RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof.
Mussa Assad kwa mwaka wa fedha 2015/16, imefichua udhaifu mkubwa katika
mradi wa mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam.
Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni mjini hapa juzi, CAG Assad
anasema kuwa katika ukaguzi wake alioufanya kwenye mradi huo, amebaini
Wakala wa Usafiri wa Mwendokasi Dar es Salaam (DART) una upungufu
mwingi.
Anasema katika utoaji wa huduma ya usalama katika vituo vya DART na
makao makuu ya wakala Jangwani, amebaini kuwa Mei 5, 2016 DART iliingia
mkataba wa miezi 12 na M/S China Tanzania Security Company Ltd wa utoaji
huduma ya ulinzi kwenye vituo vya DART na Jangwani kwa jumla Sh.
milioni 178.652.
Hata hivyo, Prof. Assada anasema kuwa katika mapitio ya taratibu za
manunuzi, imebainika matangazo na zabuni zilizotolewa hazikuwasilishwa
PPRA, mkataba ulisainiwa baada ya tarehe ya kukamilisha mkataba kuisha
kinyume cha Kanuni 370(1) cha Kanuni ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013
na pia nakala ya mkataba haikuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG) kwa ajili ya kupitia na kuhakikiwa (vetting) kinyume cha
Kanuni 59(1) na (2) vya Kanuni ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013.
"Kutokana na mazingira hayo ni vigumu kuthibitisha kwamba taratibu
sahihi za manunuzi zilifuatwa katika utoaji wa huduma za usalama, na
iwapo matumizi ya Sh. milioni 178.652 yalikuwa matumizi sahihi ya fedha
za umma," anasema.
CAG Assad anapendekeza kuwa menejimenti ya DART ifuate sheria na kanuni
za usimamizi wa mikataba, na kuweka mikakati ya jinsi ya kutatua
upungufu unaojitokeza, hivyo wahakikishe Wakala wa Serikali na taasisi
nyingine wanaimarisha mifumo ya ndani ili kuhakikisha upungufu
haujitokezi kwa baadaye.
CAG pia anasema kuwa katika ukaguzi wake wa mwaka wa fedha 2015/2016,
amebaini kwamba DART ilinunua bidhaa na huduma za jumla ya Sh. milioni
332.653 nje ya mpango wa manunuzi kwa ajili ya kukodi sehemu ya ndani,
nishati na mnara wa mawasiliano kwa Sh. milioni 154 na kutoa huduma ya
usalama katika vituo vyake na kituo kikuu cha Jangwani kwa kiasi cha Sh.
milioni 178.652.
Anasema manunuzi hayo ni kinyume cha Kanuni 69(3) ya Kanuni ya Manunuzi
ya Umma ya Mwaka 2013 inayotaka taasisi inayofanya manunuzi kufanya
makisio sahihi ya mahitaji ya bidhaa na huduma na kazi.
Anasema jumla ya mapato ya Sh. milioni 90.499 yaliyoonyeshwa kwenye
taarifa za fedha yaliyotokana na matangazo katika miundombinu ya DART
hayakuwa na uthibitisho zikiwamo nyaraka za manunuzi ya zabuni, jambo
ambalo ni kinyume cha Kanuni 55(1) cha Kanuni ya Manunuzi ya Umma ya
Mwaka 2013, hivyo ilishindikana kuthibitisha usahihi wa taratibu za
manunuzi.
"Napendekeza kuwa wakala wa serikali wafuate taratibu za manunuzi na
kuandaa mikataba kwa kila taasisi inayotumia miundombinu ya DART kufanya
matangazo," anasema.
Prof. Assad anaongeza kuwa katika ukaguzi wake wa mwaka 2015/2016,
amebaini Sh. milioni 372.6 zilitakiwa kulipwa na meneja wa mfuko wa ISP
kwenda DART kama ada ya ISP kati ya Mei 16, 2016 na Juni 30, 2016,
lakini hadi kufikia Juni 2016, kiasi cha Sh. milioni 85 kililipwa na
kubaki kiasi cha Sh. milioni 287 ambazo hazijalipwa na ISP kupitia
meneja wa mfuko DART, jambo ambalo anasema ni kinyume cha makubliano
kati ya DART na UDART ya Mei 31, 2016 ambapo meneja wa mfuko alitakiwa
kufanya malipo ya kila siku ya Sh. milioni 8.1 kwa wakala kama ada ya
upatikanaji wa huduma.
"Na ikiwa siyo siku ya kazi, malipo yafanyike siku ya kazi inayofuata.
Kutokulipa ada ya upatikanaji wa huduma kunaathiri ukwasi wa wakala, na
hivyo kuchelewesha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa," anasema CAG
Assad.
Hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Rais John Magufuli
aliwataka mawaziri mawili; Prof. Makame Mbarawa (Ujenzi) na George
Simbachawene (Tamisemi) kueleza faida za awamu ya kwanza mradi huo
unaotekelezwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia (WB), agizo ambalo lilionekana
kuwa gumu kwa Simbachawene huku waziri mwenzake akieleza kuwa jukumu
lake katika mradi huo lilikuwa kusimamia ujenzi wa miundombinu na
masuala ya faida za uendeshwaji wake yako Tamisemi.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment