Wakati
Rais John Magufuli alitishia kubadili fedha za Tanzania katika juhudi
za kuwadhibiti watu wanaodaiwa kuficha fedha, Waziri Mkuu wa India,
Narendra Modi ametangaza kuziondoa kwenye mzunguko noti za Rupia 500 na
1,000.
Akizungumza
katika mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika Septemba Mosi
katika Ukumbi wa Mlimani City, Rais Magufuli alisema kwa mamlaka
aliyonayo anaweza kuamua kubadili fedha ili zile zinazofichwa, watu hao
wakose mahali pa kuzipeleka.
Alisisitiza
kwa kusema kauli hiyo ni mahsusi kwa watu walioficha fedha katika
majumba yao na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja ili fedha hizo
ziingie katika mzunguko.
Rais
Magufuli alisema katika utawala wake fedha za bure hazitakuwapo kwa
sababu zilizokuwapo awali zilitokana na fedha za wizi kutoka serikalini
ambazo kwa sasa zimedhibitiwa.
Alisema kwa mwendo anaokwenda nao sasa ni ngumu kwa mwananchi kupata fedha bila kufanya kazi.
Habari
kutoka India zinasema Waziri Mkuu Modi alitangaza hatua hiyo ya
kushangaza kwenye runinga Jumanne usiku kuwa ni mojawapo ya harakati za
kukabiliana na ufisadi na ukopeshaji wa fedha haramu.
Modi
alisema noti zote za Rupia 500 na 1,000 “hazitakuwa fedha halali
kuanzia usiku wa manane leo” na kwamba “zitabaki kuwa makaratasi yasiyo
na maana.”
Hata
hivyo, alisema noti nyingine za Rupia 100, Rupia 50, Rupia 20, Rupia
10, Rupia 5, Rupia 2 na sarafu zote zitaendelea kuwa na thamani.
“Ulanguzi
wa fedha na ufisadi ndiyo vikwazo vikuu katika kukabiliana na
umasikini,” alisema Modi na kuongeza: “Watu wataweza kubadilisha noti
zao za zamani na mpya katika benki kuanzia Novemba 10 hadi Desemba 30 na
kwamba fedha hizo hazitatumika tena.”
Benki
zilifungwa jana huku huduma za mashine za kutoa pesa za ATM
zikisitishwa. Badala yake noti mpya za Rupia 500 na 2,000 zitawekwa
katika mfumo wa fedha kuchukua nafasi ya zilizoondolewa.
Tangazo
hilo lilisababisha mtafaruku kwenye vituo vya mafuta na maeneo mengine
ya biashara kwani wauzaji wa rejareja walikuwa wakikataa kupokea noti
hizo huku mashine za kutolea fedha zikifungwa. Katika viwango vya
ubadilishaji fedha noti ya Rupia 500 ni sawa na Sh16,000 na Rupia 1,000
ni sawa na Sh32,000.
Wateja
watakuwa na uwezo wa kubadili noti hizo ili wapewe mpya au kuziweka
kwenye akaunti, lakini watatakiwa kujieleza mamlaka ya mapato
walivyozipata.
0 comments:
Post a Comment