Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’, juzi Jumamosi alijikuta akipoteza pambano lake la Ubingwa wa Dunia (WBC) dhidi ya Mjerumani Toni Kraft licha ya kudaiwa kumpiga mpinzani wake vya kutosha.
Katika
pambano hilo la raundi kumi lililofanyika kwenye Ukumbi wa Ballhaus
Forum, Munich, Ujerumani, Mbabe alionekana kumdhibiti vilivyo Mzungu
huyo kwa kumpelekea makonde mazito kabla ya kumdondosha chini katika
raundi ya tatu kufuatia kumchapa konde kali la mkono wa kulia, hali
iliyosababisha ahesabiwe mpaka kumi lakini aliweza kuokolewa na kengele
ya mapumziko.
Baada
ya kipondo hicho, Mzungu huyo alianza kucheza kwa kukimbia muda mwingi
ulingoni huku akipokea ‘vikombe’ kutoka kwa Dullah Mbabe hadi kumaliza
raundi kumi na majaji wawili kumpa ushindi Mjerumani huyo hali
iliyosababisha mashabiki waliojitokeza kwenye pambano hilo kuamini kuwa
Mzungu mwenzao hakustahili kushinda pambano hilo.
Akizungumza
mara baada ya pambano hilo moja kwa moja kutoka katika Jiji la Munich,
Ujerumani, Mbabe alisema amesikitishwa na matokeo hayo, kwani majaji
walimpendelea mpinzani wake, licha ya kumpiga katika raundi zote.
“Kiukweli
nimepoteza pambano langu kimizengwe, majaji wamempa mpinzani wangu
ushindi wa jumla kwa tofauti ya pointi mbili, kitu ambacho kimepingwa
hata na mashabiki wa ngumi huku Ujerumani, wengi wao ni Wazungu, kwa
kuwa kila mtu ameona nilivyokuwa namshughulikia bondia wao.
“Nilimpiga
ngumi kali ya kulia akaenda chini lakini alihesabiwa mpaka nane na
akaweza kuendelea na pambano kwa ujanja kwani muda mwingi nilikuwa nampa
vitasa vizito,” alisema Mbabe.
0 comments:
Post a Comment