Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amewahakikishia wafanyabiashara wa Rwanda kuwa bandari ya Dar es salaam
ni salama kwa wao kupitisha mizigo na ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania
inaendelea kuchukua hatua za kuiboresha bandari hiyo na kurahisisha
biashara kati ya nchi hizi mbili.
Rais
Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 01 Julai, 2016 alipokuwa
akizungumza na wananchi wa Tanzania na Rwanda kupitia vyombo vya habari
wakati wa ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe.
Paul Kagame inayofanyika kwa siku mbili hapa nchini.
Dkt.
Magufuli amesema pamoja na kuchukua hatua kadhaa za kuboresha bandari
ya Dar es salaam kwa manufaa ya wafanyabiashara wanaopitisha mizigo,
Tanzania imeamua kuipatia Rwanda eneo la kujenga bandari kavu kwa ajili
ya mizigo ya wafanyabiashara wake na pia Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA) itafungua ofisi Mjini Kigali nchini Rwanda ikiwa ni juhudi za
kurahisisha na kuongeza biashara kati ya nchi hizi mbili.
Aidha,
Rais Magufuli amesema kwa kutambua umuhimu wa reli ya kati kwa uchumi
wa Tanzania na Rwanda, Tanzania imetenga shilingi Trilioni moja katika
bajeti mpya ya serikali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli hiyo kwa
kiwango cha kisasa yaani “Standard Gauge” na kwamba ni matarajio kuwa
wadau wengine wa maendeleo watajitokeza kuunga mkono juhudi za ujenzi wa
reli hiyo hapa Tanzania na nchini Rwanda huku akidokeza kuwa China
imeonesha nia ya kuunga mkono mradi huo.
Dkt.
Magufuli ameongeza kuwa serikali yake pia imechukua hatua madhubuti za
kulifufua shirika la ndege la Taifa na kwamba tayari mipango imefanywa
kuhakikisha ndege mbili aina Bombadier Q400 zinanunuliwa na zitatua hapa
nchini kabla ya mwisho wa mwezi Septemba Mwaka huu 2016.
Kwa
upande wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame amemshukuru Rais
Magufuli kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na
amemhakikishia kuwa serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi
ushirikiano uliopo kati ya nchi yake na Tanzania kwa manufaa ya wananchi
wa nchi zote mbili.
Majira
ya jioni Rais Kagame akiwa na mwenyeji wake Rais Magufuli, amefungua
rasmi maonesho ya 40 ya kimataifa ya Biashara Dar es salaam
yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo Barabara ya Kilwa,
Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es salaam.
Akizungumza
kabla ya kuzindua rasmi maonesho hayo, Rais Kagame ametoa wito kwa
Tanzania na Rwanda pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika
Mashariki kushirikiana na sekta binafsi katika kutumia fursa nyingi za
kibiashara zilizopo baina yake na kuwaletea manufaa wananchi.
Nae
Rais Magufuli amezipongeza nchi takribani 30 zilizojitokeza kushiriki
katika maadhimisho hayo zikiwemo kampuni zaidi ya 650 na wadau zaidi ya
2,000 na amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki zenye watu takribani milioni 165 na nchi nyingine za Jumuiya
ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) kuongeza biashara baina yake kwa
kuwa hivi sasa kiwango cha biashara baina ya nchi hizo ni cha chini mno.
Baada
ya kufungua maonesho hayo, Rais Kagame na mwenyeji wake Rais Magufuli
wametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya bidhaa na huduma katika
viwanja vya Sabasaba na baadaye Rais Kagame atahudhuria dhifa ya Kitaifa
iliyoandaliwa na mwenyekiji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini
Dar es salaam.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
01 Julai, 2016
0 comments:
Post a Comment