Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amerusha kombora
zito kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif
Hamad, huku akimwita mgombea wa urais wa kudumu aliyekata tamaa.
Pamoja
na hayo, Kinana amewataka Wazanzibari kuachana na maneno ya mitaani
kwani Uchaguzi Mkuu ulishamalizika na Dk. Ali Mohamed Shein
ameshaapishwa kuwa rais kwa mujibu wa sheria.
Kauli
hiyo aliitoa jana katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho za uchaguzi
mdogo wa ubunge Jimbo la Dimani zilizofanyika Maungani, nje kidogo ya
mji wa Unguja.
Alisema
CCM itaendelea kuchaguliwa na wananchi kwa sababu inatimiza wajibu wa
kuwatumikia wananchi, kutimiza matakwa na sera kwa mujibu wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM.
Kinana
alishangazwa na CUF kushindwa kutanua wigo wa demokrasia ndani ya chama
hicho na kuendelea kumshikilia mgombea urais mmoja wa kudumu kwa zaidi
ya miongo minne.
“Kuna
mgombea mmoja hapa Zanzibar ameanza kugombea urais tokea akiwa na miaka
30 na sasa ana miaka 80, toka akiwa bado kijana mbichi, sasa amekuwa
kikongwe na kupinda mgongo ila bado ana tamaa ya kuwania urais.
“Demokrasia
ndani ya chama chetu ni ya aina yake na kwamba kukubalika kwetu mbele
ya wananchi kunatokana na misimamo yetu inayotetea masilahi ya umma.
Hata demokrasia yetu ndani ya CCM kamwe haifanani na vyama vingine,” alisema Kinana huku akishangiliwa.
Kinana
alisema CCM ina umoja imara na katu hazuiwi mwanachama kuwania nafasi
ya uongozi na haina sifa ya kuwa na wagombea wa kudumu kama ilivyo CUF
ambayo tangu ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hadi sasa,
Katibu Mkuu wake Maalim Seif amekuwa mgombea wa kudumu.
Alisema
ushiriki wa wana CCM 25 ndani ya chama kuwania nafasi ya uteuzi wa
ubunge Jimbo la Dimani ni kielelezo tosha cha kuimarika kwa demkorasi,
na mgombea aliyepatikana anaungwa mkono na wanachama wote.
Alieleza
kuwa vikao vya CCM vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu
(CC) vilikutana na kupitisha jina la mgombea aliyeshinda kura za maoni,
huku CUF ikiwa kimya, ikishindwa hata kufanya vikao vyake kwa mujibu wa
katiba ya chama chao.
Akizumgumzia
kupwaya kwa dhana na misingi ya demokrasia ndani ya CUF, Kinana alisema
hivi sasa chama hicho kina wenyeviti watatu, ambao mmoja ni wa muda,
mwingine wa mpito na aliyebaki ni wa zamani
Aidha
Kinana aliwashangaa wanachama wa CUF ambao wanakubali kudanganywa
kirahisi kila siku na kuaminishwa ipo siku mgombea wao wa urais
aliyeshindwa uchaguzi atatangazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Rais wa
Zanzibar.
“Tuliambiwa
hapa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utafutwa, watakuja watu toka UN, mara
tukaelezwa wangekuja Jumuiya ya Ulaya, wakaambiwa washone nguo mpya
kusherehekea ushindi, huku siku zikitaradadi hakuna kinachotokea,” alisema.
Kinana
alisema viongozi wa CUF hawana uwezo wowote wa kuwatumikia wananchi na
kuwaletea maendeleo kwani walibahatika kuingia katika Serikali ya Umoja
wa Kitaifa, lakini bado hakuna walichofanya.
“Kama
ni mkate CUF walipata nusu na CCM nusu, wakashika wizara makini za
Biashara na Viwanda, Katiba na Sheria, Habari na Utamaduni, Mawasiliano
na Miundombinu, lakini kutokana na wao kuwa dhaifu, hawakumudu hata
kujenga kiwanda kidogo,” alisema.
Kinana
aliwaomba wananchi wa Dimani kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Juma Ali
Juma kwa sababu ni makini, mchapakazi na mwepesi wa kuwatumikia
wananchi.
Akihutubia
katika mkutamo huo wa uzinduzi wa kampeni, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM,
Balozi Seif Ali Idd, aliwaeleza wananchi wa Dimani kuwa si sifa ya
wagombea wa CUF kuwatumikia wananchi na mfano mzuri ni katika majimbo ya
Pemba.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment