MKAZI wa kijiji cha Karukekere, kata ya Namhura, wilayani Bunda, Mkoani Mara Godfrey Mgaya ambaye ni mzazi wa mwanafunzi aliyepewa ujauzito, amesema sasa binti yake anatishiwa kuuwawa na ndugu wa mtuhumiwa huyo iwapo atang’ang’ania suala hilo kulifikisha kwenye vyombo vya sheria.
Mgaya alisema hayo jana kwa njia ya simu wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, akisema kuwa mtoto wake anaishi kwa wasiwasi akihofia maisha yake.
Alisema licha ya Mkuu wa wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili kuagiza polisi wilayani humo, kuhakikisha wanamkamata mtuhumiwa Zephania Mfungo pamoja na mwenyekiti wa kijiji hicho Nyandago Magesa, aliyewazuia askari mgambo kumkamata mtuhumiwa huyo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni rafiki yake, lakini bado watu hao hawajakamatwa.
Mzazi wa mtoto huyo alisema kuwa binti yake ambaye ni mwanafunzi aliyekuwa anasoma kidato cha pili katika shule ya sekondari Muranda, iliyoko katika kata hiyo alifukuzwa shule mwaka jana kutokana na kupewa ujauzito na mwanaume huyo na sasa anaishi maisha ya wasiwasi kutokana na vitisho anavyopewa vya kutaka kuuwawa.
Alisema baada ya mtoto wake kupewa ujauzito na mtuhumiwa, alikwenda kutoa tarifa katika ofisi ya kijiji na ofisi ya kata, ambapo alipewa askari mgambo ili waweze kumkamata mtuhumiwa huyo, lakini mwenyekiti wa kijiji hicho aliwazuia mgambo hao kwa kile kinachodaiwa kuwa ni rafiki yake.
Aidha, alisema kuwa pamoja kufuatilia suala hilo ili mtuhumiwa huyo aweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani, kumekuwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na binti yake kutishiwa maisha yake kuwa iwapo akithubutu kusema ukweli hiyo mimba yake hawezi kujifungua salama na ataondolewa uhai wake.
“Sasa kibaya zaidi tangu tukio hilo, kuna ndugu yake mtuhumiwa amekuwa akimtishia mwanangu kwamba akitoa taarifa juu ya mimba yake hatajifungua salama, hata wanaweza kumkodishia gari iweze kumgonga wakati akitembea barabarani,” alisema.
Baada ya kubaini ndoto ya kusoma ya mtoto wake imekatishwa, alimuomba diwani wa kata hiyo, Jogoro Amoni kuingilia kati suala hilo, ambaye pia alitoa taarifa kwa Mkuu wa wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, aliyeagiza polisi wilayani hapa, kumkamata mtuhumiwa huyo pamoja na mwenyekiti wa kijiji hicho.
Kutokana na vitisho hivyo, baba mzazi wa binti huyo mwenye ujauzito wa miezi minne, aliamua kutoa taarifa kituo kidogo cha polisi Bulamba kuhusiana na vitisho hivyo.
Mgaya ameiomba serikali kumsaidia, ili watuhumiwa hao waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na pia alimuomba Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuingilia kati suala hilo, kwani watuhumiwa hao wamesababisha mtoto wake kukatisha masomo yake.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment