WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba,
amesema zipo kila dalili ya nchi kukumbwa na upungufu wa chakula, hivyo
wanasiasa bila kujali itikadi zao, wanapaswa kuungana kubuni mikakati na
hatua za kuchukua kudhibiti hali hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti
huyo wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema si sahihi
kuendelea kubishana kuwa nchi ina njaa au haina, wakati dalili
zinaonesha uwezekano wa kukumbwa na upungufu wa chakula.
“Watanzania tuwe pamoja kulikabili hili
kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma. Hili ni suala la kitaifa, ni
lazima tuungane kujua wakati huu tunafanya nini na hali ikiharibika
tufanye nini, tusilifanye suala hili kuwa la kisiasa,” alionya Jaji
Warioba.
Alisema nchi kukumbwa na upungufu wa
chakula ni jambo la kawaida na si jipya, kwa vile limekuwa likitokea
miaka ya nyuma kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo mvua kutonyesha
kwa wakati.
Huku akieleza jinsi Rais wa Awamu ya
Kwanza, Julius Nyerere alivyokuwa akihimiza wananchi kulima na kuhifadhi
chakula ikitokea nchi inakumbwa na upungufu wa chakula, alitaja mambo
manne yanayopaswa kufanyika ili kukabiliana na kadhia hiyo.
Sakata la nchi kukumbwa na njaa liliibuka
katika maeneo mbalimbali huku vyombo vya habari vikiripoti taarifa za
wananchi kushindia maembe na mifugo kufa, kutokana na ukame.
Wanasiasa na wasomi walizungumzia jambo
hilo na kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka huku viongozi wa dini
wakienda mbali zaidi na kuwataka waumini wao wafanye hija, mfungo,
mikesha na maombi ili kunusuru hali hiyo.
Jumatatu wiki hii, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa alisema Serikali itagawa tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki
msimu uliopita katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kupunguza kasi ya
ongezeko la bei za vyakula nchini, lakini akakana taarifa kuwa nchi ina
njaa.
Wakati Majaliwa akitoa ufafanuzi huo,
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, alisema Serikali
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), katika mwaka wa
fedha wa 2016/17 imepanga kununua tani 100,000 za chakula, na hadi
Januari 8, wakala huyo alikuwa amenunua tani 62,087 za mahindi.
Lakini jana, Jaji Warioba alisema licha ya
nchi kujitosheleza kwa chakula kuna baadhi ya maeneo yana upungufu
unaosababisha utegemezi wa chakula kutoka sehemu zingine za nchi.
“Ndiyo maana tumekuwa na mikoa ambayo
inasikifika kwa uzalishaji chakula. Lakini mwaka huu kwa dalili hizi na
mambo yanayoambatana na mabadiliko ya tabianchi, inaonekana kutakuwa na
upungufu wa chakula kwa sehemu kubwa,” alisema.
Aliongeza, “hii inatokana na mvua kutonyesha kama inavyotarajiwa. Hili si jambo jipya limewahi kutokea miaka ya nyuma.”
Alisema kwa kuwa kuna dalili za upungufu wa chakula ni lazima kujiandaa kukabiliana na hali hiyo, ikiwamo kuhadharisha wananchi.
“Pia lazima kusaidia wananchi kutumia njia
zitakazowawezesha kupata mazao. Hilo linapaswa kufanywa na Serikali na
watu wa kada mbalimbali. Hapa wananchi wanaweza kupewa elimu au mbegu
zinazostahimili ukame,” alisema.
Alisema, “bado tuna muda maana kuna sehemu
ambazo zinapata mvua za vuli. Licha ya mvua kutonyesha kama
ilivyozoeleka, wananchi washauriwe kuzitumia vizuri, ni wajibu wa
Serikali kusaidia wananchi hata kama wanahitaji mbegu.”
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, nchi
inapokumbwa na upungufu wa chakula, wananchi pia wanapaswa ama kulima au
kuhifadhi chakula na si kusubiri Serikali ishughulikie suala hilo.
“Nakumbuka mwaka fulani nchi ilikumbwa na
upungufu wa chakula, Serikali iliwataka wananchi walime. Nakumbuka
Nyerere aliwaeleza wananchi walime, la sivyo tutakufa na watu walilima
kila mahali,” alisema na kuongeza:
“Wenye uwezo wanunue chakula na kukitunza.
Haifai tuanze kulumbana, maana mwisho wa siku Serikali itajitahidi
kuziba pengo la upungufu kama upo,” alisema.
Aliongeza kuwa viongozi bila kujali vyama,
jambo la kwanza wanalopaswa kufanya ni kuhimiza wananchi watumie mvua
zinazonyesha sasa kupanda mazao, pili, kutathmini hali ilivyo na kama
itatokea waamue watafanya nini.
Alisema si sahihi kuendelea kubishana kuwa
nchi ina njaa au haina njaa, wakati dalili zinaonesha uwezekano wa
kukumbwa na upungufu wa chakula.
“Watanzania tuwe pamoja kulikabili hili,
kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma. Hili ni suala la kitaifa hivyo ni
lazima tuungane,” alisema.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment