
habari huku akidai kuwa ofisi ya msajili inasababisha mpasuko ndani ya
chama hicho na ndiyo maana imetoa ruzuku kwa Profesa Lipumba.
Licha
ya tuhuma hizo, Jaji Mutungi alisema kwamba haogopi kuchafuliwa
akizingatia ukweli kwamba yeye ni mtumishi wa umma na anafanya kazi zake
akiwatumia wananchi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisema kamwe hawezi kuyumbishwa na matusi wala kejeli zinazotolewa dhidi yake pamoja ofisi anayoiongoza.
“Nimezipata
hizo taarifa kwamba kuna baadhi ya watu wamepanga kupambana nami kwa
kunichafua, japo naendelea kuzifanyia kazi lakini waache wanichafue,
wala siogopi lolote,” alisema.
Hata
hivyo, Jaji Mutungi alisema mjadala wa ruzuku ya CUF aliyotoa kwa chama
hicho ameshaufunga na anashangazwa na maneno yanayozidi kusambazwa na
watu wanaojiita viongozi wa CUF.
Alipotafutwa
kuzungumzia tuhuma hizo, Maharagande aliendelea kusisitiza kuwa kauli
iliyotolewa wakati alipofanya mkutano na vyombo vya habari ipo hivyo na
kwamba waliitisha mkutano kumjibu msajili ambaye alifanya mkutano na
waandishi wa habari siku moja kabla kuhusu masuala ya CUF.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment