Siku
moja baada ya vigogo watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
kushushwa vyeo, uongozi wa shirika hilo umesema utaendelea na fagio hilo
kama njia ya kuongeza ufanisi kwenye utendaji.
Vigogo
hao wa ngazi za juu ambao ni wakurugenzi, wamehamishiwa Chuo cha
Mafunzo cha Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika linaboresha ufanisi
wake.
Walioshushwa vyeo ni pamoja na Declan Mhaiki aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia usambazaji wa umeme.
Wengine
ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji na Huduma kwa Mteja, Mhandisi
Sophia Mgonja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji Umeme, Nazir
Kachwamba.
Wakati
hao wakipitiwa na panga hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu,
Watson Mwakyusa, aliamua kuandika barua kuacha kazi mwenyewe.
Juzi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alisema jana wangetoa taarifa kuhusu hamisha hamisha hiyo.
Jana
mchana Idara ya Kitengo cha Mahusiano cha Shirika hilo, kilitoa taarifa
na kusema kuwa wataendelea na hatua mbalimbali za mabadiliko ya uongozi
kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa mabadiliko yanayoendelea ndani ya Tanesco yatawekwa
wazi wakati mwafaka kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za shirika
kupitia vyombo vya habari.
Kitengo hicho kilieleza kuwa kwa sasa bado wanaendelea na panga pangua na endapo watakamilisha watatoa taarifa kwa umma.
“Tunaomba
vyombo vya habari vitoe fursa kwa mamlaka husika kuendelea kukamilisha
zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla na
taarifa rasmi itatolewa baada ya zoezi kukamilika,’’ ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Januari
Mosi, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alimteua Dk. Mwinuka kuwa Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, baada ya kumng’oa aliyekuwa mkurugenzi
wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Mramba
alitenguliwa uteuzi wake siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la
kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akiwa
mjini Bukoba kwenye ibada ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli alisema amekerwa
na kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kujitokeza
hadharani na kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama uamuzi wa
Serikali bila kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.
Kutokana na hali hiyo, alisema watendaji hao ni miongoni mwa majipu yanayostahili kutumbuliwa.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment