Kiu
ya wabunge kujadili sakata la utekelezwa mbovu wa mkataba baina ya
Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enteprises Limited, imezimwa baada
Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuiagiza Serikali kukamilisha utekelezaji
wa mradi huo ndani ya miezi mitatu ijayo.
Kwa
muda mrefu, wabunge walikuwa wakisubiri ripoti ya uchunguzi kutoka
Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) ili waweze kujadili kwa kina
sakata hilo linalohusisha mradi wa Sh37 bilioni wa kufunga vifaa vya
kielektroniki vya kuchukua alama za vidole (AFIS).
Mapema
Aprili mwaka huu, wakati PAC ikipitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka ulioshia Juni 30, 2014
ilibaini kuwa Lugumi ilikuwa imefunga mashine katika vituo 14 tu kati ya
108 ilivyotakiwa kuvifunga wakati ikiwa imeshapokea asilimia 99 ya
malipo yote.
PAC
ilimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani apeleke taarifa ya
utekelezaji wa mradi huo ambayo aliipeleka Aprili 18 na kubaini kuwa
vifaa hivyo vilifungwa katika vituo 153 pamoja na makao makuu ya
polisi.
Kutokana
na utofauti wa takwimu za CAG na PAC iliunda kamati ndogo kufanya
uhakiki wa vifaa vya AFIS na sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa mradi,
huku wengi wakitarajia ripoti hiyo ingejadiliwa bungeni.
Katika
sakata hilo, wabunge walimtuhumu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Charles Kitwanga kuwa na masilahi kwa madai kuwa alikuwa mmoja wa
wanahisa wa kampuni ya Infosys iliyoshirikishwa kwenye mradi huo na
kushinikiza ajiuzulu kupisha uchunguzi.
Hata hivyo, Kitwanga alitimuliwa kazi kwa kosa jingine la kuingia bungeni kujibu maswali ya wizara yake akiwa amelewa.
Jana,
Dk Tulia alitumia kanuni 117(17) kukabidhi matokeo ya uhakiki huo kwa
Serikali, yakiwemo maoni, ushauri, mapendekezo ya namna ya kutatua
changamoto zilizoanishwa na taarifa ya kamati ya PAC na kutoruhusu
mjadala kwa wabunge
Dk
Tulia alieleza kuwa amefanya uamuzi huo baada ya kupokea taarifa hiyo
na kuangalia maudhui yake, kuzingatia matokeo ya uhakiki huo uliofanywa
na kamati ndogo na PAC kujiridhisha uwepo wa vifaa hivyo, ukiacha kasoro
zilizojitokeza.
Pia,
alisema suala hilo si jipya kwa kuwa linatokana na hoja ya ukaguzi wa
miaka ya nyuma na kilichokuwa kimebaki ni vifaa hivyo kufanya kazi.
“Naagiza sasa kwamba Serikali ihakikishe mfumo huu
unafanya kazi ndani ya miezi mitatu kuanzia leo (jana) ili kuboresha
uwezo wa Jeshi la Polisi kuwa na utambuzi wa haraka wa wahusika wa
matukio ya kihalifu katika vituo vyote nchini,” alisema huku
akishangiliwa.
Dk Tulia aliitaka pia Serikali kuyapatia ufumbuzi haraka masuala yote yaliyobainika kuwa na dosari za kiutendaji.
Dk Tulia aliitaka pia Serikali kuyapatia ufumbuzi haraka masuala yote yaliyobainika kuwa na dosari za kiutendaji.
Alisema
ameielekeza kamati ya PAC kuhakiki maagizo aliyoyatoa kwa Serikali na
baada ya uhakiki huo itoe taarifa bungeni wakati ikiwasilisha taarifa
yake ya mwaka.
“Natarajia kuwa suala hili sasa litafikia mwisho na CAG
atafunga hoja yake baada ya kujiridhisha na utekelezaji wa maagizo
niliyoyatoa,” alisema Dk Tulia.
Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly alisema
walishamaliza kazi yao baada kumkabidhi Naibu Spika ripoti hiyo, kama
kanuni zinavyotaka na kwamba yeye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho.
Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ndogo ya kuchunguza suala hilo,
Japhet Asunga alisema baada ya uchunguzi, walibaini vituo 15 tu kati ya
153 ndivyo vimeunganishwa na mfumo wa taarifa za polisi.
Asunga, ambaye
ni mbunge wa Vwawa (CCM), alimwambia mwandishi wetu kuwa kamati ilibaini
kuwa vifaa vyote vya AFIS vilivyokuwapo katika vituo vimetelekezwa bila
kuunganishwa katika mfumo wa mtandao.
Alisema sehemu nyingine walikuta
vifaa vimetupwa huku vingine vimeharibika kwa sababu vimekaa muda mrefu
kama wino wa printa umeisha muda wake.
“Tumeagiza Serikali ichukue hatua
stahiki kuhakikisha vifaa vinatumika na kuwaadhibu wote waliochelewesha
na nani hakufanya kazi ipasavyo.
“Ndiyo maana Naibu Spika baada kupima
maagizo yaliyotolewa ameona Serikali ianze kuyafanyia kazi mapungufu
badala ya kusubiri kuyawasilisha Septemba. Naona busara imetumika,” alisema
Asunga.
Alisema kamati haina tatizo na maazimio ya miezi mitatu
aliyotoa Spika kwa kuwa ndiyo mapendekezo yao na kwamba PAC wao awali
walipendekeza miezi sita.
0 comments:
Post a Comment