MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), amedai kupewa taarifa na
mawaziri kuwa muda wowote anaweza kuuawa na kikundi maalumu
kinachoendesha utekaji nchini.
Aidha, Bashe amedai kuwa mbali na yeye kuwa katika hatari hiyo, pia
ameambiwa na mawaziri hao wa serikali kuwa kuna wabunge wengine 10 ambao
wanawindwa na kikundi hicho na wametahadharishwa 'kuwa makini
barabarani'.
Bashe (41), aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana asubuhi aliposimama
na kukiomba Kiti cha Spika kuahirisha shughuli za Bunge ili kujadili
hoja ya dharura akitumia Kanuni ya 47(1),(2)na (3) vya Kanuni za Kudumu
za Bunge toleo la Januari 2016.
Huku akiungwa mkono na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema)
na kushangiliwa na baadhi ya wabunge, Bashe alisema kumekuwa kukitokea
matukio ya sintofahamu yanayowahusu wabunge na raia wa kawaida
yanayoendeshwa na kikundi hicho ambacho alidai kinatoka idara nyeti
serikalini.
Katika kujenga hoja yake, Bashe alisema Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku
(CCM), mbunge wa zamani Mkuranga mkoani Pwani, Adam Malima (CCM), msanii
Roma Mkatoliki na yeye mwenyewe ni miongoni mwa watu waliowahi kutekwa
huku akikumbushia pia madai ya kupotea kwa Ben Saanane ambaye ni
msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Aliliomba shughuli za Bunge ziahirishwe ili wabunge wajadili jambo la
dharura ambalo limekuwa likitokea kwa muda mrefu katika nchini.
"Miongoni mwa watu waliowahi kutekwa ni Mheshimiwa Musukuma (Joseph
Kasheku), Mheshimiwa Bashe kwenye mkutano mkuu wa CCM, ndugu Malima, Ben
Saanane amepotea... (makofi), juzi amepotea Roma Mkatoliki," alisema
Bashe huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge kwa kugonga meza.
Alisema zaidi: "Nasema ni jambo la dharura kwa sababu hawa ni wale ambao
wanafahamika. Hatujui Watanzania wangapi hawafahamiki katika ngazi za
chini.
"Na zipo taarifa ambazo binafsi nimezipokea kutoka kwa baadhi ya
mawaziri, wakinitahadharisha mimi binafsi kwamba 'Bashe kuwa makini,
wewe ni mmoja kati ya wabunge 11 ambao wamewekwa katika 'list' (orodha).
Mkikaa barabarani vibaya, mnaweza kupoteza maisha yenu'.
"Nasema jambo hili ni dharura kwa sababu kikundi hiki kilichomo ndani ya
idara ya ... (alitaja idara nyeti), ambacho kimeamua kuchukua mamlaka
haya ya kuteka watu, kinaharibu heshima ya serikali yetu, kinaharibu
heshima ya chama changu ambacho mimi na wabunge wenzangu wa CCM,
tuliomba ridhaa ya kutaka kuwaongoza Watanzania na siyo kuwahatarishia
maisha yao."
Bashe alimuomba Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kuruhusu jambo
hilo lijadiliwe na wabunge na ikiwezekana chombo hicho cha kutunga
sheria kiunde kamati maalumu ya kuchunguza jambo hilo.
Bashe pia alimuomba Naibu Spika kutumia mamlaka yake kuiagiza Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Usalama na Mambo ya Nje kufanya kazi changamoto hiyo
na kulipatia Bunge taarifa kwa ajili ya usalama wa nchi.
"Hali ya nchi siyo salama, Watanzania wana taharuki, Watanzania
wanajadili mambo haya katika mitandao na 'there is no statement' (hakuna
kauli) toka serikali.
Waziri wa Mambo ya Ndani..." Bashe alisema huku akikatishwa na Naibu
Spika ambaye alimtaka aketi ili Kiti cha Spika kiangalie Kanuni ya 47
inaeleza nini kuhusu madai yake.
Kabla ya kutoa uamuzi wa Kiti kuhusu madai ya Bashe, Naibu Spika alitoa
nafasi kwa Sugu kueleza hoja yake bungeni baada ya mbunge huyo kusimama
na kuomba kupewa nafasi ya kuwasilisha hoja ya dharura bungeni.
Akitumia Kanuni ya 47, Sugu aliunga mkono hoja ya Bashe kwamba Bunge
liahirishe shughuli zake za jana na kujadili hoja ya dharura ya kadhia
ya utekaji na kupotea kitatanishi kwa watu nchini.
"Taifa limekuwa gizani kwa utamaduni mpya uliozuka wa kuteka watu,
utamaduni ambao si wa kwetu, ni utamaduni wa kimafia, utamaduni ambao
kwa mara ya mwisho kwenye mipaka ya Bara na visiwani, tuliusikia
alipotekwa Mzee Kassim Hanga kule Zanzibar miaka hiyo," Sugu alisema.
"Lakini tangu kipindi hicho haujakuwapo tena. Toka operesheni hii ya
kuteka watu nyara ianze, kila anayehusika na usalama likiwamo Jeshi la
Polisi, 'always' (mara kwa mara) wanasema 'hatujui, hatujawaona kwenye
vituo vyote'.
Nchi inabaki kwenye tahayari, kapotea Ben Saanane, mara miili sita, saba
imeopolewa kwenye Mto Ruvu ikaenda kuzikwa bila kufanyiwa 'post-mortem'
(uchunguzi) kwa amri ya ambaye hatujui ni nani.
"Bashe alitekwa, Nape (Nnauye) alitekwa, akaokolewa na Maulid Kitenge,
vinginevyo pengine angekuwa ametekwa, hakuna mtu aliyezungumza kitu."
Kutokana na changamoto hiyo mpya nchini, Sugu alimshauri Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kuachia ngazi ili kulinda heshima
yake kama kweli bado ana matumaini ya kuwa Rais wa Tanzania.
"Waziri wa Mambo ya Ndani yuko kimya mpaka najiuliza kama anabanwa kiasi
hicho, huyu ni mtu 'potential' (muhimu) ambaye alifikia hatua ya
kugombea urais na bado ana 'future'," Sugu alisema.
"Kwanini asijiuzulu, akalinda heshima yake kuliko kukaa kwenye 'mess' (aibu)? Alihoji Sugu. "Kujiuzulu ni utamaduni mzuri.
Mzee (Alhaji Ali Hassan) Mwinyi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani miaka
hiyo, mwaka '76, ikatokea messy (kuboronga), 'aka-bounce back'
(akarejea), miaka ya '80 akaja kuwa Rais wa nchi hii.
"Ndugu yangu Mwigulu, nikushauri kama hushirikishwi, mambo yanafanyika, hamna mtu anakuja na majibu.
"Lakini juzi baada ya kutekwa Roma Mkatoliki, tumepata mwanga. Yupo mtu
Dar es Salaam alituambia anajua Roma aliko na angerudi kabla ya
Jumapili.
"Kama Waziri Kivuli (wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), nikatoka
Jumamosi na 'ku-demand' (kuagiza) kwamba aachiwe siku ileile na
akaachiwa, nashukuru Mungu. Sasa basi, hatujui nani 'next' (anayefuata)
atatekwa. Yawezekana Sugu ingawa mimi 'I don't care much' (sijali) kwa
sababu Mbeya wataziba nafasi yangu.
"Lakini Naibu Spika 'it could be you' (yaweza kuwa wewe). 'It is the
war' (ni vita), 'no body is safe' (hakuna aliye salama. Kwanini Bunge
hili lisijadili na hatimaye limlazimishe Bashite kama alivyojua kwamba
Roma Mkatoliki yuko wapi na angemrudisha Jumapili, tumlazimishe sasa
Bunge hili tujadili na baadaye tumlazimishe Bashite atutajie aliko Ben
Saanane na atutajie kwamba ili miili iliyotupwa Ruvu na kuzikwa haraka
haraka bila kufanyiwa 'post-mortem' ni ya kina nani kwa sababu huyu
anaonekana anajua undani wa mambo haya."
KULIPATIA UFUMBUZI
Akijibu maombi ya wabunge hao, Naibu Spika alikataa kuruhusu jambo hilo
kujadiliwa bungeni kwa kupitia utaratibu wa hoja ya dharura kwa kuwa
vyombo vya sheria vinaweza kulipatia ufumbuzi.
Dk. Acskon alisema jambo la dharura linaloweza kusababisha kuahirishwa
kwa shughuli za Bunge kulijadili ni lile lenye maslahi kwa umma na iwapo
utatuzi wake unategemea zaidi ya utekelezaji wa kawaida wa sheria.
"Waheshimiwa Bashe na Sugu wameeleza kwa kirefu kuhusu jambo ambalo
limetokea hapa na pale, lakini pia tumeliona kwenye vyombo vya habari na
tumelisoma," Dk. Ackson alisema.
"Maelezo yao kwa ujumla yanahusu mambo ambayo yanawapata wananchi ambayo
watu kadhaa wametajwa kama mifano kwamba wamekuwa wakitekwa ama
wamekuwa wakikamatwa.
"Sasa, nadhani wote tunafahamu matakwa ya Kanuni ya 47, hili jambo la
hawa watu kukamatwa ama kutekwa kwa sababu sasa hata wale waliokamatwa,
na wao wamewekwa kwenye kundi la kutekwa. Sasa sijui kama tunaweza
kuyatenganisha haya mambo mawili; nani amekamatwa na nani ametekwa?
"Lakini maelekezo yaliyotolewa kwa kirefu ni kwamba wakati mwingine mtu
akiwa haonekani, polisi ndiyo sehemu ya kwanza ambayo inaulizwa na yapo
mazingira polisi haijatoa maelezo kwamba hawa watu wako wapi na mifano
imekwishatajwa.
"Mheshimiwa Bashe amekwenda mbali zaidi akisema kwamba kipo kikundi ambacho kinafanya kazi hiyo.
Na Mheshimiwa Joseph Mbilinyi na yeye ameeleza kwamba hili jambo sasa
limekuwa kama utamaduni kwa maana ya kwamba linatokea kila wakati na
akaenda mbele zaidi na kumshauri Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi (Nchemba) kwamba aweze kujiuzulu akiona inafaa.
"Kanuni ya 47 huwa ni lazima isomwe pamoja na (Kanuni ya) 48 kwa sababu 48 ndiyo inayoweka masharti ya matumizi ya Kanuni ya 47.
Sasa kwa kuwa Kanuni ya 48(4) nitaisoma, inasema hivi 'jambo lolote
litahesabiwa kuwa ni lenye maslahi kwa umma iwapo utatuzi wake
unategemea kuwa zaidi kuliko zile za utekelezaji wa kawaida wa sheria
peke yake.
"Masuala haya yaliyoulizwa na Mheshimiwa Bashe na pia yaliyoulizwa na
Mheshimiwa Mbilinyi yako chini ya utaratibu wa kisheria na Bunge hili
litashughulika na mambo ambayo ni yenye maslahi ambayo sheria haina
uwezo wa kuyatolea majibu.
Kwa sababu hiyo, sitalihesabu hili jambo kwa mujibu wa Kanuni ya 47(4)
kwamba ni jambo la dharura lakini ni jambo ambalo utaratibu wa kawaida
wa kisheria unaweza ukafanya kazi. Hayo ndiyo majibu yangu kuhusu
matumizi ya Kanuni ya 47.
Matukio ya kupotea, kutekwa na kuuawa kwa wanasiasa nchini ni nadra,
ingawa Juni 12, mwaka jana, chama cha ACt-Wazalendo kilidai kiongozi
wake mkuu, Zitto Kabwe, alikuwa hajulikani alipo kwa zaidi ya saa 12
huku akiwa anasakwa na Jeshi la Polisi.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment