ALIYEKUWA Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta, ameondolewa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi baada ya Serikali kugoma kumlipia kodi ya pango.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, mwanasiasa huyo mashuhuri, aliondolewa katika nyumba hiyo iliyopo Masaki, Dar es Salaam na kulazimika kuanza kuhamisha vyombo vyake tangu Ijumaa ya Julai 8, mwaka huu.
Kwa
muda wote tangu akiwa Spika wa Bunge, Serikali ilikuwa inalipa kiasi
cha dola 8,000 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh milioni 12 kwa ajili ya
nyumba hiyo.
Sitta
ambaye baadaye alikuwa waziri katika Wizara ya Afrika Mashariki pamoja
na Uchukuzi, aliendelea kuishi katika nyumba hiyo kwa nafasi yake.
Kwa
mujibu wa kijana aliyekuwa nyumbani hapo, alisema walianza kuhama tangu
mwishoni mwa wiki iliyopita na wanaendelea kuhama kwa kuhamisha vitu
kidogo kidogo.
“Ni
kweli mzee amehama hapa, tangu Ijumaa tulikuwa tunahamisha vyombo
taratibu na sijui kama Serikali imegoma kulipa kodi ama la, ila sasa
amehamia jirani tu hapo Mtaa wa Manzese, hapa hapa Masaki.
“Nasikia nyumba imepata mpangaji mpya ndiyo maana wanahama,” alisema.
Alipotafutwa
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen
Mwandumbya, ili kuzungumzia hilo, alimtaka mwandishi kuwatafuta Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Fedha.
Alipotakiwa
kutoa ufafanuzi wa utaratibu wa malipo kwa maspika wastaafu, ikiwa ni
pamoja na matunzo na nyumba wanazoishi, Owen alisema Bunge halihusiki na
stahiki zozote za wastaafu kwa mujibu wa sheria.
“Watafute
Utumishi na Wizara ya Fedha, wao ndio wahusika, Ofisi ya Bunge
haihusiki na stahiki zozote za wastaafu kwa mujibu wa sheria, isipokuwa
Utumishi na Wizara ya Fedha ndio wahusika,” alisema.
Alipotafutwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angellah Kairuki, alisema hana taarifa hizo za kuondolewa kwa Sitta
hivyo atafuatilia.
Hata
hivyo, alipotafutwa tena kupitia simu yake ya kiganjani, Kairuki
alimtaka mwandishi kuwatafuta Hazina, kwamba ndio wanaoweza kulisemea
jambo hilo.
“Naomba uwatafute Hazina wakupe ufafanuzi, halafu baadaye urudi kwangu,” alisema Kairuki.
Alipotafutwa
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kupitia simu yake ya
kiganjani, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema: “Ufafanuzi kuhusu malipo kwa viongozi wastaafu unatolewa kwa viongozi husika na si kwa vyombo vya habari.”
Hali
hiyo ya Sitta, imekuwa ni tofauti na aliyekuwa Spika wa Bunge la 10,
Anne Makinda, ambaye Serikali kupitia Bunge iligharimia matengenezo ya
nyumba yake iliyoko Kijitonyama, Dar es Salaam, ambako ujenzi wake
ulikumbana na lawama kali za wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo.
Spika
Makinda alilaumiwa na majirani zake kwa kusababisha usumbufu baada ya
kuziba njia inayopita katika eneo hilo kwenda maeneo ya Sinza.
Kwa
mujibu wa Margaret Sitta ambaye ni mke wa Samweli Sitta na Mbunge wa
Urambo, alisema kuwa walikuwa wakiishi kwenye nyumba hiyo ya Serikali
kwa kuwa mumewe alikuwa Waziri wa Uchukuzi, lakini Baraza la Mawazili
lilivunjwa tangu mwaka jana hivyo walipaswa kuhama.
Chanzo: Mtanzania
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment