Mahakama Kuu Kanda ya Tabora inayoendelea mjini Kigoma, imemtia hatiani
David Kafulila na kumtaka kulipa gharama kutokana na kukiuka kanuni ya
kuwasilisha hati za kiapo mahakamani, zikiwa zimethibitishwa kama Sheria
ya Makosa ya Uchaguzi inavyoelekeza.
Hata hivyo, kiwango cha
faini anachotakiwa kulipa hakikutajwa. Kosa hilo halikuzuia ushahidi
wake kupokewa upya mahakamani hapo.
Katika kesi hiyo
aliyoifungua kupinga ushindi wa Hasna Mwilima (CCM) kuwa Mbunge wa
Kigoma Kusini, Kafulila aliyegombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi
analalamika kupokwa ushindi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni
Mwilima ambaye ni mshtakiwa namba moja wakati msimamizi wa uchaguzi wa
jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni washtakiwa namba mbili na
tatu.
Jaji wa Mahakama Kuu, Ferdinand Wambali alisema Kafulila
aliwekewa pingamizi na mawakili wa utetezi wakimlalamikia kuwasilisha
hati ya kiapo iliyokiuka kanuni za uwasilishwaji kwa mujibu wa sheria.
Katika hoja yao mawakili hao waliiomba Mahakama hiyo kutozipokea hati hizo.
Jaji
alisema Kafulila hakutekeleza matakwa ya kisheria ambayo yanaagiza
anayewasilisha haki za viapo kuhakikisha kuwa zimethibitishwa kabla, kwa
ajili ya shahidi kuanza kutoa ushahidi wake.
“Pingamizi la
wajibu maombi linakubaliwa kwa upande mmoja, lakini pia linaachwa.
Uamuzi wa Mahakama ni kwamba mleta maombi awasilishe upya hati za kiapo
mbele ya Mahakama zikiwa zimethibitishwa,” alisema jaji.
0 comments:
Post a Comment