MKUU wa Idara ya
Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro ameomba msamaha Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) asamehewa adhabu ya mwaka mmoja kujihusisha na
masuala ya soka.
Julai mwaka jana, Muro alifungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya
soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. milioni 3 baada ya kukutwa na hatia
katika mashtaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF dhidi
yake.
Katika barua yake kwa TFF, Muro amesema kwamba anakiri kupata barua ya
kufungiwa kutoka Kamati ya Maadili, lakini anaomba msamaha baada ya
kutumikia nusu ya adhabu yake.
Muro ameomba apunguziwe adhabu na kurudi kutekeleza majukumu yake kwa
mwajiri wake Yanga kuanzia kipindi hiki cha michuano ya Kombe la
Mapinduzi, inayoendelea visiwani Zanzibar.
Mapema wiki iliyopita, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa mahasimu, Simba, Hajji Manara alimwombea msamaha Muro.
Aidha, wasemaji wa timu nyingine akiwemo Massau Bwire wa Ruvu Shooting
walimwombea msamaha pia mwenzao huyo, wakiamini atakuwa amejirekebisha.
Muro alifungiwa Julai 8 mwaka jana baada ya kikao cha Kamati ya Maadili
ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Wakili
Wilson Ogunde kilichofanyika mjini Dar es Salaam.
Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu
ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 5 baada ya
kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo.
Kwa kosa hilo akahukumiwa kutengana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja
wakati shtaka lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na
kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika
kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.
Katika shtaka hilo, Jerry anadaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga
kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba kwenye mchezo huo ambao timu yake
ilifungwa 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa kuishinda TFF katika shtaka la
kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki
za matangazo ya televisheni.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment