HII unaweza ukaihesabu kama ni vita mpya baina ya mahasimu wa soka nchini, Simba na Yanga.
Hali hiyo inaletwa na mkakati wa siri
ambao Dimba imeugundua ambapo vigogo wa timu ya Simba wameamua kuingia
vitani kumshawishi na kisha kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa
Yanga, Donald Ngoma, muda mfupi baada ya kumaliza mkataba wa kuitumikia
timu hiyo ya Jangwani.
Ngoma, ambaye ni raia wa Zimbabwe,
anamaliza mkataba wake sambamba na kuhitimishwa kwa michuano ya Ligi Kuu
Tanzania Bara Mei, mwaka huu.
Habari za uhakika ambazo Dimba
limezipata kutoka kwa mmoja wa viongozi waliokuwamo katika kamati ya
usajili zilisema kwamba, mchezaji huyo anapigiwa mahesabu na klabu hiyo
ya Msimbazi kutokana na uwezo wake anaoendelea kuuonyasha katika klabu
ya Yanga.
Mjumbe huyo alibainisha kuwa, hata
hivyo, klabu yake inamtaka straika huyo siyo kwa ajili ya kucheza
michuano ya Ligi Kuu, bali wanamtaka kwa ajili ya kuiongezea nguvu timu
hiyo katika michuano ya kimataifa, ambapo wenyewe Simba wanaamini
watatwaa ubingwa msimu huu na hivyo watakuwa wakishiriki michuano hiyo
hapo mwakani.
Mjumbe huyo amekwenda mbali zaidi na
kudai kwamba, tayari dau la mshambuliaji huyo limeshawekwa mezani ambapo
Wekundu hao wa Msimbazi watatakiwa kulipa kiasi cha Dola za Kimarekani
150,000, sawa na Sh milioni 300 za Kitanzania ili kuweza kumnasa
Mzimbabwe huyo.
“Kiasi hicho tunaweza kutoa, lakini hii
itawezekana endapo tutapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa
hapo mwakani,” alisema.
Wakala wa mchezaji huyo, Jonas Tiboroha,
alikiri kupigiwa simu na kigogo mmoja wa Simba, ambaye hakutaka kuweka
wazi jina lake na kuomba taratibu za kumsajili mchezaji huyo.
Tiboroha alisema, licha ya Simba, pia
klabu za Mamelodi Sandown, Malaga FC za Afrika Kusini, Zesco ya Zambia,
Al Ahly ya Misri zimeonyesha nia ya kumhitaji mshambuliaji huyo, lakini
pia klabu yake ya sasa, Yanga nao wameshaonyesha nia yao ya kumbakiza
mshambuliaji wao huyo ambaye hadi sasa ameshaipachikia timu yake hiyo
mabao 8 katika michuano ya Ligi Kuu.
Alisema, Yanga wameweka ofa ya Sh milioni 120, kwa ajili ya mkataba mpya wa Mzibambwe huyo baada ya ule wa kwanza kumalizika.
Katika hatua nyingine, vigogo karibu
wote wa klabu ya Simba wiki iliyopita walikutana kwa siri katika sehemu
nyeti inayofahamika kwa jina la Pentagoni, iliyopo maeneo ya daraja la
Salenda, katikati ya jiji la Dar, ambapo pamoja na mambo mengine,
walijadili na kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanachukua
pointi zote 18 zilizobaki ili waweze kuchukua ubingwa msimu huu.
Vigogo hao wa kamati ya utendaji pamoja
na wadau wengine, wakiongozwa na Rais wa klabu hiyo, Evance Aveva,
wamekuwa wakikutana mara kwa mara katika kipindi hiki ambacho timu yao
iko kileleni katika msimamo wa ligi, huku wakielekea kusafiri kwenda
kanda ya ziwa kwa ajili ya kucheza mechi tatu ambazo ndizo zitakazotoa
mwanga wa timu hiyo kutwaa ubingwa au la.
Hata hivyo, Aveva aliliambia Dimba
kwamba, kukutana kwao ni kawaida kama viongozi na wadau kwa ajili ya
kujadili maendeleo ya timu yao, lakini bado kikosi chao hicho kitakuwa
na mikakati ya kifundi inayoendelea kuandaliwa na benchi la ufundi chini
ya kocha wake mkuu, Joseph Omog.
“Kocha ndiye anayejua masuala ya ufundi,
ukisikia sisi tukikutana ujue tunapanga mikakati mingine, maana klabu
si wachezaji pekee, bali na viongozi pia wana majukumu ya kuhakikisha
mambo yanakwenda sawa.
Naye Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog,
amesema katika wakati wowote aliokuwa akiifundisha Simba, kipindi hiki
ndicho kinachomuweka katika wakati mgumu, hasa kutokana na umuhimu wake.
Kocha huyo aliliambia Dimba kwamba,
anafahamu mechi zilizobaki ni ngumu, hivyo miongoni mwa mambo muhimu
anayotakiwa kuyahakikisha ni kuwaweka vijana wake katika hali ya
tahadhari ili wasijiachie wakadharau mechi zilizosalia.
Endapo ratiba haitabadilika Simba
itakipiga na Kagera Sugar Aprili 4, mwezi ujao na kisha itakwenda jijini
Mwanza kukipiga na Toto Africans na kisha itacheza na Mbao, mechi
ambazo kocha huyo alisema ni ngumu na zinazohitaji mikakati ya nguvu.
Mpaka sasa Simba ndiyo inayoongoza Ligi
Kuu ikiwa na pointi 55, ikifuatiwa kwa karibu na watani wao wa jadi,
Yanga, iliyofikisha Pointi 53, huku zote zikiwa zimeshacheza michezo 24.
Credit - Dimba
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment