WAKATI uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma unakamilika leo, Ikulu
imemtwisha mzigo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kuwa ndiye mhusika
mkuu wa suala hilo.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Machi 20, mwaka huu na Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk.
Laurian Ndumbaro, uhakiki wa vyeti vya elimu na taaluma pamoja na namba
za mitihani kwa watumishi wa umma ulioanza Machi 12, mwaka jana,
utakamilika rasmi leo.
Katika tangazo hilo, Dk. Ndumbaro anaeleza kuwa uhakiki huo haujalenga
kumkoma mtumishi wa umma bali kuhakikisha kunakuwa na watumishi wenye
sifa stahiki na kitaaluma na kitaalamu ili kutoa huduma zilizo bora na
kwa weledi kwa wananchi.
"Serikali inasisitiza kuwa mtumishi wa umma atakayeshindwa kutumia muda
uliotolewa kuwasilisha nakala za vyeti au namba za mitihani kwa wale
waliopoteza, atakuwa amejiondoa mwenyewe katika ajira serikalini,"
linaeleza tangazo hilo ambalo Florence Temba, Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Utumishi, aliithibitishia Nipashe
kuwa ni lao.
Alipoulizwa na Nipashe kama uhakiki huo unawahusu pia wateule wa Rais,
Temba alisema ni kwa watumishi wote wa umma, lakini akadai kuwa vyeti
vya wateule wa Rais vinahakikiwa na Ofisi ya Rais Tamisemi.
Nipashe ilipomtafuta Simbachawene kuzungumzia suala hilo, alidai masuala
ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wote wakiwamo wateuliwa unafanywa na
Wizara Nchi, Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
"Utumishi ndiyo wanaofanya hiyo kazi ya uhakiki na utunzaji wa taarifa
zote za watumishi na wateuliwa, hivyo siwezi kujibu hilo suala," alisema
Simbachawene.
Kutokana na majibu hayo ya Simbachawene, Nipashe ilimtafuta tena Temba
ambaye alisisitiza kuwa wanaohakikiwa na wizara yao ni watumishi wa umma
na kwamba vyeti vya elimu na kitaalamu vya wateule huwa wanavipeleka
kwenye mamlaka husika za uteuzi.
Akizungumza na Nipashe kwa simu jana mchana kuhusu uhakiki wa vyeti vya
elimu na kitaalamu vya wateule wa Rais, Mkurugenzi wa Kitengo cha
Mawasiliano Ofisi ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, alisema Simbachawene
ndiye anayepaswa kuzungumzia uhakiki huo.
"Muulize huyo huyo Simbachawene. Vyeti vinahakikiwa huko huko Tamisemi.
Simbachawene yuko Ofisi ya Rais Tamisemi ambako mambo ya uhakiki (kwa
wateule) yanafanyikia huko," alisema Msigwa.
Jitihada za Nipashe kutaka kuzungumza na Simbachawene jana hazikuzaa
matunda baada ya simu yake ya mkononi kutopokewa na hakujibu ujumbe
mfupi wa maandishi tuliomtumia kuhusu suala hilo.
Kwa miaka mingi, ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) zimekuwa zikionyesha upotevu wa mabilioni ya shilingi
kutokana na malipo ya watumishi hewa.
Kutokana na changamoto hiyo, Machi 12, mwaka jana, serikali ya awamu ya
tano ilielekeza kufanyika kwa uhakiki wa watumishi hewa kwa kukagua
vyeti vya kazi wanavyotumia ili kuwe na usimamizi na uwajibikaji.
Juni 22, mwaka jana, Rais John Magufuli akatangaza kusitisha ajira serikalini ili kuhakiki watumishi wote wa umma.
Kutokana na uamuzi huo, nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa serikali
na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali vya likizo ya bila malipo
vilisitishwa kwa muda hadi uhakiki utakapokamilika.
Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, baada ya kusitishwa kwa ajira, taarifa
zilisambazwa katika halmashauri zote na idara za serikali kutekeleza
maelekezo yaliyotolewa na wizara Juni 13, jana kusitisha ajira hadi pale
uhakiki utakapokamilika.
Kutokana na uamuzi huo, ajira 71,496 zilizokuwa zimepangwa kutolewa
mwaka huu wa fedha na serikali kwenye sekta mbalimbali ikiwamo elimu,
afya na viwandani hazijatolewa, huku zikiwa zimebaki siku 91 kabla ya
kumalizika kwa mwaka wa bajeti.
Kwa mujibu wa Temba, sekta ya elimu mwaka huu ilitarajiwa kuwa na ajira
mpya 28,957, afya 10,870, kilimo 1,791, mifugo 1,130, huku maeneo
mengine ambayo hayakutajwa, yakitarajiwa kuwa na ajira 28,748.
Ofisa huyo wa serikali aliiambia Nipashe kuwa hadi kufikia Agosti 2016,
watumishi 839 walikuwa wamefikishwa kwenye mamlaka za kiuchunguzi
likiwamo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa
(Takukuru) kwa ajili ya kutoa maelezo kabla ya kufikishwa mahakamani
kutokana na kunufaika kwa kujipatia fedha kupitia watumishi hewa.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015, serikali yake
imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kukomesha vitendo vya ufisadi vikiwamo
hivyo vya kuwapo kwa malipo ya kila mwezi yanayokwenda mifukoni mwa
maofisa wachache wasio waaminifu badala ya fedha hizo kuelekezwa katika
shughuli nyingine za maendeleo.
Credit - Nipashe
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa