Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam wa Kanisa la Anglikana, Dk valentino
Mokiwa jana alishindwa kuendesha vikao viwili baada ya kundi la waumini
kufika Usharika wa Ilala kwa lengo la kuzuia.
Askofu Mokiwa,
ambaye anapinga uamuzi wa Askofu Mkuu wa Anglikana, Dk Jacob Chimeledya
kumvua madaraka kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, alikuwa
aendeshe vikao vya kamati ya fedha na halmashauri kuu, lakini
alilazimika kuviahirisha baada ya kundi hilo kufika eneo hilo.
Wakati
waumini hao wakizuia vikao hivyo kufanyika, mashemasi, mapadri,
wainjilisti na waumini wa dayosisi hiyo wametoa tamko la kumuunga mkono
Dk Mokiwa wakipinga uamuzi wa mkuu wa kanisa hilo kumvua madaraka.
Askofu
Mokiwa anapinga uamuzi wa kumvua madaraka akisema hauwezi kufanywa na
mkuu wa kanisa, bali na halmashauri kuu ya jimbo ambayo anasema
haikushirikishwa zaidi ya kutaarifiwa uamuzi huo.
Tukio la jana
la kumzuia Dk Mokiwa kufanya mkutano lilitokea saa mbili asubuhi katika
Kanisa la Mtakatifu Nicolau wilayani Ilala, ambako kuna ofisi ya Askofu
wa Dayosisi ya Dar es Salaam.
Mmoja wa watu walioshiriki kuzuia
vikao hivyo, Haule Sylvester ambaye alijitambulisha kuwa kiongozi wa
waumini wa Anglikana jijini Dar es Salaam, alisema walichukua uamuzi huo
kwa kuwa Dk Mokiwa ameshavuliwa uaskofu.
“Huyu (Dk Mokiwa)
hapaswi kufanya shughuli zozote za kanisa kwa sababu si askofu. Lakini
amekuwa akiendesha vikao vya siri na mapadri wanaomuunga mkono,” alisema
Sylvester.
“Jana (juzi) alifanya kikao cha siri. Leo (jana)
alikuwa aongoze vikao viwili, kikiwamo cha bodi ya fedha ya dayosisi
hii, ndiyo maana tumemzuia.”
Alifafanua kuwa baada ya kikao
hicho cha fedha kilichokuwa kimepangwa kuanza saa 3:00 asubuhi, kikao
ambacho kingefuata ni cha halmashauri kuu ya dayosisi ambacho kingefanya
uamuzi wa mambo ambayo yangejadiliwa na bodi ya fedha.
Sylvester
alisema kwa mujibu wa katiba ya dayosisi hiyo, vikao hivyo vyote
vinatakiwa viongozwe na mwenyekiti ambaye ni askofu wa dayosisi.
Alisema
halmashauri ina wajumbe 10 akiwamo askofu wa dayosisi, wakati kikao cha
bodi ya fedha kina wajumbe zaidi ya 200 na kina lengo la kupanga bajeti
ya mwaka.
“Ki utaratibu ili kuendesha vikao hivi, lazima uwe
askofu wa jimbo la Dar es Salaam. Tunamsihi Mokiwa aache kufanya kazi na
kutumia ofisi kwa kofia ya uaskofu,” alisema.
Alisema waumini wengi walipanga kushiriki katika mchakato huo, lakini walienda 20 baada ya kutoa taarifa polisi.
Alipoulizwa
kuhusu suala hilo, Yohana Sanga ambaye ni ofisa habari wa Dk Mokiwa
alisema vikao hivyo vilikuwa vya kawaida vya dayosisi hiyo na vililenga
kujadili maendeleo ya kanisa.
“Tulishangaa kuona kundi lile la
watu, ambalo chimbuko lake limetoka Kanisa la Magomeni linalompinga
Askofu Mokiwa,” alisema.
Mbali na kundi hilo, kilichowasikitisha zaidi
ni kuona magari sita ya polisi, wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU), yaliyokuwa yameegeshwa nje ya kanisa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Ilala, Salum Hamduni alisema kuwa askari hao walikuwa katika doria ya kawaida.
Sanga
alisema baada ya kundi hilo kufika katika eneo hilo, liliingia moja kwa
moja kanisani na walipowauliza walijibiwa kuwa wanakwenda kujadili
masuala ya kanisa.
Alisema baada ya kuona hivyo, walisita
kufungua ofisi iliyoandaliwa kwa ajili ya vikao na baada ya majadiliano
ya muda mrefu, waliahirisha.
“Walivyoona hatufungui ofisi, waliamua kuondoka kwa mafungu.Lengo lao lilikuwa kuvunja vikao hivi,” alisema Sanga.
Taarifa
ya viongozi hao wanaomuunga mkono Askofu Mokiwa, inasema bado
wanaendelea kumtambua na kumuunga mkono kiongozi huyo kama askofu wa
Dayosisi ya Dar es Salaam na kwamba uamuzi uliochukuliwa dhidi yake ni
batili.
Hivi karibuni, Askofu Mkuu, Chimeledya alimtaka Dk
Mokiwa ajiuzulu kwa kile alichodai kuwa anatumia vibaya madaraka yake na
ubadhirifu wa fedha.
Hata hivyo, Dk Mokiwa alikanusha madai hayo na kusema mgogoro wa kanisa hilo ni wa kutengenezwa na maadui zake.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment