JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetaja sababu tatu za
kumkamata aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Mkuranga, Adam
Malima, katika tukio lililombatana na kufyatua risasi tatu angani.
Mtuhumiwa huyo jana alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam kujibu tuhuma zinazomkabili na kutetewa na Wakili Peter
Kibatala.
Hatua hiyo imekuja baada ya kusambaa mitandaoni picha za video
zikionesha gari aina ya Toyota Land Cruiser namba T 296 ATW, ambalo
liliegeshwa pembeni karibu na hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es
Salaam, wakashuka askari wawili – mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU) na mwingine polisi wa kawaida.
Akizungumzia suala hilo jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema
tukio hilo lilitokea juzi saa sita mchana Masaki karibu na ofisi za
Ubalozi wa Canada, ambapo mfanyakazi wa kampuni ya Priscane Business
Enterprises, alikuta gari la Malima limeegeshwa sehemu isiyotakiwa, huku
akisisitiza dereva wa gari alipotakiwa alipeleke gari hilo yadi
alikaidi na kulirudisha kwa nguvu lilipokuwa.
“Mfanyakazi wa Priscane alilikuta gari la Malima likiwa na dereva
aliyeambiwa ameegesha sehemu isiyoruhusiwa, lakini cha kushangaza
alikaidi ndipo mvutano ukaanza kati yake na mfanyakazi huyo na kulazimu
polisi kuingilia kati,” alisema Kamanda Sirro.
Katika video ya tukio hilo, askari wa FFU baada ya kushuka kwenye gari
hilo alionekana akinyanyua bunduki na kufyatua risasi angani, kabla
mwenzake kumfuata na kumshika kifuani na kutaka kumrudisha kwenye gari.
Tukio liliendelea kwa askari aliyemfuata mwenzake kumfuata Malima na
kuzungumza naye, lakini wakati wakiendelea na mazungumzo, yule askari
aliyefyatua risasi pia alimfuata na kumsukuma mara mbili waziri huyo wa
zamani, kisha kuinua juu bunduki na kusikika akitamka:
“Kwa nini hamheshimu Serikali nyie, mzee heshimu Serikali, mimi nimewekwa kuitumikia Serikali, siwezi kudharaulika.”
Katika video hiyo pia ilisikika sauti ya mtu ambaye hakuonekana akitamka: “Huna mamlaka, huna mamlaka ya kutishia.”
Wakati hayo yakiendelea, Malima alionekana kujibizana na askari hao
akiwa ameweka mikono mfukoni mwa suruali yake, huku mmoja wa askari hao
aliyeonekana akimsihi mwenzake aende kwenye gari akitamka: “Poti, Poti,
Poti ee!”
Katika mkutano wake na wanahabari, Kamanda Sirro alisema Malima
alipotoka nje ya Ubalozi huo, askari walimwambia gari lake linatakiwa
liende yadi kwa sababu lilikiuka sheria za maegesho, lakini alionekana
kukaidi hali iliyolamzimu askari huyo kufyatua risasi tatu angani.
Alisema licha ya amri ya askari, Malima aliendelea kukaidi huku akitamka
kuwa yeye amefanya kazi na viongozi wakubwa, hali iliyomlazimu askari
kufyatua risasi nyingine.
Sirro alisema: “Kelele za watu waliokuwa wakizomea, zilichangia askari
kutumia busara kupiga risasi hizo angani ili kuwatawanya na endapo
wangewaacha Malima na dereva wake, ingechangia kuwaaminisha wananchi
kuwa polisi wameshindwa kufanya kazi yao.”
Alitaja sababu nyingine kuwa ni mazingira hatarishi yaliyomlazimu askari
huyo kufyatua risasi, kulingana na wakati na kwamba askari wangeondoka
eneo la tukio bila kuwakamata, wangeshitakiwa kwa woga.
Aidha, alisema waziri huyo wa zamani alifikishwa mahakamani kujibu
mashitaka yanayomkabili yakiwamo ya kuzuia polisi kufanya kazi zao,
kujeruhi na kukaidi amri.
Mahakamani
Malima na dereva wake, Ramadhani Kingwande walipandishwa kizimbani
kujibu mashitaka ya kuzuia polisi kufanya kazi yake na kujeruhi.
Kesi hiyo inawakutanisha Wakili Kibatala na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono.
Wakili Mwanaamina alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage
kuwa Malima ambaye alikuwa Mbunge wa Mkuranga na dereva wake
wabnakabiliwa na mashitaka mawili.
Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo Mei 15 Masaki Kinondoni, Dar es Salaam.
Wakili huyo alidai kuwa Kingwande kwa nia ya kukataa kukamatwa kutokana
na kuegesha vibaya gari lake namba T 587 DDL, alimjeruhi Mwita Joseph
ambaye ni Ofisa Operesheni wa kampuni ya Priscane Business Enterprises
na kumsababishia maumivu makali.
Wakili huyo alidai kuwa Malima alitenda kosa la shambulio, Mei 15
Masaki, wakati akimzuia dereva wake kukamatwa baada ya kutuhumiwa
kutenda kosa barabarani.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo, Malima alimzuia askari Polisi namba H 7818
Konstebo Abdu kufanya kazi halali ya kumkamata Kingwande aliyefanya
makosa ya kumshambilia Joseph.
Washitakiwa walikana mashitaka hayo na upande wa mashitaka ulidai kuwa
upelelezi wa kesi haujakamilika na hawana pingamizi la dhamana.
Wakili Kibatala aliiomba Mahakama kutoa masharti nafuu ya dhamana kutokana na asili ya mashitaka hayo.
Pia alidai Malima ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo ni mtu
anayetambulika katika jamii kwa kuwa alikuwa Mbunge na Naibu Waziri.
Hakimu Mwijage aliwataka washitakiwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja
atakayesaini dhamana ya Sh milioni tano. Washitakiwa hao waliachwa huru
baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Kesi iliahirishwa hadi Juni 15.
Hata hivyo, Wakili Kibatala alidai mahakamani hapo kuwa katika tarehe
ijayo atawasilisha pingamizi kwamba mashitaka ya pili yanayomkabili
Malima hayaendani na maelezo yake.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza HapaFollow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment